Mitaa ya Mbagala Dar kuboreshwa
SERIKALI ipo mboni kuboresha maeneo ya Kata za Charambe, Mbagala Kuu na Mbagala chini ya mpango wa UN Habitat, Bunge limeelezwa.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani wakati akijibu swali bungeni jana.
Alisema serikali katika jiji la Dar es Salaam inatekeleza mpango wa miji bila makazi holela unaofadhiliwa na UN Habitat na kuwa mpango huo ni wa kitaifa.Celina alisema jijini Dar es Salaam, mpango huu ulizinduliwa na Waziri Mkuu Edward Lowassa, Mei mwaka huu na umeanza kutekelezwa ambapo awamu ya kwanza serikali imefanikiwa kuboresha maeneo 16 katika kata za Manispaa za Ilala,Temeke na Kinondoni.
Alisema katika awamu hiyo, serikali iliboresha barabara za maeneo hayo kwa kiwango cha lami na changarawe, imejenga viziba vya taka, vyoo na mifereji.
Naibu Waziri aliongeza kuwa katika awamu ya pili, serikali itaboresha maeneo 14 katika manispaa hizo na kwamba kata za Charambe, Mbagala Kuu na Mbagala zimejumuishwa.
Celina alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza mipango ya kuboresha makazi katika maeneo yaliyojengwa bila mpango maalum unaolenga kuondoa adha kwa wananchi.
Alitaja mipango hiyo kuwa ni mradi wa kuboresha miundombinu kwa kushirikisha wananchi ulio chini ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo Kata za Charambe, Mbagala na Mbagala Kuu zitaingizwa katika awamu ya nne.
Alisema mradi mwingine ni wa kurasimisha mali za wanyonge ambao unahusisha utoaji wa leseni za nyumba zilizojengwa maeneo yasiyopimwa na mradi wa upimaji wa viwanja 20,000 unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Aliongeza jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke limeandaa mpango mkakati wa kuboresha makazi holela na miundombinu na kuwa katika kutekeleza mpango huo, tayari ramani za matumizi ya ardhi kwa Dar es Salaam zinaandaliwa na zitakamilika mwezi ujao.Celina aliyasema hayo kufuatia maswali yalioulizwa na Mwinchum Msomi (Kigamboni-CCM).
Chanzo: Gazeti laUhuru
Saturday, 18 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment