Nitaendelea kuiombea Tanzania -Baba Mtakatifu
Na Maura Mwingira, Vatican
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa XVI amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuendeleza amani n, Tanzania ikipewa kipaumbelea utulivu nchini.
Alisema Tanzania imeendelea kuwa ilivyo, kwa kuwa viongozi wake wameendelea kuienzi misingi mizuri ya uongozi, ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Hata baada ya kufariki dunia Nyerere Tanzania imeendelea na inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu, kwa sababu ninyi viongozi mliofuata baada yake mmeendelea kudumisha, kusimamia na kuendeleza amani na utulivu,” alisema Baba Mtakatifu.
Alitoa pongezi hizo jana, katika mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete yaliyofanyika kwenye maktaba ya Baba Mtakatifu, iliyoko makao makuu ya kiongozi huyo, Vatican.
Baba Mtakatifu alimwalika Rais Kikwete kumtembelea na kuzungumza naye. Rais yuko nchini Italia kwa ziara ya kikazi ya siku sita.
Kiongozi huyo wa kanisa alisema daima amekuwa akifurahishwa na mazingira ya amani na utulivu yaliyoko Tanzania; mazingira aliyosema yanawafanya Watanzania waendelee kuishi pamoja bila ya kujali tofauti zao za dini, rangi au kabila.
"Tanzania ni nchi tunayoipa umuhimu wa kipekee, ni nchi ambayo haina matatizo ya watu kugombana kwa sababu ya tofauti ya dini au rangi zao, ninafurahishwa sana na hali ya watu kuishi kwa pamoja na kwa amani.
Nitaendelea kuiombea Tanzania ili iendelee kuwa nchi ya amani,” alisema Baba Mtakatifu.
Alisema kanisa litaendelea kuchangia katika utoaji wa huduma ya elimu na zingine za kijamii kwa Watanzania, bila ya kujali tofauti zao za kidini.
Baba Mtakatifu alisema elimu ndiyo njia pekee itakayowawezesha Watanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwamo za vita dhidi ya ukimwi.
Baba Mtakatifu aliitaka Jumuia ya Mtakatifu Egidio kumwalika Rais Kikwete kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kimataifa wa madhehebu mbalimbali ya dini duniani. Mkutano huo utafanyika kesho katika mji wa Napoli, na Baba Mtakatifu atahudhuria.
Kwa upande wake, Rais Kikwete kupitia kwa Baba Mtakatifu, alilishukuru Kanisa Katoliki kwa huduma mbalimbali za kijamii, ambazo kanisa limekuwa likitoa kwa Watanzania.
Alitumia nafasi hiyo kulishukuru kanisa kupitia jumuia ya Mtakatifu Egidio, kwa kusaidia katika utafutaji na upatikanaji wa amani katika eneo la Maziwa Makuu, hususan nchini Burundi na maeneo mengine ya Afrika.
Alisema kanisa kupitia jumuia hiyo limekuwa likitoa mchango mkubwa katika utafutaji wa amani, na kwamba ni matumiani yake kuwa kanisa litaendelea na juhudi hizo.
Rais Kikwete alimwalika Baba Mtakatifu kuitembelea Tanzania pale atakapopanga kutembelea Afrika.
Kimsingi, Baba Mtakatifu alikubali ombi hilo, na kwamba baada ya kufanya ziara nchini Marekani na Australia, atapanga kutembelea Bara la Afrika, Tanzania ikipewa kipaumbele.
Baada ya mazungumzo hayo Rais Kikwete na Baba Mtakatifu walibadilishana zawadi, ambapo Baba Mtakatifu alimpatia Rais medali ya dhahabu ya upapa, na Rais alimpatia Baba Mtakatifu meza ndogo ya mchezo wa Chess iliyonakshiwa kwa urembo wa vinyago.
Gazeti Uhuru
Saturday, 20 October 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment