Tuesday, May 12 2009
Nimeshawahi kuandika mara kadhaa kuhusu mbwa wa Ulaya hasa Uingereza wanavyothaminiwa na hata kuliko binadamu. Sina haja kurudia hayo kwa leo, ila hebu sikia mkasa uliotokea wiki hii.
Bwana mmoja, mkewe pamoja na mtoto wao mchanga wa miezi saba na mbwa wao wawili walikuwa matembezini kando ya mto. Mara mbwa mmoja akajirusha mtoni, na wa pili nae akaingia mtoni. Mto ulikiwa umejaa maji na yanaenda kwa kasi baada ya mvua kunyesha siku za karibuni. Kuona hivyo, mke wa jamaa akajitosa majini kuokoa mbwa. Unajua maji yatiririkayo mitoni huku Uingereza ni ya ajabu sana. Unaweza kuona kama yametuama au kina si kirefu lakini mtu akianguka mtoni mara nyingi huwa anapoteza maisha! Sababu hasa ni kuwa maji huwa yana mkondo uendao kwa kasi ambao hauonekani kwa juu. Pili maji huwa ni ya baridi sana kiasi kwamba hata kama mtu ni mtaalamu wa kuogelea, inamuwia vigumu kuhimili ubaridi na kusababisha viungo muhimu vya vya mwili hushindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na ubaridi - matokeo yake ni mtu kuzama na kupoteza maisha!
Baada ya mama mtu kujitosa majini, alizidiwa nguvu na mkondo wa maji na hivyo kumfanya mzee mzima naye ajitose mtoni kusaidia mama na mbwa wao! Jamaa nae baada ya kuingia majini mambo yakawa yaleyale, alizidiwa na kusombwa na maji! Wote na mbwa wao wakamezwa na kondo mkali wa mto. Baada ya jitihada za uokoaji kufanyika, mama mtu alipatikana huku akiwa hoi bin taabani, na mwili wa mzee ulipatikana mtoni baadae akiwa ameshafariki. Mbwa wao pia walikufa! Hata hivyo mama mtu nae alifariki dunia hospitalini kutokana na madhara ya ubaridi.
Kando ya mto alibakia mtoto mchanga wa miezi saba, akiwa kwenye kitoroli cha kusukumia watoto! Ndie tu aliyebaki, na bahati mbaya hawezi hata kusimulia kilichotokea maskini!!
Kutokana na mkasa huu, Waingereza wameanza kuuulizana inakuwaje wanyama wafugwao (pets) wawe na umuhimu kuliko maisha ya binadamu? Je huyu mtoto atakapokuwa mtu mzima na kusimuliwa kilichotokea atawaelewaje wazazi wake?
.....................................
Tuesday, 12 May 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Soma hapa chini habari nilizokwishaandika awali kuhusu maisha ya mbwa wa ulaya (Uingereza)
........
Friday, 25 April 2008
Mnyama mbwa wa Ulaya!
Mbwa ni mnyama ambae anathaminiwa na wengi nchini Uingereza. Anapewa matunzo ya hali ya juu na anaishi ndani ya nyumba (na sio nje kama sisi Afrika tulivyozoea kufanya)!
Jana jamaa mmoja alisema ktk mahojiano kuwa, 'choosing a dog is like choosing your partner, because dog is for life ...'*
Yaani mbwa anatunzwa na kuthaminiwa kama vile binadamu. Bajeti yake ya matunzo ni kubwa kuliko bajeti zetu ktk kaya nzima, ukizingatia hali yetu kiuchumi Bongo.
Haya nayo ni maisha!
(* mahojiano ktk kipindi the one show, kituo cha televisheni bbc-one)
Posted by MOSONGA RAPHAEL 25/04/2008
..........
Friday, 27 February 2009
Almunia wa Arsenal
Juzi golikipa namba wani wa Arsenal aligeuka kichekesho ktk vyombo vya habari Uingereza baada ya kuibuka njiani akitembeza* mbwa mitaani.
Wenyeji wanasema kuwa aina ya mbwa aliyekuwa nae kipa huyo huwa ni kwa ajili ya kina mama (wanawake). Kwa utamaduni wa wenyeji, wanaume hawatembei na mbwa wa aina hiyo. Vyombo vya habari (TV, radio na magazeti) vilimchora sana.
*Zingatia:
Ni kawaida kwa watu (Uingereza) kuwapeleka mbwa matembezini karibu kila siku. Mbwa wa Uingereza hutunzwa vizuri na pia wanawekewa bima endapo wapata matatizo.
Kuwa na mbwa kunaweza kuwa ni gharama sana kwa mtu wa kipato cha kawaida na hairuhusiwi kumuacha nyumbani bila uangalizi wowote. Rafiki yangu mmoja alikuwa akisafiri toka Reading hadi Bracknell (mwendo wa dk 20, A329-Motorway) kumpeleka mbwa kwa dada yake (amwangalizie) wakati anapoenda kazini halafu anampitia mbwa jioni baada ya kazi!
Halafu kwa bahati mbaya au nzuri mbwa hawa huishi ndani ya nyumba mchana na usiku, sio nje kama tulivyozoea Afrika.
Kuna matukio kadhaa yaliyokwisha ripotiwa ambapo mbwa wameua watoto wachanga, na wakati mwingine watu wazima nao wamechanwa sura zao na mbwa!
Posted by MOSONGA RAPHAEL, 27/02/2009
..........
Post a Comment