Huduma za benki zawafuata hadi mlangoni wananchi wa Mbagala
07 Aug 2007By Haji Mbaruku, Jijini
Benki ya Biashara ya NBC, imefungua tawi lake eneo la Mbagala na hivyo kuwapunguzia adha ya kutafuta huduma za kibenki wakazi wa Mbagala, Mtoni Kijichi, Mtoni Kwa Azizi Ally na hata Kongowe. Naibu Mkurugenzi wa Masoko wa benki hiyo, Bw.William Kalage amemwambia Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Abdilsalam Hatib kuwa, kufunguliwa kwa benki hiyo ni hatua kubwa ya kimaendeleo kwa wafanyabiashara mbalimbali wa Mbagala na Mtoni. Amesema kusogea kwa huduma hiyo pia ni maendeleo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wameshindwa kufungua akaunti kutokana na mabenki mengi kuwa katikati ya Jiji. Bw. Kalage amesema benki hiyo pia imeona ni vema kufungua tawi lake hapo Mbagala ili kuitikia wito wa Rais Jakaya Kikwete kwa mabenki nchini kufungua matawi mengi ya biashara. Amesema kwa vile Rais alizitaka benki mbalimbali nchini kusogeza huduma zao karibu na wateja wao, NBC imeona ni vyema wakaitikia mwito huo kwa vitendo. Akasema benki hiyo itaendelea kufungua matawi mengi zaidi na hivyo kuwa karibu zaidi na wateja wake. `Tutaendelea kufungua matawi kadri siku zitakavyozidi kusogea ili kutoa huduma zaidi kwa wananchi,` ameongeza. Hii ni mara ya kwanza kwa benki nchini kufungua tawi lake eneo la Mbagala na hivyo kuwapunguzia adha wakazi wa Mbagala na maeneo ya Kongowe ambao hulazimika kwenda hadi maeneo ya Posta ama Ubungo kupata huduma za benki.
* SOURCE: Alasiri
www.ippmedia.com
Tuesday, 7 August 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment