Mbongo atia aibu
15 Aug 2007By Amour Hassan
Mwakilishi wa Tanzania katika jumba la Big Brother Africa II, Richard Bezuidenhout, 25, alivaa kimini na sidiria katika onyesho la vipaji na kuonywa na Big Brother kuwa ataadhibiwa vikali kama ataendelea kubishana na bosi wa jumba hilo (Big Brother mwenyewe) katika matukio mawili tofauti ya wiki ya kwanza ya shindano hilo. Richard, ambaye alianza ushiriki wake kwa kujitenga na wenzake hadi kuanza kuandamwa na `meseji za sms` za watazamaji zinazopitishwa kwenye TV, ambazo hata hivyo washiriki hawazioni wakidai kuwa `anaboa` na atolewe kwa vile anaonekana kummisi mkewe, alionywa na Big Brother katika siku ya tano ndani ya jumba hilo baada ya kuitwa katika chumba maalum cha maswali cha `Diary Room`. Katika siku za kwanza, Richard alikuwa akibishana na Big Brother kila alipoitwa katika chumba hicho, lakini siku hiyo Big Brother ambaye haonekani na husikika sauti tu, alimuonya akimwambia: ``Uko katika jumba la Big Brother, na Big Brother ndiye anayetunga sheria, hakuna maafikiano. Kama utaendelea na tabia yako utaadhibiwa vikali.`` Awali, Richard alipoitwa katika chumba hicho aliambiwa na Big Brother kuwa ameitwa humo kwa habari mbili - moja njema na moja mbaya. Akaanza kwa kumpa habari mbaya, ambayo ni onyo hilo na kisha akampa habari njema ambayo ni pongezi ya siku yake ya kuzaliwa ambapo alikuwa akitimiza umri wa miaka 25 na akampa na keki ya `bethidei` iliyopambwa kwa mishumaa ambayo alirejea kuizima na kufurahi pamoja na wenzake 11 ndani ya jumba hilo. Tukio la kuvaa sidiria na kimini, lilikuja katika siku ya saba ndani ya jumba hilo ambayo ilikuwa ni Jumamosi ambapo washiriki wote 12 walitakiwa kuandaa jambo la kuonyesha kipaji walichonacho. Mshiriki Jeff, 23, kutoka Kenya alielezea uwezo wake wa kutunga vitabu na kimwana mwakilishi wa Uganda Maureen, 27, alicheza ngoma ya asili na kupiga msamba wakati Mtanzania alitoa kituko kilichomuweka katika wakati mgumu kwa kupanda stejini akiwa na kimini na viatu vya mchuchumio. Akaanza kusema ``haijalishi nini mtu amevaa, daima atabaki kuwa vile alivyo.`` Kisha akavua shati alilokuwa amevaa akabaki na sidiria na kimini na akasema: ``Kwa mfano mimi nitabaki kuwa mwanaume hata kama nimevaa hivi. Najivunia kuvaa hivi niwapo nyumbani kwangu na mke wangu.`` Jaji Randall aliyekuwa akitoa maoni pamoja na jaji wa kike Marlouw, alimwambia Richard: ``Ikiwa kwa wiki tatu tu umeshadata hivyo, sijui itakuwaje baada ya miezi mitatu.`` Na jaji wa kike Marlouw alimwambia:``Nilikuwa nakuamini kuwa wewe ni mwanaume mwenye mvuto zaidi kwenye jumba hili lakini leo umeniangusha.`` Mjadala huo haukuishia hapo kwani baadaye usiku wakati Richard akipiga stori za kawaida na memba wenzake wa jumba hilo alijikuta katika wakati mgumu na kulazimika kujitetea kuwa yeye si shoga. Mwakilishi wa Malawi Code Sangala, ambaye katika vipaji yeye aliimba wimbo wa kienyeji akipiga na gita lake ambalo hulitumia kuwaburisha wenzake katika jumba hilo, alimkomalia zaidi Richard ambaye hadi alianza kuwa mnyonge. Alimwambia: “Usikitetee kitendo chako cha kuvaa sidiria, kimini na viatu vya mchuchumio kwamba ni cha kawaida… si cha kawaida kwa wengine kama mimi. Wewe unasema mkeo hakushangai nyumbani kwako ukivaa hivyo, lakini kama rafiki yangu wa kike angeniona mimi nimevaa hivyo, angeshangaa sana kwamba `he huyu amekuwaje tena?``. Jumapili ijayo washiriki wataanza kutajana wenyewe kwa wenyewe kupendekeza majina mawili ya watakaopigiwa kura ya kutoka katika jumba hilo ambalo linamulikwa kwa kamera 28 zilizotapakaa kila kona kwa saa 24 zote za siku. Mshindi atapatikana baada ya siku 98 na atajizolea kitita cha dola 100,000 ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi milioni 130 za Kitanzania. Miaka minne iliyopita wakati shindano hilo lilipofanyika kwa mara ya kwanza, Tanzania iliwakilishwa na Mwisho Mwampamba aliyefikia hatua ya fainali kabla ya kuzidiwa kete kidogo na kimwana Mzambia Cherise Makubale. Richard, mzaliwa wa Ilala, ana mke mzungu raia wa Canada mwenye umri wa miaka 28 na ni mshiriki pekee miongoni mwa washiriki wa Big Brother II aliye katika ndoa.
* SOURCE: Alasiri
Thursday, 16 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment