Monday, 27 October 2008

Nyumba Ndogo: kuna nini?

Hizi nyumba ndogo ambazo zinachipuka kila kukicha kama uyoga, bado zinatikisa familia mbalimbali huku zingine zikisambaratika na zingine zikiashiria mipasuko mikubwa.

Kiini cha tatizo hilo bado ni kitendawili huku baba na mama wakirushiana mpira kukataa kuhusika. (SOURCE: Nipashe 26/10/2008)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Baba anavyosababisha nyufa ndani ya nyumba

2008-10-26 13:48:35
Na Anti Flora Wingia


Hizi nyumba ndogo ambazo zinachipuka kila kukicha kama uyoga, bado zinatikisa familia mbalimbali huku zingine zikisambaratika na zingine zikiashiria mipasuko mikubwa.

Kiini cha tatizo hilo bado ni kitendawili huku baba na mama wakirushiana mpira kukataa kuhusika.

Hebu mpenzi msomaji wangu kabla sijachambua mengi nikumegee kisa kimoja cha kusimuliwa hivi majuzi nikiwa nimealikwa na jamaa yangu mmoja kupata soda.

Tukiwa sehemu fulani huku tukiburudika na vinywaji baridi, jamaa yangu huyo alipigiwa simu na rafiki yake wanayefanya kazi pamoja.

Jamaa huyu katika mazungumzo yake, akawa anamuuliza rafiki yake huyo kuwa yuko wapi, ambapo alimjibu yuko kwao kijijini huko mikoani.

Na kwamba aliitwa kwenye usuluhishi wa mgogoro wa kifamilia kati yake na mkewe ambaye alikwenda kumshitaki kwa kumtelekeza baada ya kuhamia kwa mke mdogo.

Alipomaliza simu, jamaa yangu huyu akaanza kunisimulia kisanga kilichompata rafiki yake.

Akasema swahiba huyo alitokea kumpenda mama mmoja ambaye alikuwa tayari ameshazaa mtoto mmoja na mwanaume mwingine.

Hata pale alipokatazwa na ndugu zake kwamba asijikite kwa mwanamke huyo bali atafute mwingine wa kuoa, hakusikia la mtu.

Matokeo yake akafunga naye ndoa ya nguvu. Akabahatika kuzaa naye mtoto mmoja.

Katika pitapita zake kibiashara, akakutana na bibie mmoja, mrembo toka mkoa wa Kusini mwa Tanzania.

Kila akimuwaza, anajutia kwanini alioa mwanamke wa kwanza, pengine angesubiri angebahatika kumpata huyu anayemzingua.

Hakujivunga, akatupa karata yake ikapokelewa. Wakashikamana kimapenzi akazaa naye mtoto mmoja.

Mahusiano yalinoga na miaka mitatu baadaye akazaa naye mtoto wa pili. Kwa bi-mkubwa mawasiliano yakaanza kukata taratibu na hatimaye jamaa akahama kabisa nyumbani na kujitosa kwa bi-mdogo.

Bi-mkubwa kuona vile akafungasha virago na kwenda kijijini kushtaki kwa wazee kuhusu nyendo za mumewe.

Naye bi-mdogo katika hali ya kushangaza, akamtishia bwana huyu kwamba akithubutu kumwacha tu, naye ajue amepoteza uhai. Yaani akaapa kumuua bwana huyu endapo atamwacha kwa kisingizio cha nyumba kubwa.

Mpenzi msomaji, ama kwa hakika Maisha Ndivyo Yalivyo. Hizi ni nyumba mbili zilizojengwa na mume mmoja ambazo sasa ziko katika mtikisiko mkubwa.

Bi-mkubwa yuko kijijini kushtakia wazee juu ya nyendo za mumewe ambaye amemtelekeza na mtoto na kuhamia kwa mke mwingine. Na bi-mdogo naye anamng?ang?ania mume kwamba akimwacha tu, basi atamtoa uhai.

Nyumba hizi mbili zimekumbwa na nyufa zilizosababishwa na baba anayezimiliki. Hapa hakuna wa kumlaumu.

Kama baba huyu angetulia na mkewe mkubwa, hata tishio hilo la kifo pengine lisingekuwepo. Au siyo msomaji wangu?

Ah! Sijui bwana. Lakini bwana yule anapaswa kuwa makini kwani mke aliyemtishia kumuua endapo atamuacha anatoka kabila moja ambalo halina masihara.

Mtu wa kabila hilo akipania kuua hazuiwi kwani hata yeye mwenyewe yuko radhi kujiua baada ya kutimiza azma yake. Upo hapo?

Hakika, baba huyu mwenye nyumba mbili kwa sasa yuko njia panda. Hajui aamue lipi. Lakini yote hayo yafaa ajilaumu mwenyewe. Atachagua weee hadi ataishia kunyakua koroma.

Yafaa atambue kuwa kila siku anazaliwa mtu mpya na mzuri pengine kuliko yule wa jana. Akiendeleza tabia hiyo ya kupepesa kope huku na huko, atajikuta amelundika migogoro ya kifamilia katika kila nyumba atakayoijenga.

Habari ndio hiyo.
Msomaji wangu, kwa leo nikomee hapa nikupe fursa nawe uchangie maoni. Ukiwa tayari nikandamizie kupitia barua pepe;
flora.wingia@guardian.co.tz
Wasalaam

SOURCE: Nipashe