Monday, 18 May 2009

Vingunge wetu eee, wapi vitendo?

Mzee wa Changamoto ameniunga mkono kuhusu tabia za viongozi wetu kupiga domo tu bila kuzingatia hali halisi ya maisha ya mwananchi na ahadi hewa kila baada ya miaka mitano (wanaonekana kabla/kwenye kampeni za chaguzi, na baada ya chaguzi wanatokomea!)
Kuna vitu vingine ni vidogo sana lakini vya muhimu kwa maisha ya mwananchi. Sio vizuri kuvipuuza kwa sababu ya udogo wake. Kinachotakiwa ni usimamizi wa karibu, uwepo wa sera zenye umakini, uaminifu kitaaluma (professionalism) na utekelezaji wa ahadi kivitendo. Wananchi sio wajinga, wanaelewa kile kinachosemwa na viongozi wetu na pia wanajua kutofautisha mbivu na mbichi!

..............................................

Mzee wa Changamoto anena zaidi:

Amani, Heshima na Upendo kwako Ndugu.
Wanachonishangaza Ndugu hawa wakuu ni namna ambavyo wanaangalia "nje ya ulingo waliomo" ambao ndio uliooza.
Hakuna atakayegoma kukaa kijijini kama huduma zote muhimu zitapatikana. Kama kutakuwa na mazingira ya kumfanya aweze kuuza japo bidhaa zake. Lakini wanaendekeza siasa na kujiandaa kusikika kuliko kutekeleza. Hashangai kwanini watu wanauza pombe badala ya shughuli ambazo wao wanaweza kudhani ni za kuwapatia kipato zaidi? Hawaoni kwanini watu wamechoka kuwasiliza, wanawazomea na kuwaona waongo kama niwaonavyo mimi. Ni kwa kuwa wanasema wakijua TBC iko pale lna hakuna atakayehoji wala kutaka ufafanuzi wa ahadi walizotoa wiki mbili zijazo.
Ni upuuzi kuona Waziri Mkuu hamuwajibishi mkuu wa sehemu hiyo (awe wa wilaya ama mkoa) kujua ni kipi kinachokwamisha maendeleo ya wananchi.
Ni lazima tuwe na mikataba, kuwa mtu anapokubali kuchukua kazi kama ya ukuu wa mikoa awe na ahadi ya kufanya vitu kadhaa ndani ya muda fulani, na akishindwa na aachie ngazi. Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ni kati ya watendaji wabovu zaidi nchini Tanzania.
Waziri aanze na wasaidizi wake kabla hajawaendea wale walioshindwa kuwezeshwa wakaamua kujiwezesha.
Shukrani kwa kazi njema

No comments: