Nilifahamu katika kipindi kifupi Amina Chifupa(26), japo hatukuwa tumezoeana lakini kutokana na majukumu yangu hasa katika nyanja ya michezo na burudani, tuliweza kugongana mara chache. Amina alifariki juzi usiku majira ya saa tatu kwenye hospitali ya Lugalo na kufanya taifa kuzizima kutokana na masikitiko ya kifo chake. Alikuwa mtu, ambaye aliweza kugusa kila nyanja na hasa kwenye burudani, michezo na siasa, ambako ndiko alikokutwa na mauti yake. Chifupa alikuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano kupitia tiketi za vijana, ambapo alionyesha cheche mara baada ya kuchaguliwa kwake mwaka 2005. Mara ya mwisho kukutana naye ilikuwa mwezi Februari, mwaka huu wakati alipoandaa sherehe maalum ya kutimiza miaka mitano yake na ndoa na mumewe Mohammed Mpakanjia `Medi`. Pia mtoto wao, Rahman, alikuwa akitimiza miaka mitano kwenye sherehe hiyo iliyofanyika nyumbani kwao Sinza. Bahati mbaya kwenye sherehe ndio kulikuwa kumeanza kutokea minong?ono ya kuwepo mpasuko kwenye ndoa yake na Mpakanjia. Walichukua nafasi hiyo kuwadhihirishia marafiki, ndugu na majirani zao kuwa walikuwa bado kitu kimoja. Bahati mbaya sana yakatokea mengi yaliyotokea ndoa yake kuvunjika baada ya kutalikiwa na mumewe. Kitu kimoja kuhusu Amina, alikuwa akigonga vichwa vya habari kila mara, na kufanya kila mmoja katika jamii ya watanzania kumchukulia kivyake. Wengine walimwona mtu safi,kutokana na jinsi alivyopenda kusaidia walemavu, yatima na wale wote wenye shida. Alichukuliwa mpiganaji wa haki za wanyonge na hasa walipoingia kwenye vita ya kupambana na wauza madawa ya kulevya na wala rushwa na wabadhirifu kwenye serikali. Hiyo haikuzuia watu wengine kumwona kama mpenda sifa na mwenye kiherehere. Ukiachia yote hayo ya mitaani, Amina alikuwa na msimamo na alikuwa akifanya kile alichokiamini kilikuwa sawa kwake. Kutokana na msimamo huo, aliweza kutoa mchango mkubwa kwenye nyanja hasa za taarabu na michezo. Amina hakujali jamii ilikuwa inamchukulia vipi, bali mara zote alisimama kufanya kile alichokuwa anakiamini na kwa maneno mengine ya Kiingereza ungeweza kumwita `timetaker`. Kupitia vipindi vya burudani na hasa kwenye Redio ya Clouds alikoanzia kazi alikuwa na kipindi cha Unavyojisiki, ambapo alikuwa akipiga taarabu zaidi na kuzifanya kupanda kwenye chati za burudani. Nani atasahau mwaka 1999 hadi 2001, wakati muziki wa `Rusha Roho` ulipokuwa `matawi ya juu` na kufanya pambano la vikundi vya taarab vya TOT na Muungano kwenye miaka hiyo kuingiza kiasi cha Sh. milioni 20 katika onyesho moja. Akiwa mtangazaji wa kipindi cha African Bambataa kwenye miaka hiyo, ambapo akishirikiana na DJ Charles waliweza kuinua bendi za nyumbani. Hapo ndipo tulipoanza kushuhudia muziki wa Congo ukianza kuwekwa pembeni na watu wakaanza kupenda bendi zetu za nyumbani na pia kuibuka kwa `bongo fleva.` Chifupa ni mwaka huu baada ya kuwa Mbunge, alianza kujitokeza katika nyanja za michezo na hususan soka. Bila shaka kipindi hicho huku kukiwa hakuna makampuni yaliyojitokeza, alijitolea kutangaza zawadi kwa wachezaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars walipokuwa wanajiandaa kucheza na Burkina Fasso na Msumbiji kwenye mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika, mwaka jana. Alionyesha uzalendo wa hali ya juu alipotinga na track suit ndani ya Uwanja wa Taifa wakati Stars ilipocheza na Burkina Fasso. Pia alionyesha ukereketwa wake wakati alipokwenda Msumbiji na kuahidi kutoa motisha ya fedha ya Sh. 500,000 kwa kila goli, ambalo lingefungwa. Chifupa alionyesha uzalendo wa hali ya juu kutokana na kuwa kati ya watu wa mwanzo kujitokeza kuisaidia Stars katika kipindi ambacho kila mwanzo ilikuwa haina wadhamini. Ndio maana mara baada ya kifo chake kutangazwa jana kwenye redio na televisheni, jamii ya watanzanzia imeweza kuwagusa watu kwa njia moja ama nyingine. Kutokana na ukweli kuwa Amina kutokana na ujasiri wake na kutojali maneno ya watu, aligusa nyanja za siasa na michezo akiwa Mbunge na pia kutoa mchango mkubwa katika kukuza sanaa na burudani za Kitanzania akiwa mtangazaji wa redio ya Clouds. Anazikwa leo kijijini kwao Lupembe wilaya ya Njombe mkoa wa Iringa. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi! Amen.
*Source: Nipashe; imeandikwa na Samson Mfalila.
Thursday, 28 June 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment