Binti aliyefyekwa na mkwewe mashavu, masikio apasuliwa
MKAZI wa kijiji cha Rosoti wilayani Tarime mkoani Mara, Robi Matiko (15), amefanyiwa upasuaji wa kubandika ngozi kwenye mashavu baada ya kukatwa mapanga.
Robi inadaiwa alikatwa mashavu na mkwewe, Bw. Mwita Thomas, Machi 24 mwaka huu, baada ya kutokea ugomvi kati yake na baba yake mzazi.
Akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita katika hospitali ya rufaa ya Bugando (BMC)
jijini hapa ambako amelazwa akitibiwa majeraha hayo, Robi alidai kuwa chanzo cha ugomvi huo ni kutoroka kwa mumewe, Thomas Mwita (19).
Alidai kulazimika kutoroka nyumbani kwa mumewe huyo ili arejee shuleni kuendelea na masomo, kwani alilazimishwa kuolewa akiwa mwanafunzi wa
shule ya msingi Turwa wilayani humo.
Robi alidai kuwa mzazi wake, Bw. Daud Matiko, alipokea mahari ya sh. 350,000 kutoka kwa Bw. Thomas na kumlazimisha kuolewa akiwa darasa la tatu.
Alidai kuwa kutokana na kitendo cha baba yake mzazi kumlazimisha kuolewa, kilimfanya atoroke ukweni na kwenda kwa mama yake mdogo ambako alifuatwa na kujereshwa ukweni, lakini akatorokea kwa mjomba wake.
“Kitendo hiki cha mimi kutoroka mara mbili nikiwa ukweni, kilimfanya baba mkwe kuudhika na kwenda kudai mahari yake kwa baba yangu ambaye hakuwa tayari kufanya hivyo.
"Kuona hivyo alipomwamuru mkwe wangu afanye awezalo dhidi yangu ili kunidhibiti nisitoke tena nyumbani kwa mume wangu,” alidai Robi.
Aliendelea kudai kuwa kutokana na amri hiyo, mkwewe alichukua panga na kumkata masikio na mashavu kama adhabu ili asirudie kutoroka.
Aliongeza kuwa baada ya kukatwa viungo hivyo na kutupwa chini mbwa aliyekuwa nyumbani hapo aliamrishwa kuvila na alifanya hivyo.
“Mipango ya kuolewa kwangu ilianzia katika vilabu vya pombe, kwani ndiko baba na mkwe walikutana na kupanga namna ya mimi kuolewa na Thomas ambaye ni mtoto wa Mzee Mwita,” alisema msichana huyo kwa masikitiko zaidi.
Mpaka sasa hali ya Robi inaendelea vizuri, kwani tayari baadhi ya majeraha yameanza kupona na anaendelea na matibabu Bugando
Tuesday, 28 October 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment