Thursday, 23 August 2007

Moto: Pasi zinachangia


Pasi chanzo cha vifo Dar - Tanesco
23 Aug 2007By Joseph Mwendapole
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), limesema uchunguzi wa moto uliounguza nyumba na kusababisha vifo vya watu watano, umeonyesha kuwa chanzo ni pasi ya umeme iliyoachwa bila kuzimwa. Pasi hiyo iliachwa katika kochi lililopo sebuleni katika nyumba hiyo maeneo ya Mbezi Mwisho usiku wa kuamkia Jumatatu. Taarifa iliyotolewa na shirika hilo jana ilisema uchunguzi huo umefanywa na wahandisi na mafundi wa shirika hilo. Ilisema baada ya pasi hiyo kuunguza kochi hilo, moto ulisambaa nyumba yote na kusababisha uharibifu mkubwa. Ilifafanua kuwa wataalamu wa shirika hilo na kikosi cha zimamoto waliofika eneo hilo baada ya moto kuzimwa, walikuta nyaya za pasi hiyo zikiwa bado ukutani na soketi ikiwa haijazimwa. Aidha, taarifa hiyo ilifafanua kuwa uchunguzi umebaini kuwa nyumba hiyo ilikuwa inatumia umeme unaotoka kwenye nguzo ambayo pia ilikuwa na nyaya zinazopeleka umeme kwenye nyumba zingine tatu za jirani. Hata hivyo, ilisema nyumba hizo hazikuathirika katika tukio hilo kwasababu lilihusu mtandao wa umeme kwenye nyumba moja iliyoungua. ``Endapo chanzo cha moto huo kingekuwa umeme wa Tanesco nyumba hizo zinazopata umeme kwenye nguzo hiyo pia zingeathirika,`` ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Taarifa hiyo ilisema sio matukio yote ya kuungua kwa nyumba yanasababishwa na Tanesco na kwamba mara nyingi yanatokana na mishumaa, majiko ya mkaa na milipuko ya majiko ya mafuta ya taa. Taarifa iliwataka wateja wahakikishe kuzima pasi ama vifaa vya umeme vingine vya hatari wanavyotumia mara baada ya kumaliza kazi. Tanesco ilishauri kwamba kila baada ya miaka miwili au mitatu wateja watafute mkandarasi wa umeme mwenye leseni ili akague mfumo wa nyaya za umeme zilizotandazwa katika nyumba zao. Taarifa ilizidi kusema kwamba mfumo chakavu wa utandazaji wa nyaya za umeme unaweza pia kuwa chanzo cha ajali ya moto na kwamba umeme unapokatika wateja wanapaswa kuzima umeme ili unaporudi kusiwe na hitilafu.
* SOURCE: Nipashe

No comments: