Tuesday, 26 May 2009

Kukubali kushindwa ni ushujaa pia

Napenda kuwasihi watanzania wenzagu kuwa na moyo wa kweli kiushindani. Ktk mashindano yoyote yale ni lazima apatikane mshindi na kwa matokeo hayohayo ambaye hakushinda atapatikana pia.
Wenzetu waliogombea kule Busanda walikuwa na wiki takribani 4 za kujinadi. Baada ya muda huo, ikaja zamu ya wapiga kura kuamua na WAMESHAAMUA ni nani awe mbunge wao. Ni mategemeo yangu kuwa wagombea walioshindwa wangekubaliana na kauli ya wananchi. Huo ndio ukomavu wa kidemokrasia.
Hongera sana Mheshimiwa Lolensia Bukwimba wa Chama Cha Mapinduzi. Wananchi wameonyesha imani nawe kwa kukuchagua kuwa mwakilishi wao. Ninakutakia kila la heri katika majukumu yako. Moja ya kazi ninazokutuma Bungeni ni kufuatilia utaratibu mbaya uliopo ktk sheria za uchaguzi uliosababuisha wewe na wagombea wengine kutopiga kura kwa kuwa mlijiandikisha sehemu nyingine tofauti na Busanda. Hebu fuatilia hilo, inauma mtu kugombea halafu usiruhusiwe kupiga kura!

4 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Mgombea wa CCM atangazwa mshindi

Wakati Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Busanda, Wilaya ya Geita, mkoani Mwanza, Dani Mollel, akimtangaza aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lolensia Bukwimba, kuwa mbunge mpya wa jimbo hilo, aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Finias Magessa, amekataa matokeo hayo.

Magessa ambaye ameshika nafasi ya pili baada ya kujizolea kura 22,799 sawa na asilimia 44 katika uchaguzi huo, aliyakataa matokeo hayo, huku akitoa sababu kadhaa kutilia mkazo madai yake ya msingi kwamba, uchaguzi huo uliofanyika Jumapili wiki iliyopita kuwa haukuwa huru na wa haki. Bukwimba alipata kura 29,242 sawa na asilimia 54.

Kutokana na sababu hizo, Magessa ambaye muda wote wa kusubiri hadi kutangazwa kwa matokeo hayo aliongozana na maafisa wawili waandamizi wa Chadema; Benson Kigaila na Basil Lema, alidai matokeo yaliyotangazwa jana, ni ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na CCM na kwamba, siyo ya wananchi wa Jimbo la Busanda.


CHANZO: NIPASHE 26th May 2009

MOSONGA RAPHAEL said...

Chadema wakataa matokeo Busada II

Finias Magesa alisema uchaguzi huo haukuwa huru kwa vile uligubikwa na visa na matatizo mengi, ikiwamo kununuliwa kwa shahada za wapigakura na kuandikwa kwa namba zake, kiasi ambacho idadi ya waliojitokeza kupigakura hawakuzidi 50,000, kati ya watu 135,163 waliojiandikisha kupiga kura jimboni humo.

Pia, alidai kipindi chote cha kampeni za kuwanadi wagombea katika uchaguzi huo, kilitawaliwa na vitisho dhidi ya wapiga kura, vilivyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha.

“Masha alikuwa akipita na kuwatishia watu wetu kuwa atawakamata wasipige kura,” alidai Magessa.

Alidai katika hali hiyo, baadhi ya wafuasi wa Chadema walipigwa na kujeruhiwa na wengine kutishiwa maisha, akiwamo Lema aliyejeruhiwa kichwani kwa panga, huku wahusika wakiachwa bila kuchukuliwa hatua, badala yake waliopigwa ndio waliokamatwa na kuwekwa ndani.

Mbali na hilo, alidai wakati zoezi la kupiga kura likiendelea, Waziri Masha alionekana mara kwa mara akilazimisha kuingia ndani ya vituo vya kupiga kura bila kujulikana nini alichokuwa akikifanya humo.

Alidai katika kituo kimoja kilichopo katika kijiji cha Msasa, Waziri Masha aliingia na baada ya kutoka, aliingia askari polisi, ambaye haijulikani nini alichokwenda kukifanya humo.

Pia, alidai Diwani mmoja katika Kata ya Katoro alionekana akiingia na kutoka katika kituo cha kupiga kura cha Mkapa kilichopo katika Kata hiyo. Hata hivyo, hawajui alichokuwa akikifanya kituoni humo.

Alidai pia, Msimamizi wa Uchaguzi wa Kata ya Katoro alikamatwa akiwa na sanduku la pesa ndani ya kituo cha kupiga kura.

Hata hivyo, alisema wakati wote huo wamekuwa wakipeleka malalamiko kwa Mismamizi wa Uchaguzi kuhusu vitendo hivyo, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Alisema baya zaidi wao kama chama kilichoshiriki kikamilifu uchaguzi huo, hawakupewa nafasi ya kuwa sehemu ya matokeo yaliyotangazwa jana.

Alisema kati ya fursa walizonyimwa na Msimamizi wa Uchaguzi, ni pamoja na kushirikishwa katika mchakato mzima wa majumuisho ya kura na kujieleza mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi na pia, kupewa nakala ya matokeo ili wayalinganishe na yale waliyoyakusanya katika vituo.

“Sasa nisaini matokeo gani? Hayo ni matokeo ya CCM na Tume, wananchi wa Busanda hawana mbunge, nenda kawaulize, wanamjua mbunge wao,” alisema Magessa.

Kabla ya matokeo hayo kutangazwa, mzozo mkubwa ulitokea katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kati ya viongozi wa Chadema walioongozana na Magessa na Msimamizi wa Uchaguzi, Mollel, Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo na baadhi ya viongozi wa CCM wilaya ya Geita na mkoa wa Mwanza na kutishia kuzuka mapigano.

Mzozo huo uliibuka baada ya viongozi hao wa Chadema kudai wapewe nakala ya matokeo na fursa ya kujieleza mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi, huku Msimamizi huyo pamoja na Diallo na viongozi hao wa CCM wakipinga suala hilo.

Hali hiyo ilisababisha makada wa CCM waliokuwa wakisubiri kuvamia jengo hilo na kuanza kushinikiza matokeo yatangazwe haraka.

Vurugu za wana CCM hao zilitulizwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Elias Kalinga, aliyefanya kazi ya ziada kuwasihi wawe wastahamilivu hadi muda wa kutangazwa matokeo utakapowadia.

Msimamizi wa Uchaguzi alishikilia msimamo wake wa kukataa kutekeleza madai ya viongozi hao wa Chadema, na wao wakasema kwa msimamo huo, matokeo hayo wanayachukulia kuwa ni ya CCM na Tume ya Uchaguzi.

Wagombea wengine waliojitokeza kuwania kiti hicho, ni Oscar Ndalahawa kupitia Chama cha Wananchi (CUF) aliyepata kura 977 (1.03%) na Beatrice Lubambe aliyeambulia kura 271, (0.5%).

Mollel alisema idadi ya watu waliopigakura katika uchaguzi huo, ni 55,460 kati ya watu 135,163 waliojiandikisha kupigakura na kwamba, kura halali zilizopigwa ni 53,309 wakati zilizoharibika ni 2,069.

source: nipashe 26/05/2009

MOSONGA RAPHAEL said...

Mgombea Chadema sasa akubali yaishe-

Aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Busanda wilayani Geita mkoani Mwanza kupitia Chadema, Finias Magesa, ameshindwa kuwasilisha malalamiko yake juu ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi na kueleza kwamba yote anamwachia Mungu. Mgombea huyo juzi alikataa kusaini matokeo ya uchaguzi huo mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi, Dani Mollel, akidai kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi uliofanyika Mei 24 mwaka huu jimboni Busanda.

Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Lolesia Bukwimba aliibuka mshindi kwa kupata kura 29,242 dhidi ya 22,799 za Magesa, hali iliyoonyesha kumchanganya mgombea huyo na baadhi ya viongozi wa chama hicho. Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili katika ofisi ya malipo ya fedha katika halmashauri ya wilaya hiyo jana, mgombea huyo alisema ameamua kurejea Dar es Salaam kuendelea na shughuli zake na kubainisha kwamba yaliyotokea kwenye uchaguzi huo anamwachia Mungu.

“Mimi narudi kwenye shughuli zangu, lakini msimamo wangu ni kwamba siyatambui matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Busanda kwa sababu hayo ni matokeo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na CCM na si ya wananchi wa Busanda, lakini Mungu ndiye atajua afanye nini,’’ alilalamika Magesa. “Mimi kukataa kusaini yale matokeo nilitaka tu ujumbe ufike na naamini ulifika, kwa sababu tumetoa malalamiko mengi sana wakati wa kampeni na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Kwani hata kama nimekataa kusaini yule tayari ni mshindi hakuna njia nyingine, nilichotaka ni kufikisha tu ujumbe kwa wahusika,’’ alisema Magesa. Alisema anachokifahamu yeye ni kwamba wananchi wa Busanda wanamfahamu yeye kama mbunge wao na si kama matokeo yanavyoonyesha kama ilivyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya na kudai hakwenda kwa ajili ya kuupata ubunge, bali kuwasaidia wananchi wa jimbo hilo.

“Sikwenda kugombea ili nipate ubunge…nilichotaka tu ni kuliokoa jimbo la Busanda ambalo naamini kwamba linakwenda kupotea, nilitaka kuwajengea wanafunzi mabweni kwa kila shule ya sekondari, lakini sasa siwezi kufanya hivyo tena,’’ alifafanua. Hata hivyo, katika hatua nyingine mgombea huyo aliwalaumu wananchi wa Busanda kwa kumnyima kura na kumpa mgombea wa CCM na kusisitiza kwamba wataendelea kudidimia kimaendeleo hadi siku ya mwisho huku akisema kama mambo ndiyo yako hivyo, huenda asigombee tena jimbo hilo kwenye uchaguzi ujao.

Hata hivyo alipoulizwa kama hakuhitaji ubunge kwa nini asiendeleze mipango yake ikiwamo ujenzi wa mabweni kwa kila shule ya sekondari, alisema: “Wamenikataa hivyo basi na mimi siwezi tena kuwasaidia”.

source: Habari Leo; Tarehe: 27th May 2009 @ 07:47

MOSONGA RAPHAEL said...

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Kabwe Zitto, alikaririwa kwenye vyombo vya habari akisema licha ya chama chake kushindwa katika uchaguzi huo, wameongeza wapiga kura kutoka asilimia nne mwaka 2005 hadi 44 sasa.

Alisema: “Kwetu sauti ya umma imenena ingawa hatukupata nafasi kuwawakilisha bungeni, matokeo haya yanatupa nguvu ya kuelekea Biharamulo tukiwa na nguvu na imani kubwa”.

Katika hatua nyingine, NCCR-Mageuzi imesema kushindwa kwa vyama vya upinzani Busanda kulitokana na vyama hivyo kutoungana na kusimamisha mgombea mmoja. Ofisa Tawala wa chama hicho, Florian Rutayuga, alisema chama chake kilishaona tatizo hilo na kuvieleza vyama vingine lakini vilipuuza ushauri na hatimaye kukumbana na dhahama hiyo ya kushindwa.

Alivitaka vyama vya upinzani kuwa na desturi ya kukubali matokeo yanapotangazwa na Tume na kutopinga bila sababu za msingi, kwani kufanya hivyo mara kwa mara husababisha migogoro na fujo zitakazoleta maafa katika jamii.


source: Habari Leo; Tarehe: 27th May 2009 @ 07:47