Thursday, 2 October 2008

Mwita Mwikwabe, Katibu UVCCM Tanga

.................................................
"Narudia kusema mimi ni Mkurya, nikiwa chuo kikuu nikawa Rais wa DARUSO kamwe sikuwahi kurudi nyuma au kusema uongo kwa kile ninachoamini, Nyerere alisema uongo si nidhamu, lazima tuseme ukweli,"
.................................................
"Mimi ni muumini mkubwa wa Baba wa Taifa kwa vitabu na hotuba zake, nazifuatilia kweli...sasa chama ndicho kinapoteza imani kwa wanyonge na wafanyakazi na kinabaki mikononi mwa mafisadi, ipo siku nasi wanyonge tutachukia...ukiwa mkweli leo unasulubiwa"
..................................................

Katibu UVCCM Tanga abwaga manyanga
*Adai hawezi kwenda kumpikia Nchimbi chai

KATIBU wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Tanga, Bw. Mwita Mwikwabe, ametangaza kuacha kazi ndani ya Jumuia hiyo kwa alichodai ni kukerwa na kuonewa kunakosababishwa na kusema ukweli dhidi ya ufisadi.

Bw. Mwikwabe ambaye ni miongoni mwa wana CCM watano walioomba kuteuliwa na CCM katika kura za maoni za kumtafuta mgombea ubunge wa Tarime, alitangaza uamuzi huo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa.

Aliwaambia waandishi hao kuwa amekuwa na ugomvi mkubwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Bw. Emmanuel Nchimbi, kuhusu msimamo wake juu ya kutounga mkono vitendo vya ufisadi kwa Watanzania.

Bw. Mwikwabe alidai baada ya kumaliza elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliajiriwa kuwa Katibu wa UVCCM na baadaye Sekriterieti ya Chama ilimpendekeza kuwa Katibu wa Jumuia hiyo mkoa huo lakini Bw. Nchimbi alipinga na kumpeleka Tanga na Dar es Salaam kupangiwa mtu anayetoka naye mkoa mmoja.

Hata hivyo, alidai kuwa alikubali kufanya kazi mkoa wa Tanga kwa muda wote hadi sasa, kabla ya juzi kuomba likizo ili kuomba ridhaa ya wana CCM wa Tarime kumpigia kura za maoni awatumikie kama mbunge baada ya kumsomesha.

Alidai kuwa katika kura hizo alipata nafasi ya tatu na kumuunga mkono mwana CCM aliyepitishwa na vikao vya chama, na baada ya kuombwa alimfanyia kampeni na akiwa katika kijiji kimoja alipigiwa simu akijulisha kuwa amepewa uhamisho kwenda makao makuu kuwa Katibu Msaidizi wa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya hiyo.

Aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa taarfa hiyo, aliwaambia hajakubaliana na uamuzi huo na kuwaeleza kuwa huo ndio mwisho wake kutumikia UVCCM na kwamba hataripoti akiwa hai labda upelekwe mwili wake.

Bw. Mwikwabe alidai kuwa alitambua kuwa uamuzi huo ulichukuliwa baada ya yeye kukataa kubadili uamuzi wa vikao vya Jumuia hiyo mkoani Tanga iliyotoa muda hadi Mei 4 mwaka huu watu wanaotajwa kwa ufisadi wajiuzulu nyadhifa zao na baada ya hapo, wafikishwe mahakamani mara moja.

“Kikao cha Vijana Tanga ndicho kilichopitia azimio hilo si mimi mwenyewe, lakini nilipigiwa simu kutakiwa eti nikanushe na niseme haukuwa uamuzi wa vijana ... mimi nilipinga hatua hiyo, kwa vile lengo ni kusadia Chama na Serikali kwa umma wa Watanzania kuondoa watu wanaokichafua,” alidai.

Alidai kuwa baada ya kusimamia uamuzi huo, alizidi kutishiwa na wakati mwana UVCCM mwingine, Bw. Nape Nnauye akizungumzia mkataba wa ujenzi wa kitega uchumi wa UVCCM makao makuu, alimuunga mkono kutokana na ukweli kuwa mkataba huo haukuwahi kujadiliwa na kupitishwa kama ilivyodaiwa.

Kutokana na msimamo huo, wenyeviti wa mikoa waliitwa Dodoma, awali wakimuunga mkono Nape, lakini baada ya kikao cha siri walisalia wenyeviti watatu tu waliomuunga mkono hadi ulipofikia uamuzi wa kumsimamisha kwa kusema ukweli.

Bw. Mwikwabe alidai kuwa kutokana na kuwa miongoni mwa vijana wanaochukizwa na ufisadi, ndiyo maana viongozi hao wamechukua uamuzi wa kumhamisha na kumpeleka makao makuu ya vijana kwa nafasi hiyo, ambayo alisema ndio mwisho wa kutumikia UVCCM kwa madai kuwa haitaki mtu msemakweli.

“We fikiria, wananipeleka kuwa msaidizi wa Nchimbi ambaye tayari hatuelewani ili ikitoka pale siri nifukuzwe...nina elimu yangu ya chuo kikuu, unanipeleka 'desk' niwe mhudumu wa chai wa Nchimbi sitaweza kamwe, chama kikinihitaji sawa, la sivyo nakwenda kufanya kazi yangu ya taaluma, nilijitoa kutumikia chama kwa moyo wangu wote, lakini nimeshindwa na nguvu ya pesa,” alidai Bw. Mwikwabe kwa uchungu.

“Mimi ni muumini mkubwa wa Baba wa Taifa kwa vitabu na hotuba zake, nazifuatilia kweli...sasa chama ndicho kinapoteza imani kwa wanyonge na wafanyakazi na kinabaki mikononi mwa mafisadi, ipo siku nasi wanyonge tutachukia...ukiwa mkweli leo unasulubiwa,” alisema.

“Narudia kusema mimi ni Mkurya, nikiwa chuo kikuu nikawa Rais wa DARUSO kamwe sikuwahi kurudi nyuma au kusema uongo kwa kile ninachoamini, Nyerere alisema uongo si nidhamu, lazima tuseme ukweli,” alisema.

(source: majira, Na George John, Tarime
::Habari za Tanzania Alhamis Okt 02, 2008
Imetolewa mara ya mwisho: 02.10.2008 04:30 EAT)

No comments: