Friday, 22/05/2009
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa wajibu mkubwa wa Watanzania wanaoishi nchi za nje ni kufanya jitihada za kujenga na kuendeleza kwao, ili kuthibitisha ubora wa kuishi kwao nje.
Rais amesema kuwa na wala Watanzania hao wasihangaike na kutafuta jinsi ya kusaidia kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa sababu shughuli hiyo ni wajibu wa Serikali na wanaweza wasiwe na uwezo wa kushiriki katika kuendeleza miradi hiyo mikubwa ya maendeleo.
“Mkiweza kupata mwekezaji mzuri, leteni tu. Mkipata mtu mwenye fedha za kusaidia ujenzi wa miradi mikubwa kama mabarabara na shule leteni, lakini ushauri wangu mkubwa kwenu ni huu… jengeni na endelezeni kwenu kwanza, ili mthibitishe kwa nini ni bora kuishi nje,” Rais Kikwete amewaambia Watanzania wanaoishi katika eneo la Kusini mwa Jimbo la California.
Akizungumza na Watanzania hao leo, Jumanne, Mei 19, 2009, kwenye Hoteli ya Beverly Hills Hilton mjini Los Angeles, Rais Kikwete amesema:
“Ujumbe wangu kwenu ni kwamba msisahau kwenu. Wathibitishie mliowaacha nyumbani kuwa ni bora zaidi kuishi huku mliko kuliko nyumbani. Jengeni kwenu, endelezeni kwenu. Msije kufikia mahali mnarudi nyumbani mkakosa hata mahali pa kufikia,” amewaambia Watanzania hao wanachama wa Chama cha Watanzania Wanaoishi Kusini mwa California.
Rais amewasisitizia Watanzania hao wakati akijibu maswali yao: “Tengenezeni kwenu. Haya makubwa ya ujenzi wa mabarabara, tuachie sisi wa Serikali, ndio maana tupo. Hatutaki kuwasumbua kwa masuala ya ujenzi wa barabara na shule. Hii ndiyo kazi na wajibu wetu. Nyie jengeni kwenu, ili ndugu zenu wajue kuwa kuishi kwenu nje kuna maana.”
Rais Kikwete ambaye amekutana na kuzungumza na Watanzania hao baada ya kuwa amewasili mjini Los Angeles akitokea mjini San Francisco ambako alianzia ziara yake ya Marekani pia ametumia muda mwingi kuelezea mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali yake ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule 2,700 za sekondari katika miaka mitatu iliyopita.
Rais amezungumzia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya, ujenzi wa barabara, akisisitiza kuwa, kwa mfano, kiwango cha malaria nchini kimepungua kwa kiasi cha asilimia 38 katika miaka mitatu kutokana na maamuzi ya Serikali tokea iingie madarakani.
“Ni kweli kuwa malaria inabakia ugonjwa unaoua watu wengi zaidi nchini, lakini hatua tulizozichukua katika miaka mitatu, minne iliyopita, zimepunguza kiwango cha malaria kwa asilimia 38. Katika Zanzibar ni kama tumemaliza ungonjwa huo kabisa.”
Rais pia amewaeleza Watanzania hao kuhusu mpango mkubwa wa Serikali kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata nchini akiongeza:
“Hata kwa yale magonjwa ambayo tumekuwa tunalazimika kuwapeleka watu nje, tunachukua hatua. Kwa mfano, Wachina wamekubali kutujengea hospitali kubwa ya kutibu magonjwa ya moyo.”
(Source: Ikulu Mawasiliano (Blog). Tuesday, May 19, 2009)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment