Friday, 10 October 2008

Tarime, yaliyotokoea yasirudiwe tena!!

Hali na maendeleo ya kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Tarime, Mara sio shwari.

Kwa kweli tangu wakati wa mazishi ya aliyekuwa mbunge marehemu Chacha Wangwe hali haikuwa ya kuridhisha kiusalama.

Vurugu na vitendo vya uvunjaji wa sheria (umwagaji damu) vimetawala mazungumzo na matangazo ktk vyombo vya habari. Watanzania na dunia kwa ujumla walitegemea kusikia au kuona kampeni majukwaani huku kambi za vyama husika zikitoa hoja na sera zenye manufaa na za kuboresha maisha ya wana-jimbo, lakini badala yake siasa zimegeuka uhasama na uadui hadi vitendo visivyo vya kiustaarabu na vya uvunjaji wa sheria vikishika kasi na kutawala kampeni na kuonekana vya kawaida!

Naomba vyombo vya dola viwe makini ili kulinda usalama wa kila mwana jimbo bila kujali itikadi za vyama au ushabiki wa kisiasa. Kila mwananchi alindwe na pale wanapotokea wakorofi wanaovunja amani na ustaarabu ni vizuri wachukuliwe hatua za kisheria.

Ikiwa imebakia siku moja tu kabla ya uchaguzi, ningependa kuona habari zinazotawala kurasa za magazeti au ktk vyombo vya habari kwa ujumla zikiwa ni siasa, sera na mikakati ya uchaguzi na sio za kuongelea mapigano au umwagaji damu!

Mimi sitoki wilaya ya Tarime ila natoka mkoa mmoja na Tarime. Kwa kweli vitendo vilivyotokea Tarime hivi karibuni na hasa jana (kukatana mapanga usoni) ni vya aibu sana katika dunia ya leo. Hii aibu ni yetu wote hasa tunaotokea mkoa huo kwani tumeona chaguzi nyingi sana nchini Tanzania tangu siasa za vyama vingi ziliporuhusiwa lakini hatujawahi kusikia damu inamwagika isipokuwa Tarime! Tabia hii naikemea na kuipinga kwa nguvu zote hasa ukizingatia muasisi wa Taifa letu, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, anatokea mkoa wetu, na hizi aibu pia zitakuwa zinamgusa kwa namna moja au nyingine. Inabidi tumuenzi Baba wa Taifa kwa kuonyesha ustaarabu na ukomavu kisiasa na pia kudumisha yale mema aliyotufundisha au kuyaonyesha enzi za uhai wake.

Kama watu tunatofautiana ktk hoja au suala lolote zipo njia muafaka za kufikia maafikiano kwa amani na kwa ustaarabu. Au ikishindikana kuafikiana 'watu hukubaliana kutokubaliana' kwa amani, sio kwa ncha ya upanga!

4 comments:

MOSONGA RAPHAEL said...

Damu yakaribisha helikopta ya CCM

2008-10-10 13:35:41
Na Mashaka Mgeta, Tarime


Wafuasi wanaoa minika kuwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamewapiga na mmoja wao kuwakata kwa mapanga vijana wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini hapa.

Mmoja wa vijana hao, Genya Sabai (28), mkazi wa Nkende, alikatwa kwa panga kuanzia pembeni mwa sikio kwenye taya la kushoto, hadi sehemu ya chini ya kidevu.

Sehemu ya nyama katika eneo lililoathirika kuning\'inia, hadi alipofikishwa katika zahanati ya Tarime na kushonwa nyuzi 19.

Mganga Mfawidhi wa zanahati ya Tarime walipofikishwa majeruhi hao, Dk. Philemon Hungiro, alisema Sabai alishonwa katika tabaka mbalimbali za ndani na kushonwa nyuzi 19 za nje.

Haikufahamika mara moja sababu za majeruhi hao kupelekwa katika zahanati hiyo badala ya hospitali ya Wilaya ya Tarime inayomilikiwa na serikali.

``Amejeruhiwa sana na inaonekana dhahiri kwamba jeraha hilo limetokana na kukatwa kwa panga,`` alisema Dk. Hungiro.

Majeruhi wengine katika tukio hilo ni Athuman Seleman (22), mkazi wa Rusoti mjini hapa, aliyekatwa katika kiganja cha mkono wa kushoto, Mahende Joseph Daniel (25) na Mashamu Edward (23) ambaye ni bubu, aliyekatwa sehemu ya nyuma ya shingo yake.

Kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu waliofika katika zahanati hiyo, kuwajulia hali majeruhi hao.

Miongoni mwa watu waliofika kuwajulia hali majeruhiwa hao, ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wagombea ubunge na udiwani kupitia chama hicho, Charles Mwera na John Heche.

Dk. Hungiro, alisema hali ya Sabai ilikuwa mbaya sana, hali iliyosababisha uongozi wa zahanati hiyo kumfungia wodini kwa kutumia kufuli kubwa, ili watu wasiingie ndani.

Utoaji huduma za tiba ulisitishwa kwa muda katika zanahati hiyo, kutokana na wauguzi wake kufanya kazi ya ziada, kuwatoa nje na kuwazuia kuingia ndani ya zahanati hiyo.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa majeruhi hao, Seleman, alisema walifika katika uwanja wa mpira Serengeti, ili kuweka uzio wa kamba, kuwazuia watoto wasiingie katika eneo lililotarajiwa kutua helikopta inayotumika katika kampeni za Chadema.

Seleman alisema baada ya kufika katika eneo hilo, walikuta wafuasi wa CCM wakiburudishwa na kikundi cha Tanzania One Theathre (TOT), na walianza kuweka kamba kuzunguka eneo itakapotua helikopta.

``Tulikuwa tunaweka uzio wa kamba, wakatokea watu kutoka katikati ya umati wa wafuasi wa CCM, wakaanza kutupiga na mmoja wao akatukata kwa panga, tunamjua kwa sura,``alisema, alipohojiwa kabla ya kupata tiba katika zahanati hiyo.

Hatua ya CCM kimejibu mashambulizi na kuanza kampeni zake kwa kutumia helikopta katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime mkoani Mara.

Helikopta hiyo ilitua jana mchana katika uwanja wa mpira wa Serengeti na kulakiwa na washabiki wa chama hicho waliovalia sare zao huku wakitumbuizwa na kikundi burudani cha chama hicho Tanzania One Theatre (TOT).

Helikopta hiyo yenye namba za usajili 5YMNW inayomilikiwa na kampuni ya Titan Air Ltd ya Nairobi, Kenya ilikuwa ikiendeshwa na rubani Sigilaia Evans.

Baada ya ndege hiyo kutua ilipambwa na mabango yenye kuwahamasisha wananchi kumchagua mgombea wa ubunge kupitia chama hicho, Christopher Kangoye.

Mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, John Komba alisema kampeni hizo hivi sasa zitakuwa rahisi.
Mwanzoni mwa wiki hii, Chadema walianza kampeni kwa kutumia helikopta.

Kuhusu purukushani kati ya wafuasi wa CCM na Chadema, baadhi ya watu walioshuhudia, walisema palikuwa na malumbano kati ya majeruhi hao na wafuasi wa vyama hivyo kabla ya kufanyika kwa shambulio hilo.

Mkazi mmoja wa Tarime aliyekuwa katika eneo hilo, Richard Chacha, alidai kuwa, Mashamu ambaye ni bubu, alijeruhiwa wakati akipita karibu na eneo hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mtu aliyewakata kwa panga majeruhi hao, aliondoshwa kutoka katika eneo hilo, kwa kutumia gari aina ya Nissan Patrol, linaloaminika kuwa mali ya mmoja wa wagombea udiwani wa kata ya Tarime mjini.

Hata hivyo, Nipashe ilipofika katika eneo la tukio, ilikuta magari mawili ya polisi wenye silaha za mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto, wakifanya doria na kukamata baadhi ya watu kwa ajili ya kuwahoji.

Wakati huo, wananchi waliokuwa katika eneo hilo, walianza kupiga kelele wakiwaonyesha askari hao gari linalodaiwa kumbeba mtuhumiwa wa shambulio hilo.

Gari hilo liliondoka kwa kasi kutoka uwanjani hapo, bila askari hao kuchukua hatua yoyote kulizuia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Liberatus Barlow, alisema mtuhumiwa wa shambulio hilo alitoroshwa kwa kutumia gari lenye namba T 910 ALF, lakini mashuhuda waliokuwa katika eneo la tukio wametaja namba za gari hilo kuwa ni T 910 AVE.

Wakati huo huo, Barlow alisema watu wawili wanashikiliwa na polisi, wakituhumiwa kupanga njama za kufanya shambulio kwa kutumia mapanga.

Aliwataja watu hao waliokamatwa wakiwa na silaha hizo kuwa ni Wangwe Ryoba na Menganyi Ryoba anayesadikiwa kuwa raia wa nchi jirani ya Kenya.

Aidha, Barlow alisema watuhumiwa wa vurugu za kisiasa katika kampeni za uchaguzi mdogo, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, watafikishwa mahakamani baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo.

Barlow alisema polisi imefanikiwa kukamilisha baadhi ya uchunguzi na kwamba kuna watu na baadhi ya viongozi wa siasa, walioguswa na ambao hawawezi kunusurika kufunguliwa mashitaka.

``Kwa hili hatumuogopi mtu, kwa maana hata sisi polisi tunapofanya kosa, tunakiona cha moto, hivyo hatutamuonea haya mtuhumiwa yeyote,`` alisema.

Waitara aitahadharisha CCM na siasa za makundi

Aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), mkoa wa Tanga, Mwita Mwikwabe Waitara, amedai kuwa Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba, wanaendeleza siasa za makundi ndani ya CCM.

Alisema kutokana na hali hiyo, hakuna fursa kwa CCM kuepuka migogoro ya mara kwa mara inayozidi kukidhoofisha chama hicho kilichodumu madarakani tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977 kikirithi madaraka hayo kutoka kwa Tanu na ASP vyama vilivyoleta uhuru na kuungana mwaka huo.

``Mimi nimeondoka CCM, lakini ninamwachia salaam Rais Jakaya Kikwete, kwamba Makamba na Nchimbi bado wanaendeleza siasa za makundi ndani ya chama hicho,``alidai.

Alidai kuwa, miongoni mwa ishara za viongozi hao kuendeleza makundi, ni jinsi walivyomuondoa katika wadhifa wa Ukatibu wa UVCCM mkoani Tanga, na kumhamishia kuwa Katibu Msaidizi wa Dk.Nchimbi.

Hata hivyo, Waitara alikataa kutumikia wadhifa huo mpya, na kuapa kuwa, hawezi kukanyaga katika ofisi ya Nchimbi, labda akiwa maiti.

Waitara alijiondoa CCM na kujiunga Chadema katika mkutano wa hadhara wa kampeni, uliofanyika mjini Sirari juzi.

Kabla ya kujiondoa CCM, Waitara aliyewania nafasi ya kutaka kugombea ubunge jimbo la Tarime na kushika nafasi ya tatu, alikosoa mwenendo wa kampeni za chama hicho na matumizi makubwa ya nguvu za jeshi la polisi mjini hapa.

Pia, Waitara alidai kuwepo mkakati ndani ya CCM, kufanikisha kuwa wagombea wake wa ubunge na udiwani, Christopher Kangoye na Peter Zakaria wanashinda.

``Mkakati huo niliujua nikiwa CCM, lakini wanahangaishwa na msimamo wa wananchi wa Tarime, nimeungana na wanachi hawa na tutapambana kuhakikisha kuwa tunalinda haki na kura zetu,`` alisema.

Naye Muhibu Said anaripoti kuwa, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), umeitaka serikali na Watanzania kushirikiana ili uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Tarime, ufanyike kwa amani.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum mara baada ya kuzindua maonyesho ya filamu za EU, katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam jana, Kiongozi wa Umoja huo nchini, Jacques Champagne de Labriolle, alisema anatoa ushauri huo kwa vile wameona kuwa uchaguzi huo uliandaliwa kwa haraka, jambo ambalo linachangia kuchochea uvunjifu amani.

``Uchaguzi wa Tarime haujaandaliwa vizuri, kwani haiwezekani baada ya kifo tu, siku chache unaandaa uchaguzi.

Hivyo, kuna umuhimu wa kuwapo uwajibikaji wa pamoja kati ya serikali na wananchi ili kuhakikisha amani inapatikana katika uchaguzi,`` alisema de Labriolle.

Uchaguzi huo, ambao unatarajiwa kufanyika keshokutwa, unafuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, marehemu Chacha Wangwe (Chadema) aliyefariki dunia Julai 28, mwaka huu kwa ajali ya gari katika eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa, mkoani Dodoma.

Hata hivyo, de Labriolle ambaye ni Balozi wa Ufaransa nchini, alisema EU imepeleka timu yake maalum kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi huo na kwamba, tayari imeshaongea na wagombea wote kuhusu uchaguzi huo.

Wanaogombea ubunge katika uchaguzi huo na vyama wanavyotoka kwenye mabano, ni Charles Mwera (Chadema), Enock Harun (NCCR-Mageuzi), Christopher Ryoba Kangoye (CCM) na Benson Makanya (DP).

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...

Habari za Tanzania Jumamosi Okt 11, 2008
Imetolewa mara ya mwisho: 11.10.2008 0020 EAT•

CCM yaomba radhi Tarime
Na Richard Mwaikenda, Tarime

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimewaomba radhi wananchi wa Tarime kutokana na vurugu zilizotokea kwenye uwanja wa Sabasaba na kusababisha wafuasi wanne wa CHADEMA,
kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa CCM wakigombea uwanja huo ili helikopta za vyama hivyo zitue.

Maombi hayo yalitolewa jana na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Kapteni mstaafu John Chiligati katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Tarime, mjini hapa.

"Tumesikitishwa na tukio hilo lisilo la kistaarabu ambalo limesababishwa na vijana wa vyama hivyo, kila upande kugombea uwanja huo ukitaka helikopta zao zilizokodiwa na vyama hivyo kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mdogo zitue kwenye uwanja huo,” alisema Kapteni Chiligati.

"Licha ya uwanja huo CCM kuomba siku hiyo, nasikia vijana wa CHADEMA, walivamia na kuweka kamba na bendera nyekundu, ili ndege ya CCM isitue kwenye uwanja huo na kutaka ndege yao iruhusiwe kutua, hali ambayo ilizaa mabishano na kusababisha kupigana mapanga,” alisema.

Alisema si kwamba tukio hilo lilipangwa, bali lilitokea kwa bahati mbaya, hivyo si busara kuanza kunyoosheana vidole.

Kapteni Chiligati, alitoa mwito kwa vyama vya siasa kuacha tabia ya kuchokozana na kusababisha vurugu na
kuwataka viongozi wao wakiwa kwenye kampeni, kueleza sera za vyama vyao.

Alisema kampeni za kuchafuana, kuleta fujo ni za kihuni na kwamba hukumu ya chama chochote kinachofanya
hivyo ni siku ya uchaguzi kwa wananchi kukinyima kura.

Kapteni Chiligati alikanusha fununu zilizoenea
kuwa CCM inamtumia Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, kusaidia kampeni za chama hicho katika uchaguzi huo.

Alisema ni matusi kwa CCM kwamba inamhonga Mchungaji Mtikila ili awasaidie katika kampeni hizo na kwamba
hawawezi kufanya hivyo, kwani chama hicho kina mtaji wa kutosha wa wanachama zaidi ya milioni 4.

(source: majira 11/10/008)

MOSONGA RAPHAEL said...

Maoni ya mhariri -Nipashe

Chonde chonde Polisi, sasa dhibitini umwagaji damu huu

2008-10-10 12:49:28
Na Mhariri


Kwa mara nyingine tena, damu imemwagika katika harakati za kampeni za kuwania kiti cha ubunge jimbo la Tarime baada ya watu watatu kuchomwa visu kwa kile kinachoelezwa kugombea eneo la kutua kwa helikopta za vyama vyao jimboni humo.

Tunasikitika kwamba kadri siku zinavyosogelea tarehe ya kupiga kura, Oktoba 12, 2008 yaani keshokutwa, hali ya usalama inazidi kuwa tete licha ya Jeshi la Polisi kumwaga askari wengi jimboni humo. Matukio ya kupigwa watu, na hata wengine kupoteza maisha kwa sababu tu ya ushabiki wa vyama yamekuwa ni ya kawaida kabisa.

Tuliandika tena katika safu hii, tukiasa na kuchagiza Jeshi la Polisi kufanya kazi kama walinda usalama waliobobea katika taaluma hiyo. Tulisema Polisi ndio wanaweza kusababisha ama uchaguzi huu mdogo wa ubunge na udiwani uwe huru au kinyume chake.

Tulisema hayo kwa sababu moja tu. Kwamba kulikuwa na malalamiko makubwa dhidi ya Jeshi la Polisi kwamba inaegemea upande mmoja.

Polisi wamelaumiwa kwamba wanawasumbua wagombea na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); lakini polisi nao wamejitetea kwamba wafuasi wa chama hicho wanachokoza dola.

Pamoja na malalamiko haya, jana wananchi watatu wameumizwa vibaya kwa kuchomwa visu, wengine tunapozungumza wanauguza majeraha yao makubwa waliyopata, chanzo cha kuumizana wananchi hao wanodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, ni ugomvi wa uwanja wa kutua helikopta za vyama vyao.

Tunaamini, kwamba Polisi walijua kwamba uwanja uliokuwa itue helikopta ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni upi, na pia helikopta ya Chadema ingetua wapi, kwa maana hiyo ingekuwa imeimarisha ulinzi kiasi cha kutosha.

Tunasema ulinzi kiasi cha kutosha kwa sababu idadi ya askari waliomwagwa Tarime wanatosha kwa kila kitu.

Kwa hali hiyo, polisi wangekuwa wamesimamia jinsi uwanja huo ungehakikishiwa usalama wa helikopta hizo, na kwa kweli hata hao wafuasi wanaodaiwa wa CCM na Chadema wasingepata huo upenyo wa kupambana kiasi cha kuumizana na damu kumwagika.

Ni kwa kutafakari hali hii tunashindwa kujua kama Polisi walioko Tarime wanafanya kazi yao sawasawa kiasi cha wananchi kutembezeana visu mbele yao. Hali hii inatufanya tujihoji kama kweli polisi hawa wapo Tarime kuimarisha usalama au wapo tu kuonekana wapo.

Tunajua kwamba polisi waliko Tarime wana zana zote za kazi, picha mbalimbali ambazo zimeonekana magazetini na kwenye luninga, zinathibitisha uwezo huo wa kizana na wingi wa kutosha, sasa kama wanashindwa kuthibiti usalama wa uwanja unaotua helikopta, tuseme watathibiti watu walioko mafichoni?

Kabla ya kupiga kura Jumapili hii, zimebakia siku mbili tu za kampeni. Hizi ni dakika za lala salama ndiyo maana vyama vyenye ushindani mkali, yaani CCM na Chadema, wameamua kutumia helikopta kuvuta wananchi wengi zaidi hivyo kujizolea kura siku ya mwisho; kwa maana hiyo tulidhani kwamba na polisi nao wamejipanga kwa mkao huo huo kujiimarisha kiulinzi ili kuhakikisha kwamba kadri joto la uchaguzi huu linavyoelekea kileleni, vitendo kama hivi vya jana vinakuwa adimu.

Tuaamini Polisi wana wajibu wa kwanza kabisa wa kulinda maisha ya wananchi na mali zao.

Tunaposema maisha tunakusudia pia usalama wa miili yao, ikiwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayemshambulia mwenzake, hakuna anayedhuru mwili wa mwenzake kwa hali yoyote ile.

Kwa maana hiyo kuendelea kutokea kwa vitendo vya mapigano hasa vya kutumia sila za jadi kama vizu na mapanga, kwetu tunaona kama Polisi hawajaweza kudhibiti hali ya Tarime.

SOURCE: Nipashe

MOSONGA RAPHAEL said...

Mawazo ya Mbatia ni sahihi, nayaunga mkono! -Mosonga.

Imetolewa mara ya mwisho: 06.10.2008 0140 EAT

Mbatia: Upinzani ushindane kwa hoja

Na Richard Mwaikenda, Tarime

MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi, Bw. James Mbatia amesema upinzani wa kisiasa Tanzania usiwe wa kupigana bali uwe wa kushindana kwa hoja.

Bw. Mbatia alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa kampeni za chama hicho jana, kwenye stendi kuu ya mabasi mjini Tarime, mkoani Mara.

Alitoa kauli hiyo akilinganisha matukio ya watu kupigwa mawe, mbwa kuvalishwa sare ya CCM, ambayo yamekuwa yakitokea na kudaiwa kufanywa ana vijana kwenye kampeni za uchaguzi mdogo zinazoendelea.

Bw. Mbatia, alikemea kitendo cha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa. Kuwatumia vijana wa vijiweni kuwarubuni kwa 'vijisenti' wafanye vurugu, badala ya kuwapa elimu ya uraia ili wajue haki zao.

Alisema, baada ya kuona vijana wapo vijiweni kutokana na kukosa kazi, wanasiasa hao wameamua kuwatumia kufanya maovu badala ya kuwaelimisha namna ya kujikwamua katika maisha yao.

Alisema, matukio ya fujo yanayotokea Tarime si aibu tu bali ni laana kwa Tanzania ulimwenguni kote kwa kuwa kila yanapotokea husambaa duniani kote.

Bw. Mbatia alisema, upinzani Tanzania haupaswi kuwa uadui wa kutukanana, kubebeana mapanga na kubebeana mawe bali kushindana kwa hoja.

Alisema, kwa vitendo vya fujo, vinavyotokea Tarime, vinaonesha jinsi ambavyo viongozi wa siasa hawajaelekeza somo la uraia la kila mwananchi kujua haki yake.

Bw. Mbatia alitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea wa chama hicho,
Bw. Enock Haroun anayewanaia Ubunge na Bw.Gidion Wangwe anayewania Udiwani Kata ya Tarime mjini.

(kutoka gazeti majira)