Saturday, 30 May 2009

Jicho la 3

Ili tuendelee watanzania tunatakiwa tuwe wawazi na wakweli. Hakuna kitu kibaya kama unafiki wa kusifia hata pale panapoonekana kabisa kuna dosari.

Wananchi, ambao kwa kweli ni wanyonge, wanahitaji watu ambao watasimama kidete kuwatetea na kulinda haki zao. Wananchi hawahitaji mtu wa kuwagawia hela njiani. Wananchi wahitaji haki yao iwepo wazi. Kila stahili yao ni lazima ipatikane kwa uwazi bila kuzungushana hasa hasa huduma za kijamii kama vile hospitalini, shuleni, maofisini n.k. Watendaji wasizitoe kama vile ni 'favour'. Kuzungushana-zungushana ndio mwanzo wa kuchochea rushwa.

Serikali yetu nayo inahitaji msukumo kutoka pembeni. Tusijidanganye eti kwa kuisifia ndio tutaonekana 'wazuri' mbele yake. Tena wakati mwingine serikali hushukuru inapomulikwa utendaji wake. Kama kuna udhaifu ndani ya vyombo vya utendaji au watendaji serikalini, ni lazima usemwe na kukemewa vikali.

Kama serikali yetu inafanya vizuri kazi yake mimi nitakuwa mtu wa kwanza kuisifia au kuipongeza. Lakini kama serikali inafanya 'madudu' na kukiuka ahadi ilizozitoa ktk ilani ya chama chake wakati wa uchaguzi mkuu, mimi nitakuwa miongoni mwa wataoisema na kuilaumu. Hakuna cha urafiki ktk kulinda maslahi ya Taifa letu. Wale wenzetu walioko serikalini wakumbuke kuwa wako pale kwa ajili ya kusimamia rasilimali za Taifa na kutuongoza ili tujikomboe kiuchumi na kimaendeleo. Na tunataka maendeleo ya Taifa yatafsiriwe kupitia ustawi wa maisha ya wananchi kwa ujumla.

Ndio maana nasema kuwa ni wajibu wa serikali kuongoza nchi kwa misingi inayokubalika. Haki, uhuru na stahili za wananchi zisitolewe kama fadhila.

Mwisho, tusisahau kujikumbusha hotuba muhimu za watangulizi wetu. Kwa ujumla karibu hotuba zote za Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere ni nzuri, ila kama nafasi hairuhusu napendekeza turejee hotuba mbili. Ya kwanza ni ile aliyokuwa anaongea na waandishi wa habari mwaka 1994, na hotuba ya pili, kwa mapendekezo yangu, ni ile ya kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kitaifa mjini Mbeya (Uwanja wa Sokoine) mwaka 1995. Naye Rais mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliwahi kutoa hotuba nzuri ktk NEC ya Chama Cha Mapinduzi au Bungeni (sina hakika) -aliipa hotuba hiyo kichwa cha 'The Courage of Leadership' (na inapatikana ktk tovuti ya Chama Cha Mapinduzi). Huu ni urithi mzuri kwetu na kwa vizazi vijavyo.

2 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKK), Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKK), Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, amewataka watanzania wasisite kukemea vitendo vya rushwa na ufisadi na kumuunga mkono kila aliyepewa ujasiri na Mungu kujitoa mhanga katika kukemea ili vita iwe endelevu.

Dk. Shao aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ibada maalum iliyofanyika katika kanisa la Kisereni Evangelical Lutheran Church, ELCT, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Kila mtu nchi hii ana haki na wajibu wa kupambana na vitendo vya rushwa, lakini Mungu amewapa ujasiri watu wachache ambao wamekuwa mstari wa mbele kukabiliana na ufisadi, hivyo tunapaswa kuwaunga mkono kuhakikisha wanaendelea na kazi hiyo," alisema.

Alimsifu Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, kwa uamuzi wake wa kuwataja watuhumiwa wa ufisadi papa hadharani na aliwataka wengine kuiga mfano huo.

“Tunakusifu na tunakusihi usirudi nyuma bali uendelee na moyo huo wa kuipenda nchi yako," alisema akimgeukia Mengi ambaye alishiriki katika ibada hiyo.

Dk. Shao aliwataka watanzania kuwa makini katika Uchaguzi Mkuu unaokuja mwakani na kujiepusha na kuwachagua wagombea wanaotoa rushwa. Alisema ana imani kubwa kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu Tanzania itashinda vita dhidi ya rushwa.

Askofu Shao aliwaonya watu aliosema wamemejitokeza hivi karibuni na kueneza uongo kuwa Mengi anataka kuwamia urais mwakani.

Alisema anavyoamini, Mengi hajawahi hata kuwa na wazo la kuwania urais na hata siku moja hatawania nafasi hiyo.

“Kama angekuwa kweli anataka urais angeshakuja kwetu kutuomba kura lakini sijawahi kumuona akifanya hivyo na amekuwa akijikita zaidi kuwasaidia watanzania ili waondokane na umaskini," alisema.

Kwa upande wake, Mengi alilalamikia kitendo cha kunyanyaswa na vyombo vya usalama tangu ataje majina ya mafisadi papa.

Alisema amekuwa akinyanyaswa na vyombo hivyo vikimtaka atoe uthibitisho ya tuhuma alizotoa.

Mengi alitaja vyombo ambavyo vimeshamhoji kuwa ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Kamati mbalimbali za usalama.

Alisema pamoja na usumbufu huo, hatosita kuendelea na kupambana na ufisadi kwani ana uhakika kuwa anaungwa mkono na Rais Jakaya Kikwete, Mungu na watanzania.

“Nimetengeneza maadui wengi tangu niingie katika mapambano dhidi ya ufisadi, hivyo nawaomba mniombee ili maadui wangu wasifanikiwe," alisema.


CHANZO: NIPASHE, 2nd June 2009.

MOSONGA RAPHAEL said...

"tabia ya ‘Mkubwa’ kuwa ndiye kisima cha hekima imejengeka hadi kupindukia kama utamaduni wetu"
-rai ya jenerali, raia mwema juni 10-16 toleo na. 85