Monday, 17 September 2007

Rushwa ya ngono inaweza kuisha ikiwa...

Nimeipenda sana hii makala. Sijui kina dada wangapi wataisoma au kuipenda ...!
By Mosonga.

Rushwa ya ngono ndani ya vyumba vya habari inaweza kuisha ikiwa...

16 Sep 2007
By Anti Flora Wingia

Taaluma ya Uandishi wa habari ni moja ya nyenzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote lile. Waandishi ndani ya taaluma hii jukumu lao kubwa ni kukusanya habari, kuziandika kwa usahihi na ukweli, kisha kuzisambaza kupitia vyombo vya habari iwe ni redio, magazeti na televisheni na kadhalika ili umma ufahamu kinachoendelea.

Habari hizo zaweza kuwa za kisiasa, kiuchumi, kijamii ambazo kwa ujumla wake zinahusu maendeleo ya nchi na watu wake.Lipo tatizo moja ambalo serikali imeamua kulivalia njuga kutokana athari zake katika maendeleo ya taifa letu.
Hili ni tatizo la rushwa katika siasa.

Waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele kuandika habari zinazohusu wanaobambwa na rushwa ya aina hii, japokuwa kwa uchache wamenaswa baadhi ya vigogo lakini wengi ni wale samaki wadogo.

Lakini tatizo hili ni kifo cha wengi kwani hata ndani ya vyombo vya habari kwenyewe, tatizo la rushwa lipo kupitia vijibahasha vilivyosheheni `mishiko`.

Hili na hata waandishi kwenye vyombo vya habari vya IPP na Mwananchi Communication wamekiri wakati walipokutana kwenye warsha ya siku moja Jijini Dar es Salaam Alhamisi wiki hii.

Mpenzi msomaji, niruhusu nizungumzie rushwa ya ngono inayowanyima raha waandishi chipukizi wa kike katika vyumba vyetu vya habari.

Jambo hili katika warsha ile lilitolewa maoni na baadhi ya washiriki ambapo wapo waliosema mabinti wenyewe ndio wanaojisogeza kwa waandishi au wahariri wa kiume ili kubembeleza habari aliyoandika itoke.

Wengine wakasema waandishi au wahariri wanaume ndio wanaowalazimisha mahusiano ili kuwachapishia habari waziandikazo. Rushwa hii kwa kiasi kikubwa imewatia woga waandishi chipukizi wa kike wanaotaka kujiunga na taaluma hiyo.

Katika warsha hiyo ambayo pia nilikuwa mzungumzaji, niliwaambia waandishi wenzangu kwamba tatizo hilo la rushwa ya ngono lipo na mabinti wengi wamejikuta ama wanasuasua kumudu uandishi wa habari au hawajiamini kutokana na mazoea ya kuandikiwa habari zao na wahariri wa habari au waandishi waandamizi ambao huwapa masharti ya mahusiano kimapenzi.

Lakini kusema ukweli mabinti hawa wanaweza kukataa hali hiyo na hakika inawezekana kabisa. Labda nieleze uzoefu wangu kuthibitisha hilo.

Niingia chumba cha habari mwaka 1978 nikiitwa mwandishi mwanafunzi.

Nikajifunzia uandishi pale pale huku tukiwa wasichana wawili tu wanafunzi, na kinamama wawili watu wazima(sub-editors).

Wengine katika chumba kile cha habari walikuwa wanaume watupu. Walikuwa watundu sana.

Wengine hivi sasa ni wanasheria, mahakimu, wahadhiri na kadhalika.

Wakawa wanatunyanyasa kwa kejeli kwamba wanawake hawafai kuwa waandishi, eti ile ni kazi ya wanaume. Sisi tukakomaa.

Tukaziba masikio. Yupo mhariri wa habari mmoja alitafuta njia mbalimbali kunitega, akashindwa. Matokeo yake kama kunikomoa akawa ananipangia kazi ngumu lakini zote niliweza.

Siku moja akanikataza kwenda kula mchana wakati tayari amenipanga late duty (kutoka wa mwisho ofisini). Nikakaidi nikaenda zangu kula.

Ilikuwa Jumapili. Jumatatu niliporipoti ofisini, wenzangu wote wakapangiwa kazi mimi nikaachwa. Jumanne na Jumatano vivyo hivyo. Nikaona ujinga.

Nikaanza kulia. Msanifu Mkuu Mzalendo akanikuta nalia akaniuliza kulikoni, nikamweleza.

Akaondoka kumbe alienda kumjulisha Mhariri Mtendaji(Bosi wa Shirika). Huyu akaniita nikamweleza kilichotokea.

Akaniambia kesho yake nikatafute habari yoyote mitaani kisha niiandike, nitoe nakala nimpelekee. Nakala halisi ya habari ile nimpatie mhariri yule wa habari anayeninyanyasa.

Ilikuwa ni Ijumaa na nilipotizama gazeti nikaona habari ile imechapishwa.

Tokea siku ile alikoma kabisa kunisumbua. Hadi naondoka katika chombo kile cha habari sikulegeza uzi ule.

Kwa hiyo, kupiga vita rushwa ya ngono katika vyumba vya habari inawezekana ikiwa mabinti watakuwa ngangari, wakatae na kama wanazidi kusumbuliwa watoe ripoti ngazi za juu ili wale wanaowasumbua wadhibitiwe.

Mpenzi msomaji, taaluma hii ya uandishi wa habari pia inahitaji uwiano wa kijinsia. Hawa ndio watakuwa mawaziri wa habari huko waendako.

Siyo kila mahali ni mfumo dume tu umejikita kwa kisingizio kwamba eti wanawake hawawezi. La hasha, wakipewa nafasi wanaweza sana na pengine kuliko hata wanaume.

Wahariri wanaume na hata waandishi waandamizi wanatakiwa kuwasaidia waandishi chipukizi wa kike bila masharti.

Wakumbuke kwamba hata wao walianzia katika ngazi za chini hadi kufikia hapo walipo. Waache tamaa hizi za fisi wanazofikiri wanaonyesha urijali kumbe wanaangamizana.

Baadhi yao wanao wake zao majumbani na mabinti wengine wanao waume zao au wachumba zao. Sasa michezo hii ya kuigiza wanayofanya wanadhani wanamfurahisha nani kama siyo kugawiana masikitiko?

Tatizo hili linahitaji mjadala mpana kujaribu kutafuta njia sahihi na za kudumu za kulitokomeza kabisa. Baadhi ya wasichana wanadai hali ngumu ya uchumi ndiyo inayowafanya wajirahisi. Lakini niwaulize, wakijirahisi uchumi huo utadumu kwa muda gani?

Wakumbuke kuwa uvumilivu hula mbivu. Wengine tulivumilia ndio maana tupo hapa tulipo. Unafikia mahali mtu anakurubuni nawe unamjibu... hata mimi ninazo. Naweza kujikimu mwenyewe kwa kazi yangu.

Hiyo ndiyo jeuri ambayo wanawake katika taaluma hii wanapaswa kuiweka mbele. Tunachotaka ni kinababa hawa watizame chini au wafikirie mara mbili mbili nitumie gia gani kumpata fulani.

Tukatae rushwa hizi ambazo badala ya kudhani zitakuinua kiuchumi kumbe zinakudidimiza na kukuchelewesha kule uendako.

Utashi na dhamira yako mwandishi wa kike ilenge kujitegemea wewe mwenyewe na siyo kuwa tegemezi. Ukiendekeza utegemezi, basi uelewe kuwa rushwa hizi za kujitakia zitakuzunguka maisha yako yote.

Jiamini na ujitume mwenyewe, hakika, utaweza. Usikubali njia za mkato. Kumbuka kila mwenye mafanikio amepitia vikwazo vingi ambavyo hatimaye alivishinda. Na hiyo ni kutokana na kutokata tamaa. Maisha Ndivyo Yalivyo.
Wasalaam
Email: fwingia@yahoo.com

* SOURCE: Nipashe

No comments: