Tuesday, 28 October 2008

EPA: A-Z (2)

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ernst and Young, wizi ulibainika katika EPA kwa mwaka 2005/06 ulikuwa katika mafungu mawili.

Fungu la kwanza, lilihusu wizi wa Sh. bilioni 90, ambazo mkaguzi huyo alipata ushahidi unaothibitisha kuwa fedha hizo ziliibwa waziwazi na kupendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliohusika wa wizi huo.

Fungu la pili, lilihusu kiasi cha sh. bilioni 42 ambazo mkaguzi huyo alishindwa kupata ushahidi wa kuthitibithisha wizi wake na hivyo kupendekeza uchunguzi ufanyike kwa kina.

Agosti 21, mwaka huu, akilihutubia Bunge, Rais Kikwete alisema hadi wakati huo, watu waliochota fedha kwenye EPA, walikuwa wamerejesha zaidi ya Sh. bilioni 60 na akawapa muda hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu wawe wamerejesha fedha hizo, vinginevyo watafikishwa mahakamani kuanzia Novemba mosi.
Vilevile, Rais Kikwete alisema fedha zinazorejeshwa, ambazo zinahifadhiwa katika akaunti maalum, zitaingizwa kwenye mfuko wa kilimo kwa ajili ya kuwakopesha wakulima.
(SOURCE: Nipashe, 28/10/2008)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Njama za kuokoa mafisadi EPA dhidi ya jinai zabainika

2008-10-28 16:31:30
Na Muhibu Said

Zikiwa zimesalia siku tatu kuisha muda uliowekwa na serikali kwa mafisadi waliochota Sh. bilioni 133 kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kurejesha fedha hizo, njama za kuwaepusha watu hao na kesi ya jinai, zimegundulika.

Njama hizo zimegundulika baada ya Timu ya Rais inayochunguza suala hilo, kueleza bayana kwamba, watakaoshindwa kurejesha fedha hizo katika muda waliopewa na serikali, watafunguliwa kesi ya madai mahakamani.

Akizungumza na Nipashe, jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngole, alisema kazi inayofanywa na timu hiyo hivi sasa ni kukusanya fedha kutoka kwa watu hao na kwamba, watakaoshindwa kurejesha ndani ya muda uliowekwa, timu itawapeleka mahakamani kuomba mahakama isaidie fedha hizo zirejeshwe.

Ngole, ambaye pia ni Msemaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alieleza hayo, alipotakiwa na Nipashe aeleze hatua iliyofikiwa na timu hiyo katika kushughulikia suala hilo katika muda uliosalia wa kurejesha fedha hizo.

``Hivi sasa kuna kazi mbili zinafanywa na timu. Kutekeleza maelekezo ya Rais ya kukusanya fedha ili ikifika Oktoba 31 fedha zote ziwe zimerejeshwa, na pia wasiorejesha timu iwapeleke mahakamani, ikaiombe mahakama isaidie fedha hizo zirejeshwe,`` alisema Ngole.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Ernst and Young, wizi ulibainika katika EPA kwa mwaka 2005/06 ulikuwa katika mafungu mawili.

Fungu la kwanza, lilihusu wizi wa Sh. bilioni 90, ambazo mkaguzi huyo alipata ushahidi unaothibitisha kuwa fedha hizo ziliibwa waziwazi na kupendekeza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya waliohusika wa wizi huo.

Fungu la pili, lilihusu kiasi cha sh. bilioni 42 ambazo mkaguzi huyo alishindwa kupata ushahidi wa kuthitibithisha wizi wake na hivyo kupendekeza uchunguzi ufanyike kwa kina.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, anayeongoza timu hiyo, alimuomba Rais Kikwete kwamba hadi kufikia mwisho wa muda uliowekwa na serikali wawe wamekusanya asilimia 73 ya fedha zilizoibwa kwenye EPA.

Rais Kikwete aliitaka timu hiyo iwe imekusanya kutoka kwa watu hao Sh. bilioni 64.8 kufikia muda wa mwisho, timu hiyo iliyoomba kuongezewa na kukubaliwa na serikali.

Hata hivyo, umezuka utata, baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo Jumatano wiki iliyopita, kukaririwa na televisheni ya TBC1 akisema kwamba, hadi kufikia siku hiyo, zilikuwa zimekusanywa kutoka kwa watu hao Sh. bilioni 68. Kiasi ambacho ni kikubwa kuliko kile ambacho timu ya Mwanyika iliomba.

Katika sakata hilo, vyanzo huru ndani na nje ya serikali vinasema kwamba wale ambao wamerejesha fedha za EPA kwa timu hawatashitakiwa kwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya kutokushitakiwa kama wangerejesha fedha hizo.

``Kulikuwa na makubaliano ya kiuungwana kwamba warejeshe fedha, ili wasishitakiwe, hivyo ni dhahiri kuwa hawatashitakiwa (wale waliorejesha fedha),`` kilisema chanzo kimojawapo.

Chanzo kingine kilisema ingawa hakuna makubaliano ya maandishi, lakini mwenendo wa mambo yanavyokwenda inaonyesha kuwa waliorejesha hawatapelekwa kortini.

``Hawakuandikiana na timu, lakini kuna makubaliano ya kiungwana,`` kilisema chanzo hicho.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema haiwezekani wezi wakashtakiwa kwa kesi ya madai na kuongeza kuwa wanapaswa washtakiwe kwa kesi ya jinai.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Slaa, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alisema kama watu hao hawatapelekwa mahakamani kwa kesi ya jinai, itakuwa ni uvunjaji mkubwa wa sheria za nchi.

``Kwa mfano kampuni ya Kagoda imegushi nyaraka zote, Hata ripoti ya Ernst and Young imesema nyaraka zao ni za kughushi. Kwa nini wasipelekwe mahakamani kwa kughushi?,`` alihoji Dk. Slaa.

Wakati Dk Slaa akisema hayo, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Juvenalis Ngowi, aliiambia Nipashe jana kwamba endapo Timu ya Mwanyika itawapeleka watuhumiwa wa EPA kwa kesi ya madai basi ni uthibitisho kuwa fedha zilizoibwa ni za serikali na si za wafanyabiashara kama inavyosemwa.

``Huwezi kuwafunguliwa kesi ya madai kama wewe si mwenye fedha hizo, serikali inaweza kufungua kesi ya jinai tu na si ya madai. Wakifungua kesi ya madai tutajua fika fedha hizo ni za serikali,`` alisema Ngowi.

Agosti 18, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alipokea rasmi ripoti ya uchunguzi wa upotevu wa fedha hizo, aliyokabidhiwa na Mwenyekiti wa Timu hiyo, Mwanyika.

Wengine, wanaounda timu hiyo, ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.

Agosti 21, mwaka huu, akilihutubia Bunge, Rais Kikwete alisema hadi wakati huo, watu waliochota fedha kwenye EPA, walikuwa wamerejesha zaidi ya Sh. bilioni 60 na akawapa muda hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu wawe wamerejesha fedha hizo, vinginevyo watafikishwa mahakamani kuanzia Novemba mosi.

Vilevile, Rais Kikwete alisema fedha zinazorejeshwa, ambazo zinahifadhiwa katika akaunti maalum, zitaingizwa kwenye mfuko wa kilimo kwa ajili ya kuwakopesha wakulima.

SOURCE: Nipashe, 28/10/2008