Kama mpenzi na mshabiki wa timu ya mpira wa miguu na mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, napenda kutumia nafasi hii kutoa maoni au mapendendekezo yangu kwa uongozi wa timu kama salaam zangu za mwaka mpya kwa timu/klabu.
Tangu miaka ya 1990 Yanga imekuwa ikipata wafadhili au wahisani mbalimbali ambao wameisaidia sana timu ktk kipindi kigumu kiuchumi hadi hii leo. Misaada mikubwa imekuwa ya kifedha na imeelekezwa sana ktk huduma za wachezaji, walimu na uongozi hasa ktk kulipa bili za chakula, nauli, mishahara na marupurupu kwa wachezaji/walimu wao. Msaada wa namna hii ni mzuri ila ni wa muda mfupi na matunda yake huwa sio endelevu.
Njia muafaka ya kusaidia timu/klabu ni kuchangia (kufadhili) au kuwekeza ktk miundombinu ya timu kwa manufaa ya muda mrefu.
Kwa hiyo Yanga inahitaji wafadhili wa kuwekeza ktk vitega uchumi vya timu kama vile majengo ya ofisi yenye huduma kama hoteli, migahawa, vifaa vya kisasa vya mazoezi ya timu na uwanja wa timu wenye nafasi za kukaa kiasi cha watazamaji 25,000.
Pia kuingia mkataba wa kibiashara na watu wenye viwanda vya bidhaa mbalimbali; mathalani jezi na nguo, mabegi, kofia, kalenda na steshenari zenye nembo (brand) ya timu. Kwa njia hii timu itajipatia kipato na kujiendesha kibishara katika mfumo endelevu na kwa mazingira ya kisasa zaidi.
Endapo mikakati hii itafanyiwa kazi, timu haitakuwa inawategemea sana wafadhili kwa ajili ya mambo madogo madogo. Mfano nimewahi kusoma magazetini timu kukosa nauli ya wachezaji kambini (Chuo Kikuu) kwa sababu ya ukata hadi mchezaji wa zamani Aaron Nyanda kutoa hela yake mfukoni 35,000/= kwa ajili ya posho ya wachezaji! Hii ni aibu sana kwa timu kama Yanga na kukosa dira ktk mipango na maendeleo.
Wakati mwingine timu inategemea sana wadhamini wa ligi, na kama wasipotoa fedha au jezi kwa wakati timu inayumba.
Dawa ya yote ni kubadilika na kwenda na wakati. Na hii ni changamoto ninatoa kwa uongozi -kina Lucas Kisasa na wenzake wote.
Kila la heri Yanga katika mwaka ujao 2008, uwe wa mafanikio kimichezo na kiuchumi!
Friday, 28 December 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment