Friday, 28 December 2007

Umeme bei juu: 2008 hatufi ila cha moto...!!!

Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imeliruhusu Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupandisha bei ya umeme.

Kuanzia mwezi Januari mwakani bei ya umeme itaongezeka kwa asilimia 21.7, wakati ile ya kuwaunganishia wateja wapya itaongezeka kwa kati ya asilimia 66 na 215.

Mwezi Agosti mwaka huu, Tanesco iliomba kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 40 na asilimia 281 kwa wateja wapya wanaounganishiwa umeme.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Haruna Masebu, alisema mamlaka hiyo imeona kuwa bila kufanya hivyo Tanesco haiwezi kujiendesha.

Alisema bei ya umeme wa matumizi madogo ya kaya umepanda kutoka Sh. 40 kwa uniti moja hadi kufikia Sh. 49, wakati Tanesco ilipendekeza bei iwe Sh. 56.

Alisema kwa matumizi makubwa ya kaya bei imepanda kutoka sh. 128 kwa uniti hadi kufikia Sh. 156. Tanesco yenyewe ilipendekeza Sh. 179.

Bw. Masebu alisema matumizi ya kawaida gharama za huduma kwa mwezi zimepanda kutoka Sh. 1,892 hadi kufikia Sh. 2,303.

Alifafanua kuwa kwa wateja wanaotumia msongo mkubwa gharama za huduma kwa mwezi imepanda kutoka Sh. 7,012 na kufikia Sh. 8,534.

Kuhusu wateja wapya wanaounganishiwa umeme, alisema wenye matumizi ya kawaida ambao watatumia mita za kawaida (Single Phase) umbali usiozidi mita 30 watalipia Sh. 342,619 badala ya bei iliyopendekezwa na Tanesco ya Sh. 469,393.

Alisema watakaounganishiwa umeme kwa kutumia mita za LUKU watalipa Sh. 385,682 tofauti na bei iliyopendekezwa na Tanesco ya Sh. 469,393.

Watejawatakaounganishiwa umeme umbali wa mita 30 umeme mkubwa (Three Phase) kwa kutumia mita za kawaida watalipa Sh. 880,772 na Tanesco ilikuwa imependekeza bei iwe Sh.1,065,735.

Bw. Masebu katika kundi hilo, alisema wateja watakaounganishiwa kwa kutumia mita za LUKU watalipa Sh. 772,893.

Alisema watakaounganishiwa umeme umbali wa mita 70 Single Phase nguzo moja na mita ya LUKU watalipa Sh. 1,145664.

Bei iliyokuwa imependekezwa na TANESCO ni Sh. 1,388,972.

Alisema watakaounganishiwa umbali wa mita 70 Three Phase kwa kutumia mita za LUKU watalipa Sh. 1,799,062 kinyume na Sh. 2,180,188 zilizopendekezwa naTanesco.

Mkurugenzi huyo alisema watakaounganishiwa umbali wa mita 120 Single Phase kwa kutumia mita za LUKU watalipa Sh. 1,696,120 na si sh. Sh. 2,054,999 zilizokuwa zinapendekezwa na Tanesco.

Alisema wateja wa umbali wa mita 120 Three Phase kwa kutumia mita za LUKU watalipa Sh. 2, 604, 391 na Tanesco ilipendekeza iwe Sh. 3,154, 635.

Alisema walifanya tathmini ya kina kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali nchini kabla ya kutoa uamuzi huo.

Alisema baada ya kupata maoni ya wananchi na kufanya uchambuzi wa kina, EWURA ilibaini kuwa hoja ya TANESCO ina mantiki na ni halali.

Alisema nyongeza ambayo imeidhinishwa kwa bei ya umeme na gharama za kuwaunganishia wateja wapya italiwezesha shirika hilo kulipa gharama zake za uendeshaji na ukarabati wa miundombinu.

Alisema ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 21.7, italiwezesha shirika hilo kupata Sh. bilioni 56, ambazo litazitumia kujiimarisha kiutendaji.

Bw. Masebu alisema shirika hilo litafanya utafiti wa kutambua viwango vya upotevu wa umeme wa kiufundi na wa kibiashara katika mfumo wake.

* SOURCE: Nipashe, 28 Dec 2007
By Joseph Mwendapole

No comments: