Saturday, 1 December 2007

Ukimwi: Mababu na Mabibi walea wajukuu!

Ni nyakati za jioni siku ya Ijumaa tunapowasili sehemu inayoitwa Ghuba ya Richard yaani Richard`s Bay huko Durban, Afrika Kusini.

Nia ya ziara yetu hapa ni kutembelea miradi ya Msalaba Mwekundu eneo la KwaZulu Natal.

Wakati huohuo wa jioni tunatembezwa sehemu mbalimbali ili kuzifahamu mapema sehemu ambazo tungezitembelea kesho yake asubuhi.

Tunapopita eneo la Slovo, eneo ambalo limekuwepo kwa muda wa miaka kumi tangu lianzishwe, tunakutana na watoto wengi wakiwa wanajishughulisha na kazi mbalimbali za nyumbani, kama vile kubeba kuni na ndoo za maji kichwani, kusafisha vyombo, na kadhalika.

Inaonekana kama vile watoto hawa hawana muda wa kucheza, na hivyo, tunaamua kuitembelea moja ya familia zilizo eneo hili.

Bibi Busisiwe Ngwekizi, mwenye umri wa miaka 70 anafungua mlango wa nyumba yake.

`Ninaishi na wajukuu wangu wawili, Phindile, mwenye umri wa miaka minane, na Thandeka, mwenye umri wa miaka 13. Mama zao walifariki miaka mine iliyopita,` anasema.

Habari hii ya kusikitisha ni jambo la kawaida katika eneo hilo.

Si kwamba watoto wanaishi katika mazingira magumu tu kwa vile wazazi wao wamefariki kutokana na Ukimwi, bali babu na bibi wa watoto hao wanajikuta hawana muda wa kupumzika maishani mwao kutokana na jukumu la kuwalea wajukuu zao licha ya umri wao kuwa mkubwa.

`Wote walifariki mwezi mmoja mwaka 2001, na wote nilikuwa nikiwahudumia wakati wakiwa wagonjwa,` anasema bi kizee huyo huku machozi yakimtiririkia kwenye mashavu yake yaliyokunjamana.

`Ulikuwa ni wakati mgumu kwangu kuwahudumia binti zangu na watoto wao. Nilipitisha siku nyingi bila kuwa na usingizi kutokana na hali ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya,` anaongeza kusema.

`Tulikumbwa na ukame mkubwa mwaka huo na chakula kikawa adimu. Mabinti zangu hao wawili walikuwa wakipata dawa za tiba na walikuwa wanatakiwa kula vizuri kabla ya kumeza dawa, lakini chakula kilikuwa hakipatikani.`

Busisiwe, kama walivyo wazee wengine, anapata pensheni ya Randi 720 za Afrika Kusini kwa mwezi ambazo ni sawa na shilingi 125,000 za Tanzania, lakini kutokana na majukumu aliyo nayo, fedha hiyo haitoshi.

`Niliweza tu kununua debe la unga ambalo tulilitumia kwa ajili ya kupata chakula chetu nyumbani,` aanasema .

Licha ya juhudi zake, binti za Busisiwe waliaga dunia na kumwacha mama yao mpendwa, na kumwachia jukumu kubwa la kuwalea watoto wao wachanga.

Ni karibu miaka mine sasa tangu wafariki na hakuna mafanikio yoyote ya matumaini kutokana na umri wake kuongezeka, wakati ambapo mahitaji ya watoto hao yanazidi kuongezeka kulingana na wanavyokua.

Kipato chake kinamlazimu kufanya maamuzi magumu.

`Kutokana na pensheni hiyo, ninalazimika kulipa karo za watoto hao, kuwanunulia chakula, nguo na mahitaji mengine,` anasema.

Alishindwa kulipa ada kwa vile fedha ilitumika kununulia dawa kwa ajili ya matatizo yake ya ugonjwa wa kisukari.

Anategemea kulipa ada hiyo mwezi ujao, jambo ambalo linamaanisha hatakuwa na fedha ya kutosha kununulia chakula.

``Ninazidi kuzeeka na kuchoka. Sijui nini kitawakumba watoto hawa nikifa, lakini ninataka wakue wawe watu wazima,`` anasema Busisiwe kwa masikitiko.

Karibu na nyumba yake kuna makaburi ya binti zake. Mambo yakiwa magumu zaidi huenda kusali eneo hilo akiwa na matumaini ya binti zake kujibu maombi yake kutoka mahali walipolala.

Tunapozungumza naye giza tayari limeingia na hapana moto uliowashwa kwa ajili ya kutayarisha chakula cha jioni kwani hakuna cha kupika.

`Ndiyo kwanza nimetoka kufanya kazi katika shamba moja la mtu, lakini sijalipwa chochote kwa vile kazi yenyewe sijaimaliza. Usiku wa leo tutakula vipande vya mkate vilivyo bakia siku tatu zilizopita,` anasema Busisiwe.

Janga la VVU/Ukimwi limekifuta kizazi kizima. Kwa upande wa wazee, hali inazidi kuwa mbaya. Badala ya wao kutunzwa na watoto wao, wanalazimika kuwatunza wajukuu zao. Hali ya Busisiwe ni kielelezo kamili cha eneo la KwaZulu Natal ambako watoto hulelewa na babu au bibi zao.

`Ni kazi ngumu sana kwa wazee kulea watoto,`anasema Anne-Marie Kazungu, mrabitu wa VVU/ukimwi wa tawi la Richard`s Bay la Chama cha Msalaba Mwekundu cha Afrika Kusini. `Watoto wengi wameacha shule kwa sababu kadhaa.

Wengine ni kwa kukosa karo, chakula na nguo au kulazimika kuwasaidia babu au bibi zao kwa kazi za mashambani,` anasema Anne-Marie, akiongeza kwamba baadhi ya watoto wameajiriwa kufanya kazi za malipo duni au wao wenyewe kuendesha ukahaba ili kuweza kuwatunza wadogo au watoto wao.

`Hivi sasa tunatoa vyakula na mablanketi na vifaa vingine kwa familia mbalimbali, lakini hatuna uwezo wa kuzisaidia familia zote zenye matatizo haya.

Misaada hii ni midogo sana ukilinganisha na hali inavyozidi kuwa mbaya,` anasema.
`Tunatia maanani sana mustakabali wa watoto hawa.

Angalao wakimaliza elimu inayostahili, wanaweza kujikimu wenyewe na wadogo au watoto wao,` anasema Anne-Marie, akiwataka wadau wote kujitokeza kuwasaidia watoto waliokumbwa na janga la VVU/Ukimwi.

Taasisi ya Shirikisho la Kimataifa (International Federation) kusini mwa Afrika imeanzisha kampeni ya utetezi chini ya wito wa `Watoto Wetu, Mustakabali Wetu` ili kuwasaidia watoto waliokumbwa na matatizo haya.

`Hali itakuwa mbaya sana iwapo mataifa ya Kusini mwa Afrika na wadau wote wasipotoa misaada kwa yatima na watoto wengine wenye matatizo yanayotokana na VVU/Ukimwi,` anasisitiza Françoise Le Goff, mkuu wa shirikisho hilo tawi la Harare, Zimbabwe.

Mwanamke huyo anasisitiza haja ya wadau wote, hususani sekta binafsi, serikali na taasisi za misaada ya kibinadamu, kushiriki katika kuwahudumia yatima na watoto waliokumbwa na janga la VVU/Ukimwi katika masuala ya chakula, afya, elimu, makazi, mavazi, na kadhalika, ili kuhakikisha hali yao bora siku zijazo.

`Janga la kimya lenye nguvu ya tsunami linakiangamiza kimya-kimya kizazi cha sasa, na kuwaacha mamilioni ya watoto katika matatizo. Ni muhimu kwa wadau wote kuungana na kulitatua tatizo hili.

Tusipofanya hivyo, tutapoteza watawala, wafanyabiashara, wafanyakazi na wateja wetu wa siku zijazo. Inatulazimu kuanza kuwekeza kwa watoto hawa sasa,` anaongeza kusema.

Inakadiriwa kwamba kuna yatima zaidi ya 4,132,000 waliotokana na janga la Ukimwi katika nchi kumi za Kusini mwa Afrika ambamo Chama cha Msalaba Mwekundu kinaendesha shughuli zake, robo yao wakiwa nchini Afrika Kusini.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2010.

* SOURCE: Nipashe, 01 Dec 2007

No comments: