Sakata la EPA kwa ufupi
*Mwaka 1970 na 1980, Serikali ya Tanzania ilipokea huduma mbalimbali kutoka kampuni na taasisi za nje, lakini kushuka kwa thamani ya sarafu yake kulikochangiwa na vita ya Kagera kuliifanya Serikali ishindwe kulipa madeni hayo kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.
*Kati ya mwaka 1985 na 1995, Benki ya Dunia iliona haja ya kuisaidia Tanzania kulipa madeni hayo kupitia mikakati mbalimbali ukiwamo wa kuyanunua (Debt Buy Back).
*Mwaka 1985 Akaunti ya EPA ilihamishwa kutoka NBC kwenda BoT.
*Mwaka 1994, ili kuhakiki wadai halisi, Tanzania ilitangaza kwenye vyombo vya habari vya kimataifa wenye madai wajitokeze. Kampuni chache sana ziliitikia mwito huo.
Hivyo kwa sehemu kubwa, orodha muhimu ya madeni ikawa ikitumika ile iliyoandaliwa awali na NBC, ambayo wakaguzi wengi waliitilia shaka kuwa haikuwa sahihi kwa asilimia 100.
*Mwaka 1997, Serikali ilianza kutilia shaka uendeshaji wa EPA na kuiandikia barua BoT. Haikupewa hesabu hizo.
*Mwaka 2004, wakaguzi wa kimataifa wakiongozwa na kampuni ya M/S Lazard walitoa ripoti inayoonesha mwenendo wa akaunti ya EPA, wadeni waliolipwa, wasiolipwa na sababu zao na hali halisi ya madeni. Pia wakaishauri BoT isilipe sehemu kubwa ya deni lililokuwapo kwa sababu lina utata.
*Novemba 25, 2004, kampuni ya wakaguzi wengine wa kimataifa PriceWaterhouseCoopers ilithibitisha kuwa mapendekezo na yale yote yaliyobainishwa na ripoti ya Lazard na wenzake, pamoja na kasoro ndogo ndogo, yalikuwa sahihi.
*Julai, 2005, Gavana wa BoT, Dkt. Ballali aliijibu Serikali kuwa hawezi kutoa mchanganuo wa akaunti ya EPA kwa sababu ya ubovu wa mfumo wa kompyuta. Hakuwahi kutoa mchanganuo huo.
*Septemba, 2005 hadi Januari mwaka juzi, harakati nzito zilifanyika kwenye akaunti hiyo ambapo kampuni 22 za kitanzania zililipwa jumla ya sh. bilioni 133 zikidai ni mawakala wa kampuni za nje zinazoidai Serikali.
*Mwaka juzi, wakaguzi wa ndani wa BoT, kampuni ya Delloite & Touche, walibaini malipo yenye utata katika akaunti ya EPA kwenda kampuni ya Kagoda Agriculture.
*Septemba 8 na 9 mwaka juzi, Gavana wa BoT, Dkt. Ballali aliwaambia wakaguzi kuwa Serikali ndiyo inayojua yote kuhusu fedha zilizochotwa na Kagoda kutoka EPA.
*Septemba 15 mwaka juzi, Waziri wa Fedha, wakati huo, Bibi Zakia Meghji, alijibu wakaguzi kuwa Serikali inazitambua fedha hizo kuwa zilitumika katika 'matumizi mahsusi yenye maslahi kwa Taifa.' Alishindwa kutoa nyaraka kuthibitisha matumizi hayo.
Baadaye alikiri kuwa alidanganywa, hakupewa maelezo sahihi na maofisa wa BoT.
*Oktoba 28 mwaka juzi, Waziri Meghji alikiri mbele ya wakaguzi wa Deloitte & Touche, kuwa aliposaini barua ya kuidhinisha malipo kwenda Kagoda, aliegama zaidi katika maelezo tu ya Gavana Ballali kuwa ni malipo halali.
Alikiri katika mahojiano na wakaguzi kuwa baadaye alibaini kulikuwa na ubadhirifu kwenye akaunti ya EPA.
*Mwaka jana, wakaguzi wa Ernst & Young nao walisema baada ya mahojiano marefu na Waziri Meghji, hakuna ushahidi kuwa Serikali iliagiza malipo kutoka kwenye akaunti ya EPA.
*Januari mwaka huu, Ikulu ilitoa kwa ufupi kilichobainika kwenye ripoti ya Ernst & Young na kuanza hatua alizozichukua Rais Kikwete za kuunda Kamati Maalumu kuangalia hatua zaidi za kuchukuliwa dhidi ya waliohusika. Ikapewa miezi sita.
*Januari 10 mwaka huu, Rais Kikwete alitangaza kumfuta kazi Dkt. Ballali na nafasi yake kuchukuliwa na Profesa Ndulu.
*Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri na kumwondoa Bibi Meghji na nafasi yake kuchukuliwa na Bw. Mustapha Mkulo.
*Agosti, Rais Kikwete alihutubia Bunge na kulizungumzia kwa kirefu suala la EPA ambapo alitoa hadi Oktoba 30 mwaka huu, waliohusika wawe wamerejesha fedha hizo. Rais Pia aliagiza ifikapo Novemba mosi, wote watakaokuwa wameshindwa kutekeleza agizo hilo, wafikishwe kortini. (kutoka: gazeti 'Majira' 23/10/2008)
Thursday, 23 October 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment