Jumatano 20/05/2009
Nakumbuka zile hadithi ktk vitabu nilizozisoma wakati nilipokuwa mdogo. Karibu kila kitabu nilichosoma kilianza na huu msemo; 'hapo zamani za kale paliondokea ....'
Hasa nakumbuka hadithi za kitabu fulani kilichokuwa na hadithi 3 nzuri! Sura ya kwanza ilikuwa na kichwa 'Mkataa pema pabaya panamwita'. Sura ya pili ilikuwa na ' ... jamani fungeni mkutano wengine zimeyeyika' - ile ambayo fisi alihudhuria mkutanao wa wanyama wenye pembe huku yeye akiwa amejiwekea pembe bandia na kugundisha na nta. Muda ulipokwenda sana nta ikaanza kuyeyuka na akahofia kuwa 'pembe' zitadondoka na hivyo akatoa hoja mkutano ufungwe! Sura ya tatu ilikuwa na kichwa 'usitukane wakunga na uzazi ungalipo'.
Kitabu kingine kilihusu hadithi za usukumani ambako kuma mtu alikuwa akisafiri anaaacha maziwa 'fresh' kwenye kibuyu au bakuli, na kwa muda wote atakapokuwa safarini 'salama' maziwa yanabakia 'fresh' na kama akipata tatizo au kufariki maziwa yanaganda! Hii ni hadithi ya Mwanamalunde. Siikumbuki vizuri ila kwa mbali nakumbuka maudhui yake!
Natamani wanangu kama angepata nakala moja ili aone tulichosoma enzi zetu tulipokuwa na umri kama wake. Na kwa kweli vitabu hivi na vingine vya aina hiyo vyafaa kuhifadhiwa kwa ajili ya kumbukumbu ya vizazi vijavyo.
Kila kizazi kinanao wajibu wa kutunza mabaki ya kumbukumbu za shughuli na maendeleo yake (legacy) kwa ajili ya vizazi vijavyo. Na huu ni wajibu wa kila mtu binafsi na wadau mbalimbali! Kwa kuanzia mie nina kumbukumbu za kazi zangu zote za darasani (daftari za mazoezi na karatasi za mitihani) kuanzia nilipokuwa darasa la kwanza elimu ya msingi. Na bado ninaendelea kuhifadhi kumbukumbu zaidi za kazi zangu. Tayari mwanangu ameshaanza kunicheka sana kila anapoona kazi yangu ya darasa la pili (analosoma sasa), kwa sababu anaona nimekosa maswali rahisi mno au mwandiko wangu wa ajabu enzi hizo! Nadhani mwanangu atajifunza kutokana na makosa yangu kama anavyoyaona mwenyewe kwa macho yake bila kusimuliwa au kuambiwa!
Wednesday, 20 May 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment