Monday, 10 December 2007

Wanawake 'wanawazeesha' waume zao?

Ukiwaza sana ya mkeo na uzee utakujia vibaya!

Wiki iliyopita katika safu yetu hii, niliandika kisa fulani ambapo jamaa mmoja anaomba ushauri baada ya kupata suluba toka kwa mkewe aliyempenda kwa dhati. Jamaa alidhani kapata mke kumbe kapatikana na sasa yu taabani asijue la kufanya.

Kisa chake baada ya kuchapishwa hapa, wapo baadhi ya wasomaji wameungana naye kwa kumpa ushauri kuhusiana na sekeseke hilo la kifamilia.

Kwa leo nitachapisha email mbili zikijaribu kumtuliza jamaa yetu huyo ambaye anasema akiwa ulaya anajawa na amani kuliko akiwa pale nyumbani kwake na mkewe huyo aliyempenda mwenyewe lakini sasa amekuwa mwiba mkali.

Hebu tusikie ushauri anaopewa mwenzetu huyu kwa leo. Email ya kwanza inaanza hivi: ``Kwa kweli mimi binafsi nampa pole sana huyu jamaa, ila nimwambie kilichounganishwa na Mungu mwanadamu hawezi kukitenganisha.

``Kabla ya kumpa ushauri huyu bwana, ngoja nieleze dukuduku langu. Vijana wengi wanapopata nafasi kidogo hukimbilia kuoa bila kufanya uchunguzi wa kina ni nini kiolewacho.

Hii husababishwa na mapenzi motomoto ya mwanzo wa penzi.
``Nimeona vijana wengi wamalizapo vyuo hukimbilia kuoa mapema na matokeo yake wanajuta. `SI WANAWAKE WOTE WAOLEWAO, BALI WATEULE TU’ hata kama ni wazuri.

``Wanawake ni wajanja sana waonapo jamaa amesoma au ana mwelekeo wa kupata pesa hata kwa wakati ujao, au wanajitahidi kujenga mazingira ya kuoana. Suala hili linatugharimu sana sisi vijana tusio na uzoefu wa mapenzi.

``Mitego, iwekwayo na wanawake wajanja wa mapenzi ni kujitambulisha kwa kila mtu kuhusu mahusiano yenu siku za mwanzo wa penzi, kupenda kutoka outing pamoja mara kwa mara, kukushauri mwende mkasali ili ujue anamtanguliza Mungu katika mtego wake ili nawe uwe na hofu ya Mungu katika maamuzi yako.

``Yafaa uwe makini sana na watu aliokuwa na mahusiano hapo awali ili ujue ameachana nao. Wakati mwingine atakushauri mpunguze starehe kwa kujifanya anaandaa zaidi future, atakuomba ruhusa kutoka kwenda popote hata kama yupo kwao, na mengine mengi.

Ila ukitaka kujua yote hayo ni uongo au ni kweli mpe muda mrefu wa kuchunguzana lazima atarudia tabia zake halisi.

``Ushauri wangu kwa jamaa huyu ni kuvumilia na kufikiria zaidi watoto watano alionao, pia kwenda kupima DNA, ili kujua kama watoto ni wake au analea watoto wa mume mwenzake.

``Misalaba duniani ni mingi kwa hiyo ndugu yangu vumilia hilo ndio chaguo lako, somesha watoto wako kama wewe unavyosoma, watoto wakiwa wakubwa mama yao atajirekebisha tu, pia jitahidi mwende mkapime VVU. Hii inaweza kuwa njia muhimu ya kumjenga hofu mkeo ili atulie.

``Kumbuka pia kumpeleka kwa wazazi wake akapumzike kwa kipindi fulani mbali na huyo unayehisi ana mahusiano nae kimapenzi ili uone kama anakukumbuka au ndio itakua nafuu kwake kukata mawasiliano nawe.

Mwisho mtangulize Mungu mbele ili mkeo abadilike wala usifikirie kumuacha
Naitwa Pastory Stephano Simu: 0713494671
Mpenzi msomaji, hivyo ndivyo anavyomaliza email yake ndugu yetu Pastory na namshukuru sana kwa maoni yake murua. Sasa tumgeukie msomaji wetu mwingine tuone anasemaje kuhusiana na tatizo hilo.

Yeye anaanza hivi;-
“Napenda nichangie mada ya huyo baba aliyeingia mkenge! Kwanza kabisa nianze kwa kusema maisha ndiyo yalivyo kwanii, kila mtu ana matatizo yake na asijione ni yeye tu wapo wengi wa aina hiyo.

Kitu ambacho napenda kumshauri ni kuwa, pamoja na vituko vya mwanamke huyo, lakini aliweza kuvumilia mpaka sasa ni takribani miaka 25 na wamejaliwa kupata watoto 5.

Mambo mengi ya huyo mke amekwisha yafahamu kama ulivyotueleza kuwa ana mwanaume mwingine na pia hataki kwenda huko ng`ambo, ndio sababu pengine inayomfanya asitake kwenda huko.

Vilevile mume huyo anasema huko ng’ambo ana amani kubwa sana. Mimi namwambia ashikilie hapo hapooooooo! kuna usemi wa siku hizi usemao raha jipe mwenyewe...akiendelea kuwaza ya mkewe hata uzee wake utamjia vibaya, aendelee na mambo yake huko aliko, kwani sikio la kufa halisikii dawa. Ila asisahau kutunza watoto wake ambao sasa nafikiri ni wakubwa.
Wako Dorry

Hayo ndio maoni ya msomaji wetu wa pili. Asante sana Dorry kwa mchango mzuri ambao hakika utamliwaza mwenzetu huyo. Bila shaka msomaji wangu umeyasikia. Kama unayo ya ngongeza unakaribishwa. Lakini kwa jumla Maisha Ndivyo Yalivyo.

Jeuri kubwa aliyo nayo mwanamama tuliyemzunguzia ni kule kuwa na mahusiano ya nje. Bado anaye mpenzi wake wa nje ampendaye kupita kiasi na kumweka kando mumewe mpenzi aliyempenda na kumthamini lakini ikawa ni kazi bure.

Mke huyu hakika ni kiruka njia. Ya ndani kwake hayataki sharti aruke ukuta na kutafuta wachuchu wa nje. Ni hatari sana.

Iliyopo ni bwana yule aridhie moyo wake, ahangaikie wanawe waweze kusonga mbele tayari kwa maisha yatakayowawezesha kujitegemea. Awasomeshe vema ili iwe ufunguo halisi wa maisha yao.

Raha ya mke kwa bwana huyu ndiyo kama imefikia tamati. Afanyeje sasa? Kama mke wake ameamua kuweka uzio kati yao basi naye ajiwekee tahadhari kwani mahusiano ya nje ya mkewe hayana matokea mazuri.

Hana hata sababu ya kumfuatilia mke huyu anayeonekana ni jeuri. Nimpe tena pole baba huyu kwa maji aliyoyavulia nguo ambayo sharti ayaoge.

Wasalaam,

By Anti Flora Wingia
Email: fwingia@yahoo.com
09 Dec 2007

* SOURCE: Nipashe

No comments: