Siku ya tarehe 19/10/1983 (robo karne iliyopita!) ni siku muhimu kwangu. Siku hiyo nilikuwa mmoja wa wahitimu wa darasa la Saba waliofanya mtihani wa Taifa wa kumaliza Elimu ya Msingi ktk Shule ya Msingi Baranga, Musoma. 'LY' ni kifupi cha maneno 'Last Year' (wahitimu wa darasa la Saba wanajua sana hicho kifupi).
Mwalimu Mkuu wangu kipindi hicho nilipohitimu alikuwa ni mwalimu Amas Joseph, mwenyeji wa Singida.
Nakumbuka baada ya mitihani miwili ya asubuhi, tulipata chakula cha mchana shuleni (wali/ugali wa mahindi na nyama ya kondoo). Asubuhi tulifanya masomo mawili (Hisabati na Sayansi) na jioni tulimaliza mtihani wa Taifa kwa somo la Maarifa. Baada ya Mtihani, wanafunzi na baadhi ya walimu wetu tulipata nafasi ya kuagana rasmi kwa kucheza michezo mbalimbali. Mimi nilishiriki katika mpira wa volley (volleyball). Mwalimu wetu Mkuu alikuwepo na alicheza -alikuwa mtaalamu sana wa kucheza volleyball.
Kuna mambo mengi sana ya kukumbuka kipindi hicho (memories) shule ya msingi. Kwa mfano, nakumbuka sare (uniform) yetu ya kwanza kabisa ilikuwa shati ya khaki ya rangi ya kijani ikiwa na mifuko miwili kwa mbele yenye vifuniko na vishikizo, begani kulikuwa na kimkanda kama vile vya kijeshi na vimkanda hivyo (ktk mabega yote) viliwekewa kipande cha kitambaa cha njano (mfano wa nyota za wanajeshi) halafu kaptura ilikuwa ya khaki ya rangi nyeusi - Vijana Chipukizi!!! Vile vile huwa nacheka sana ninapokumbuka siku ya kujiandikisha shuleni (registration day). Siku hiyo nilienda peke yangu shuleni kujiandikisha (iko jirani na nyumbani kwetu). Sasa wakati wa kujiandikisha nilikuwa mtu wa mbali kidogo. Watoto walionitangulia walikuwa na majina yanayofanana sana. Utasikia wanataja; Chacha Marwa Mwita, Mwita Marwa Chacha, Mwita Chacha Marwa, Marwa Chacha n.k. Kabla ya zamu yangu kufika nikawa najiuliza hivi hii 'Chemistry' au 'permutation' ya 'elements za Chacha, Marwa na Mwita' ndio formula ya majina ya wanafunzi??
Kitu kingine ninachokumbuka enzi hizo ni wakati wa mitihani, mitihani ilikuwa inaandikwa ubaoni kwa chaki na mwalimu msimamizi alipokuwa anamaliza kuandika alimjulisha mwanafunzi mmoja au wawili nao walianza kuita kwa sauti (mfano) "la tano 'A'", wengine wanaitikia "la tano 'A'" hivyo hivyo mpaka wanafunzi wote wa darasa la V 'A' wanapata habari na kuingia ktk chumba cha mtihani!
Karibu kila asubuhi ulikuwa tunaenda na vitendea kazi mfano majembe, panga, fyekeo n.k. Mchana saa 9 baada ya masomo tunaenda shambani au msituni kukata miti (masanzu) ya kuzibia uzio -walikuwapo wakataji miti (wachache) na wengine wasombaji. Kuchomwa miiba miguuni ilikuwa kawaida! Wakati mwingine haikuwa rahisi kupata hizo nyenzo majumbani na waliokosa kupeleka nyenzo shuleni walipewa adhabu kali, mara nyigi viboko! Tulikuwa tunaagizwa vitu kila jioni vya kuleta asubuhi. Mara nyingi tuliagizwa nyasi za kuezekea. Tulipoanza darasa la kwanza tulitengeneza vijiti vingi vya kuhesabia na kuvitengenezea kaupinde na kamba. Vijiti hivyo viliwekewa vitundu vya kupitisha kamba nyembamba ambayo ilitumika kuvining'inizia vijiti. Kaupinde hako na vijiti vyake vilineokana na umbile mfano wa zeze!, tukawa tunatembea navyo kila mahali tulipokuwa shuleni! Vijiti hivyo vilitokana na mabaki ya mimea ya zao la mtama lilikwisha kuvunwa.
Wakati wa mitihani, kila tunaporudishiwa makaratasi ya mitihani mimi na marafiki zangu Marwa Richard Nyamonge, Juma Marwa Chororo, Naomi Matutu na Chacha Nyamonge tulikuwa na utaratibu wa kukutana na kujumlisha alama (maksi) za kila somo na kwa kila mmoja wetu na kuona nani amepata alama nyingi. Na kwa aliyepata alama nyingi ktk kikundi hiki cha rafiki zangu alikuwa na uhakika wa kuongoza darasa zima kimatokeo na kuwa wa kwanza!! Kwa hiyo hicho kikundi mara nyingi kilitoa mtu wa kwamnza hadi wa tano darasani. Matokeo yalipotengwa kimikondo, Chacha Nyamonge na Juma walichuana kivyao huku mimi, Marwa Richard na Naomi Matutu tukitoana jasho! Katika mtihani huo wa Taifa tulioufanya -ni Mimi na Naomi Matutu ndio tuliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza. Hata hivyo Marwa Richard, Juma Marwa na Chacha Nyamonge (na wengine wengi) walikuja kuchaguliwa na kuendelea na elimu ya Sekondari walipojaribu bahati yao kwa mara ya pili!
Kabla ya kuingia darasani kulikuwa na ukaguzi wa usafi -uniform, nywele, kucha, meno, kunawa miguu n.k. Kwa sasa vinaonekana ni vitu vya kawaida ila kwa kipindi hicho ilikuwa shida sana kwa watoto hasa kutokana na ukosefu wa maji na fedha za kununua sare mpya.
Baada ya matokeo ya darasa la Saba kutangazwa, tuliletewa shuleni vyeti cha kuhitimu Elimu ya Msingi. Cheti hicho cha kuhitimu Elimu ya Msingi ni muhimu sana katika historia yangu kielimu, maana huko ndiko nilikoanzia na msingi mzuri kielimu ndio mwanzo mzuri ktk safari ya kielimu na maisha kwa ujumla!
Walimu wangu: Darasa la I-VII (Baranga S/M):
Fanuel Namba (FN) -English (Mwl. Mkuu wa kwanza hadi 1980)
Makaranga Kubwela (MK) -Kiswahili
Nyafungo Kubwela (NK) -Sayansi Kimu (dada wa Makaranga, baadae mrs CW)
Amas Joseph (AJ) -English (Mwl Mkuu 1980-86)
Chacha 'Mbegete' Jasson (CJ) -Siasa, Michezo, Kiswahili
Chilemeji Wilson Mabuba (CW) -Kiswahili, Hisabati, English
Telesphory Paschal (TP) -English
Flora Matutu (FM); Mrs Amas Joseph -English
Leonidas Lwehumbiza (LL) -Sayansi
Robert Makuna (RM) -Jiografia
Obedi Mangunu (OM)-Kiswahili
Mwita Nyamhanga Obonyo (MN)-Sayansi Kimu, Jografia
Tui Nyamhanga Obonyo* (TN)-Kiswahili, Siasa
Mwita Magweiga Kisyeri (MM) -Hisabati
Daudi Sira 'Philipo Daniel' (DS) -English, Siasa
.......................................
Wanafunzi wenzagu (classmates) Darasa la I-VII:
1. Marwa Richard Nyamonge -mkondo B
2. Juma Marwa Chogoro -mkondo A
3. Naomi Matutu -mkondo B
4. Mbusiro Michael Kehengu-B
5. Rhobi Chacha Mosenye(?) -B
6. Chacha Nyamonge -Std VIA akahamia Sisimba S/M Mbeya
7. Severina Joram Nkenge -Std VIIA
8. Nyamahemba Washiki -B
9. Wesiko Marwa (monita std I-III) -B
10. Mwita Gati -B
11. Ogunya Mkama Ogunya -B
13. Bhoke Magabe -B
14. Mtatiro Marwa Tienyi -B
15. Bhoke Nyakorema -B
16. Rhobi Msoba -B
17. Chacha Nyamaranya -A
18. Nyawasha Machela -A
19. Elizabeth Wanda -A
20. Marwa Gati -A
21. Bhoke Sarya Mrisya -A
22. Charles Messanga -A
23. Mwita Magabe -A
24. Bhoke Magweiga Kisyeri -B
25. Nyamahemba Washiki-B
26. Chacha Mwita -A
27. Chacha Mwita -B
28. Mwita Mashauri -B
29. Chacha Mashauri -A
30. Mwita Marwa Kisyeri -B
31. Mwema Mnanka Samo -Std IVB akahamia Kongoto
32. Musoma Wanda* - Std VIIA
33. Wegesa Wambura Nyakubhilela* -A
34. Ghati Magweiga Kisyeri* -A
35. Scholastica William -B
36. Laurent John-B
37. Buhuru Samson -B
38. Ms Kichele Gati -A
39. Ms Kichele Magige Bwana -A
40. Bhoke Kiginga -A (Bibi Afya)
......................
*wameaga dunia
Monday, 20 October 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment