Thursday, 2 August 2007

Habari kutoka Uhuru

JK alonga:
CCM haina viongozi wa kudumu Maslahi ya Chama kwanza, urafiki baadaye
Anayetaka kumng’oa mgombea athibitishe mabaya yake
NA MWANDISHI MAALUM, DODOMA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete amewataka wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kuitumia vyema na kwa haki dhamana waliyopewa ya kupitisha ama kutopitisha majina ya wanachama walioomba nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama.Alisema asingependa kuona kikao kikubwa kama hicho, kinakuwa kikao cha watu waliokula njama kumwondoa mtu fulani bila ya kutoa sababu zinazoridhisha za kumtoa mtu huyo. Alionya kwamba, kwa kufanya hivyo ni kuvunja heshima ya kikao hicho.Rais Kikwete alikuwa akizungumza katika siku ya kwanza ya kikao cha NEC, ambacho moja ya jukumu lake kubwa ni kupitisha majina ya wanachama walioomba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama. “Anayetaka kumwondoa mtu ajiandae kututhibitishia ndani ya kikao hiki sababu za kutaka aondolewe si kupinga tu, tuambie hicho unachojua wewe, uturidhishe, hii ndio misingi ambayo sisi katika Kamati Kuu tuliitumia na ndiyo maana tukachukua siku tatu, ningependa na ninyi wajumbe mzingatie pia,” alisisitiza.Aliwaasa wajumbe hao wa NEC kupitisha majina kwa kuzingatia sifa na uwezo wa mtu kukitumikia Chama. “Mpitisheni mtu kwa sifa za kufaa kuwa kiongozi wa kukitumikia Chama na wananchi, usimpitishe mtu kwa sababu tu ni rafiki yako, zingatieni maslahi ya Chama kwanza si yako”.Aliwataka wanachama wa CCM kutoogopa ushindani katika kuwania nafasi za uongozi, kwa sababu hakuna kiongozi wa kudumu ndani ya Chama, na kila mmoja lazima atambue nafasi ya uongozi anayoshika ina ukomo wake. “Lazima utambue kama wewe ni mwenyekiti wa wilaya, wa mkoa, mjumbe wa NEC au Rais lazima utambue kwamba uongozi wako ni wa miaka mitano.“Utambue kwamba nafasi hiyo iko wazi kwa mwanachama yeyote wa CCM… anao uhuru wa kuomba nafasi hiyo na wala si dhambi, tafadhalini sana ni lazima tulitambue hilo,” alisema.Aliongeza: “Ukiwa kwenye kiti ungetamani sana watu wasijitokeze kuomba nafasi hiyo, lakini hakuna namna lazima watu wajitokeze, tukilitambua hilo kwamba baada ya miaka mitano unakwenda kushindana, hakutakuwa na sababu ya kugombana na mtu, hutakuwa na sababu ya kumtafuta mchawi, wala hutauliza huyu naye anatafuta nini, anatafuta hicho ulichokitafuta wewe”.Rais Kikwete aliwataka viongozi ambao nafasi zao zinawaniwa na watu wengine, badala ya kugombana na wale wanaowania nafasi hizo, wajiulize kwa nini watu wengine wanaitaka nafasi yake, watamshinda kwa hoja zipi na kama kasoro basi azifanyie kazi.“Ukikosana na mtu nenda kamwombe radhi tu ili mmalize matatizo yenu na wale unaoishi nao katika eneo lile, kwa sababu hata ukitembea na orodha ya wabaya wako na ukidhani utawakomesha haitakusaidia kitu, wanademokrasia lazima tulitambue hilo kwamba kuna uchaguzi na kuna kushindana,” alisema.Aliwataka wanachama wote wanaoomba nafasi za uongozi ndani ya Chama, wajinadi wao wenyewe kwa sifa na uwezo wao, badala ya kusingizia kwamba wao wametumwa na kiongozi fulani wa ngani za juu.Akizungumzia mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM, aliwakumbusha wanachama kwamba Chama Cha Mapinduzi ndiyo Chama tawala, na kwa hiyo viongozi wake katika ngazi yoyote ile ni sehemu ya utawala.Alifafanua kwamba ndiyo maana mchakato wa uchaguzi unapoanza ndani ya Chama, kila mwananchi anaufuatilia kwa makini, vikiwamo vyama vingine vya siasa.

Kigogo apigwa ‘stop’ uchaguzi wa CCM
Madiwani watano wavuliwa uanachama
NA SIMON NYALOBI, DODOMA
MBUNGE wa zamani wa Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo amezuiwa kugombea nafasi za uongozi katika Chama Cha Mapinduzi kutokana na mwenendo wake kuwa mbaya.Taarifa ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Aggrey Mwanri, iliyotolewa mjini hapa jana, ilisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, imemvua Nyimbo haki ya kuchaguliwa katika uongozi wa Chama, baada ya kuthibitika kuwa tabia na mwenendo wake vinamfanya kupoteza haki hiyo.Nyimbo ambaye alichukua fomu kuwania uenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, taarifa ilieleza aliwahi kupewa adhabu ya karipio kwa tabia na mwenendo huo, lakini hakujirekebisha.“Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imemvua haki ya kuchaguliwa katika uongozi wa Chama... atatumikia adhabu hiyo kwa miezi 24,” ilifafanua taarifa hiyo.Katika hatua nyingine, taarifa hiyo ilisema madiwani watano wilayani Tunduru wamefukuzwa uanachama kwa tuhuma mbalimbali.Waliofukuzwa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tunduru, Burhan Makonje, Zuhura Mafutari, Suleiman Chisopa, Aindi Darwesh na Halima Luambano.Wakati huo huo, Kamati Kuu iliwateua wagombea watatu wa nafasi ya meya katika Manispaa ya Arusha, ambao ni Anaelson ole Joel, Laurence Heddi na Julius ole Sekayan.Mwanri alisema katika taarifa hiyo kuwa, watapigiwa kura za maoni na kamati ya madiwani wa CCM wa manispaa hiyo, na atakayeshinda jina lake litapelekwa kwa mkurugenzi wa manispaa ya Arusha.Nafasi ya Meya wa Manispaa ya Arusha imekuwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Paulo Lotha Laizer kujiuzulu.Kamati Kuu pia iliwateua wanachama watatu kushika nyadhifa za makatibu wa CCM wa wilaya. Walioteuliwa ni Zabron Msemwa, Othman Dunga na Mary Maziku.Kuhusu Jumuia ya Wazazi, taarifa ilisema imewasimamisha viongozi watatu wa kitaifa kwa tuhuma ya ubadhirifu wa fedha za shule za sekondari za Wazazi na kutumia madaraka yao vibaya. Taarifa iliwataja waliosimamishwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa jumuia hiyo, Abiud Maregesi, Makamu wake, Ramadhan Nzori na Kaimu Katibu Mkuu Cosmas Hinju.Kwa mujibu wa taarifa hiyo Babilas Mpemba, ambaye ni Katibu wa Siasa na Oganaizesheni wa ofisa ya makao makuu ya jumuia hiyo, pia amesimamishwa uongozi kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa Chama na jumuia zake.“Lengo la hatua ya Kamati Kuu kuwasimamisha ni kutoa nafasi kwa vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma kabla ya uamuzi kamili juu yao kutolewa,” ilifafanua taarifa hiyo.Taarifa ilifafanua kuwa viongozi hao watatu wa kitaifa walisimamishwa uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, toleo la Mei, 2005 kifungu cha 110 (7).

uhuru 02/8/2007

No comments: