Madeni ya vyama vya ushirika tutayabeba - JK
01 Sep 2007By Dunstan Bahai
Serikali imeamua kuchukua madeni yote ya vyama vya ushirika yaliyokuwa yakidaiwa na mabenki na kuyalipa ikiwa ni hatua ya kuvifufua vyama hivyo.
Hatua hiyo ni pamoja na kuviongezea uwezo wa kuwahudumia wakulima vyama hivyo. Rais Jakaya Kikwete aliyasema hayo wakati akiwahutubia Watanzania katika utaratibu aliojiwekea wa kila mwisho wa mwezi kulihutubia taifa kwa kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayowahusu Watanzania.
Alisema, kwa lengo la kuviondolea vyama vya ushirika mzigo wa madeni ili viweze kujipanga upya kibiashara, mwaka jana serikali ilifuta madeni hayo yaliyokuwa yanadaiwa na serikali na taasisi zake. Rais alisema, kupitia azimio la Bunge namba 4/2006, madeni ya nyuma ya vyama hivyo yenye thamani ya Sh. 15,013,073,960 hadi kufikia Desemba, 2004 yalikuwa yamefutwa. `Aidha kwa nia ya kutaka kuzidi kuviwezesha vyama vya ushirika kukopesheka, serikali iliamua kubeba madeni ya vyama hivyo yaliyokuwa yanadaiwa na mabenki na wakulima.
Kwa ajili hiyo, deni la Sh. 3,807,087,503 la mabenki na la Sh. 2,359,783,423 la wakulima yatalipwa na serikali,` alisema Rais. Alisema ili kufanikisha azma hiyo ya serikali, raslimali fedha takribani Sh. bilioni 2.6 zitatumika na kwamba serikali ilianza kazi hiyo mwaka jana kwa kutenga Sh. milioni 370 katika bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ajili ya kazi hiyo iliyoanza Aprili hadi Juni mwaka huu na kwamba katika bajeti ya mwaka huu zimetengwa Sh. biliobi 1.9 na kiasi kilichobaki cha Sh. milioni 280 kitapatikana katika bajeti ijayo. Hata hivyo, alisema usimamizi dhaifu wa mfumo wa soko huria, uongozi mbovu usiowajibika ipasavyo kwa wanachama na usiokuwa adilifu, ndivyo vilivyodhoofisha ushirika nchini.
Rais Kikwete alisema miongoni mwa mazao yaliyoathiriwa sana na matatizo ya ushirika ni korosho na pamba. Kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi, Rais alisema mwaka jana aliagiza kufanyika kwa uchunguzi na uchambuzi wa kina kuhusu malalamiko ya wananchi juu ya ugawaji na miliki ya viwanja, mashamba na ardhi.
Alisema aliagiza kuundwa kwa kamati maalum zikiwa chini ya uongozi wa wenyeviti wa Halmashauri husika kufanya kazi hiyo na wajumbe wake wawepo pia polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa.
`Nafurahi kwamba kamati hizo zilifanya kazi yake vizuri na zoezi hilo limefanyika kwa muda muafaka.
Malalamiko 13,915 yalipokelewa kote nchini na kushughulikiwa kama nilivyoagiza Malalamiko 9,740 yamepatiwa ufumbuzi mpaka Juni 30, 2007,` alisema Rais.
Rais alisema hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwahamisha maofisa 43 walioonekana kukaa muda mrefu kituo kimoja cha kazi na watumishi wanne waliobainika kuhusika kama sehemu ya migogoro hiyo walifukuzwa kazi na wengine kesi zao zinaendelea.
* SOURCE: Nipashe
Saturday, 1 September 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment