Monday, 15 October 2007

Jenerali Ulimwengu na 'ukarimu' wa Watanzania!

15.10.2007 1239 EAT

Amani si sera ya chama ni matokeo- Jenerali Ulimwengu
*Atadharisha ukarimu wa Watanzania kutumiwa vibaya
*Asema wapo sokoni yeyote mwenye fedha aweza kuwanunua
*Wasomi Mlimani washangilia, wakatiza mada yake, waimba

Na Joseph Lugendo
MWANDISHI mkongwe wa habari nchini na Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Bw. Jenerali Ulimwengu amesema amani si sera ya nchi yeyote duniani na kuhoji sababu za baadhi ya aliowaita watawala, kuihubiri kama sera ya chama.

Akitoa mada katika Kongamano la Kumbukumbu ya miaka 8 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana, Bw. Ulimwengu alisema hakuna mtu ambaye anachukia amani.

Alisema Mwalimu Nyerere aliwahi kusema amani haiji hivi hivi ila ni matokeo ya utekelezaji wa sera zilizowapa wananchi matumaini na kuhoji kama amani inapatikana kirahisi hivyo kwanini isingepatikana kwa wengine.

Aidha alitahadharisha watu wasitumie vibaya ukarimu wa Watanzania na kuongeza kuwa Siera Leone walikuwa wakarimu kuliko Watanzania lakini waligeuka ghafla na kuwa wakatili kiasi cha kukatana mikono.

Kwa mujibu wa Bw. Ulimwengu, ukatili huo ulisababishwa na utawala mbovu uliohusisha vitendo vya rushwa na kuonya kuwa wachochezi wa vita vya baadae ni mafisadi wa leo.

"Ogopa sana upole wa Mtanzania ambaye ukimkanyaga anaomba msamaha kwa kuweka mguu wake chini ya mguu wako," alisema Bw. Ulimwengu na kusababisha wanafunzi waliokuwepo kusimama na kuanza kumshangilia huku wakimba 'Sema usiogope sema sisi vijana hatuogopi vibaraka sema!'

Alikumbusha kuwa ingawa Mwalimu Nyerere alikuwa na katiba ambayo ilimruhusu kuongoza kidikteta katika mazingira ambayo hakukuwa na vyombo vya habari vya kusema hadharani, lakini hakuutumia uwezo huo kujinufaisha.

"Mwalimu angeweza kabisa kumwambia Bw. Edwin Mtei(Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania - BoT) achukue kiasi cha dola kadhaa kutoka BoT na kuziweka kwenye akaunti London kama Mobutu alivyofanya," alisema Bw. Ulimwengu na kuongeza kwamba hata kama watu wangetaka kumpinga yeye alikuwa na ushawishi mkubwa wa kuwaambia wananchi wawakatae na wakakatiliwa ila hakufanya hivyo kwakuwa alikataa mali.

Alisema wakati Mwalimu Nyerere alichukia dhuluma na utawala wa mabavu hivi sasa ni tofauti ambapo tatizo dogo linapotokea watawala hutuma vikosi vya Polisi wa Kutuliza Fujo (FFU) badala ya kutumia busara kidogo kutatua.

Alitolea mfano wa matumizi ya FFU katika vurugu zilizowahi kutokea katika eneo la Mwembechai Dar es Salaam na huko Pemba jambo ambalo liliwafanya wanafunzi waliokuwa wamefurika kupaza sauti na kusema 'Mfano mzuri ni hapa hapa !'

"Wakati mwingine kiongozi anaweza kusikiliza mawazo ya anaowaongoza hata kama yanapingana na yake na tatizo likaisha kwa kuruhusu watu kujieleza," alisema Bw. Ulimwengu na kuongeza kuwa watawala wanaotumia mabavu ni waoga wa hoja zitakazotolewa kwa kuwa hawana majibu ya hoja.

Alitoa mafano wa tatizo lililotokea chuoni hapo hivi karibuni la kumzuia Mbunge wa Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe ambaye naye alikuwepo chuoni hapo jana, kuzungumza kwenye mdahalo uliokuwa umeandaliwa na wanafunzi wa chuo hicho wiki mbili zilizopita na kusema tatizo sio Zitto ila ni kuwepo kwa maswali mengi na kwa muda mrefu kwa wananchi ambayo hayajapatiwa majibu.

Kuhusu hali ya utawala baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Bw. Ulimwengu alisema hakuna mtu au kiongozi anayeweza kusema hadharani kuwa hataki kumuenzi Mwalimu Nyerere lakini ukiwaambia watekeleze usemi wao, wanajiondokea.

Alisema Tanzania ina upungufu mkubwa wa viongozi kutokana na hali ya rushwa ambayo imefikia kununua wapiga kura na kuongeza watu wanaweza kupiga mahesabu wakiwa nje ya nchi jinsi ya kuja kununua uongozi.

"Mtu anaweza kuwa Texas Marekani na akatumia dola bilioni 3 kununua kura jimbo hadi jimbo," alisema Bw. Ulimwengu na kuongeza Watanzania wajijue kuwa wapo sokoni na yeyote mwenye fedha anayetaka kuwanunua, atawanunua.

Alisema hali hiyo inakuwa mbaya zaidi inapotokea sehemu kubwa ya fedha za bajeti inatoka nje ya nchi kwakuwa hata sera zitakuwa zinatoka nje ya nchi na kuongeza kuwa alikuwa na hamu ya kumuona Waziri wa Fedha Bi. Zakia Meghji muda mfupi kabla ya bajeti ya mwaka ili amuulize bajeti imekuja lini toka Washington Marekani?

Katika tukio lingine Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lilipofanyikia kongamano hilo, ulipambwa kwa mabango mbalimbali yaliyokuwa yaliyobeba ujumbe mzito.

Baadhi ya mabango hayo yalisema 'Mwalimu akifufuka leo Mtafanya kazi ofisi moja?'. Lingine liliandikwa 'Alichokichukia Mwalimu ndicho kinachopendwa sasa UFISADI.' Lingine 'Kutoka Baba wa Taifa hadi Vibaka wa Taifa.' Lingine Nchi itamalizwa kuunzwa lini? Je ndiyo mawazo ya Mwalimu?' Na lingine liliandikwa 'Mwalimu fufuka nchi inaangamia.'

Kitendo cha kutotokea viongozi wa kitaifa zaidi ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. John Magufuli, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt. Salim Ahmed Salim na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Bw. Joseph Butiku kilisababisha wanafunzi hao kuhoji kama siku ya jana ilikuwa ya kitaifa au na kuongeza kuwa kama Mwalimu angefufuka angewakana baadhi ya watu.

Akitoa maoni kuhusu michango ya wanafunzi hao, Dkt. Salim alisema alifurahi kuona vijana wakichangia hoja kwa ufasaha. Alisema Mwalimu alikuwa kiongozi nadra kutokea ambaye alitetea watu na kupambana na uonevu.

Alisema alikuwa msomi wa hali ya juu kwa kuweza kutafsiri mambo makubwa kwa lugha rahisi na kuungana na wanafunzi hao kwa kusema kuwa haitoshi kujivunia kuwa na Mwalimu Nyerere bali tujitahidi kutekeleza alivyosema.

Kuhusu hali ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt. Salim alisema Taasisi hiyo inamatatizo ya kukosa chanzo cha kudumu cha mapato na kuongeza kuwa baadhi ya watumishi akiwemo yeye, wanafanya kazi kwa kujitolea.

Awali akichangia hoja kwenye mada zilizotolewa, Bw. Hasmukh Maganial Pandya aliyejitambulisha kuwa ni muasisi Jumuiya ya Viajna wa TANU, alisema alisoma habari kuhusu hali ya ukoo wa Nyerere zilizochapishwa na gazeti la Majira Jumapili na kusikitishwa na jambo hilo na kutumia fursa hiyokuchangisha fedha kutoka kwa watu waliohudhuria kongamano hilo ili kusaidia ukoo huo.


Mwisho.....

source: gazeti Majira

No comments: