Tuesday, 9 October 2007

Shugamami anapo-'opoa' mume kijana!

Shugamami kauza nyumba, katimua watoto kisa, kaopoa mume kijana!
07 Oct 2007
By Anti Flora Wingia

Karibu wiki mbili zilizopita, safu hii ilijadili na kuchapisha maoni ya wasomaji wetu mbalimbali kuhusu suala la rushwa ya ngono katika vyumba vya habari.

Wengi wamekemea tabia hiyo ambayo hakika si tu haipendezi, bali pia inafifisha taaluma yenyewe na pia juhudi za taifa za kupambana na rushwa ikiwemo ya aina hiyo.

Hebu leo tuchepuke kidogo, tuangalie suala lingine ambalo kwa kiwango kikubwa limechangia mizozo na migongano ndani ya familia zetu.

Tunaweza kuona ni jambo la kawaida kutokana na kutokea hapa na pale na kukaa kimya, lakini athari zake ni kubwa katika maisha yetu ya kila siku.

Naam. Mpenzi msomaji, bila shaka umewahi kusikia watu wanaojulikana kama MASHUGADADI. Hawa ni wanaume watu wazima, wengine wenye heshima na nyadhifa zao wanaotamani mabinti wadogo na kuwarubuni kimapenzi.

Hawa siyo mabachela tu bali baadhi yao wameoa na hata kubahatika wajukuu. Mabinti wanaoshikamana na mijibaba ya aina hii, hutamba eti ni mashuga-dadi wao.

Hali hiyo ipo pia kwa kinamama kwani wapo baadhi hujisheua na kuwatia ulimboni vijana wadogo wa kiume, wengine wakiwa na umri sawa na watoto wao na hata kufikia hatua kuwaweka kinyumba. Hawa wamekuwa wakijulikana kama MASHAGAMAMI.

Kinamama wa aina hii ndio nitakaozungumzia leo nikihusisha mfano hai niliounasa hivi majuzi toka kwa jirani yangu.
Wapo mashugamami wanajenga mahusiano na vijana wadogo lakini kila mmoja akiwa kwake.

Yaani kuwa na mawasiliano kisha kuonana mara kwa mara. Katika kundi hili hata wanafunzi wao. Lakini wengine wakinogewa, kama wako single, basi hugandamana moja kwa moja na kuwa mke na mume.

Kabla sijaendelea, sikia kisa hiki cha kusikitisha.
Ni mfano hai niliosimuliwa na jirani yangu akisononeshwa na hatua iliyochukuliwa na mama mmoja ndugu yao hata kusababisha familia kusambaratika, kisa kampata mume kijana baada ya kufiwa na mumewe.

Mama huyu aliishi maisha ya raha na starehe na mumewe.
Walibahatika kupata watoto watatu, wavulana wawili na msichana mmoja.

Mumewe alikuwa mtu mwenye uwezo na madaraka makubwa. Kwa nafasi yake akaweza kujenga nyumba tatu, moja akiwa anaishi na familia yake na nyingine mbili akazipangisha.

Katika safari zake za kikazi, baba yule akapata ajali na hatimaye kufariki dunia. Wakati huo watoto walikuwa bado hawajaweza kujitegemea kwani wawili walikuwa katika ngazi ya sekondari na mmoja shule ya msingi.

Mama huyu badala ya kusimamia vema mali zile za urithi wa mumewe ili ziweze kutunza watoto wake, akaanza kupepesa macho kutafuta washikaji wa kumliwaza.

Inaelezwa na ndugu zake kwamba kazi yake kubwa ni kutafuta vijana wadogo wadogo ambao aliwalaghai kwa kuwapa fedha na bila shaka, zilizotokana na kodi za nyumba alizoacha mumewe. Mahali alipojua kuwa amekwama ni pale alipompata kijana mmoja kutoka visiwa vinavyozalisha karafuu kwa wingi.

Kijana huyu, hakika alimchengua shugamami huyu hata kupelekea kumhamishia nyumbani kwake.

Watoto wakiwa wanatizama kinachoendelea, mama akaweka mkakati akawafukuza wanawe wakaishi kwa ndugu na jamaa zao kwa maelezo kuwa anauza nyumba ile.

Shugamami huyu kwa kunogewa penzi la kijana wakaoana rasmi, kisha akaanza kuuza nyumba moja baada ya nyingine na zilipoisha wakahamia kwenye nyumba ya kupanga.

Akaamua kujiremba kwa vito vya thamani huku akivalia mavazi ya gharama ili amvutie mumewe huyo chekibobu.
Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo.

Shugamami huyu, ni miaka miwili sasa tokea mumewe afariki, lakini mali zote za mume ameziuza na sasa, kwa mujibu wa maelezo ya ndugu zake, anahama nyumba moja hadi nyingine, tena za bei nafuu baada ya maisha kumwendea kombo.

Mitaani anapita kwa kuvizia ili asikutane na mtu anayemfahamu kutokana na kuficha aibu. Vito vya thamani alivyokuwa amesheheni mwilini na mavazi ya gharama vimetoweka, fedha za mauzo ya nyumba za urithi zilishayeyuka, watoto hawataki hata kumuona mama yao kutokana na jinsi alivyowatelekeza na mambo mengine kibao.

Ama kwa hakika, mbio za sakafuni huishia ukingoni.
Na ngoma ikilia sana, iko mbioni kupasuka. Ndugu walimshauri mwanzoni namna ya kutunza mali zile kwa manufaa yake na watoto, lakini aliwapuuza.

Sasa majuto ni mjukuu na asiyesikia la mkuu, mwishoni huvunjika guu.

Laiti angetulia na kutafakari namna ya kutunza watoto wake, yote hayo yasingemkuta.

Sasa inaelezwa hata huyu mume kijana huenda akamwacha kwani mama sasa anakuwa tegemezi kuliko mtoaji kama ilivyokuwa awali. Si unajua tena penzi tamu kama asali linapogeuka shubiri.

Mpenzi msomaji, bila shaka umepata picha kamili ya kisa hicho kinachoacha maswali kibao. Wapo kinamama wanaotafuta bahati aliyokuwa nayo mama huyu niliyemzungumzia lakini wanaikosa.

Fikiria unaye mume mtafutaji, aweze hata kujenga nyumba kadhaa au kuwa na miradi kadhaa kwa ajili ya pato la familia, kwa mapenzi ya Mungu anatwaliwa, kisha nawe mbio unavuruga mali zote, tena kwa muda mfupi tu. Wewe ni mwanamke wa aina gani?

Tena, ukiwa unajua fika kuwa unao watoto, tena wako mwenyewe, unauza mali zote za urithi toka kwa baba yao(mumeo), unawaacha wanateseka. Nani atakusamehe kwa hilo?

Kisa cha hayo yote umempata mume kijana, chekibobu.
Kama ilikuwa ni lazima kujirusha naye, kwanini basi uuze mali zote ukafaidi naye badala ya kuwaachia watoto urithi toka kwa baba yao?

Ona sasa, nyumba zote kauza, watoto wamemsusa, chekibobu mbioni kumwacha na kuoa mwingine na kibaya zaidi wala mama huyu hakuzaa hata mtoto mmoja na kijana yule. Kama siyo laana ya Mwenyezi Mungu ni kitu gani?

Alitaka mtoto au watoto kwa kijana yule wakati wale waliotangulia aliwapiga teke?

Kwanini asingekumbatia wanawe, hata kama alimhitaji kijana wake huyo kama liwazo, ili kuwafariji na kuwaendeleza kimaisha?

Mpenzi msomaji, napata maswali mengi kichwani mwangu pasipo ukomo.

Hili ni tatizo ndani ya jamii yetu. Ukiona mfano huo umejitokeza hadharani, ujue ipo mingine mingi iliyofichika na familia husika kuendelea kugumia maumivu ya kimaisha kimya kimya. Hapana. Zungumza ili jambo hili likemewe hatimaye tuwe na familia zilizojengeka imara.

Labda tu kabla sijahitimisha niwaase kinamama kuchukulia mfano wa kisa hiki kama changamoto katika kupambana na tabia au maamuzi mabovu yanayosambaratisha familia badala ya kuzijenga.

Tuonyeshe mfano kwa kukataa tabia hii ya kupenda vijana wadogo ambao, wengine umri ni sawa na watoto mliowazaa.

Kama tunaiga kinababa- mashugadadi- tuache, tujikemee na kisha tuwakemee na kinababa.

Baba au mama ambao ni watu wazima ni aibu kuwa na mahusiano na vijana. hawa ni wazazi, walezi ambao busara zao zinategemewa katika kuwajengea maisha bora vijana wetu na si kuwabomoa.

Tabia hizi chafu za watu wazima kuvamia vijana na hata watoto wadogo ndizo zimechangia matukio ya aibu kama hilo nililozungumzia na pia mengine kama ya ubakaji kwa kuwa vijana wanaingia katika ngazi fulani ya maisha kabla ya wakati wao.

Tunalaumu eti vijana hawana adabu mbele za wazee kumbe baadhi ya wazee, watu wazima, wake kwa waume ndio hawana adabu mbele za vijana wetu.

Kama kweli tumepania kujenga kizazi kilicholelewa katika maadili mema, kinachoheshimika na kuheshimiana miongoni mwa watu wa rika zote, basi tupige vita hayo niliyojadili hapo juu.

Mpenzi msomaji, kumbuka mie nimechokoza. Kama unayo maoni au ushauri zaidi juu ya yaliyomo katika makala haya, unakaribishwa. Niandikie kupitia; Email:

fwingia@yahoo.com

Wasalaam

* SOURCE: Nipashe

No comments: