Saturday, 20 October 2007

Serikali yaboresha sekondari

Serikali yatoa mabilioni kuboresha sekondari

Ni kupitia mpango wa MMES
Yaonya watakaokiuka matumizi
NA MAGRETH KINABO
SERIKALI imepeleka mikoani zaidi ya sh. bilioni 45 za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), na kuzionya kamati za ujenzi na bodi za shule katika matumizi ya fedha hizo.
Fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, maabara, majengo ya utawala, hosteli, fidia ya ada kwa wanafunzi na chakula.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Da re Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta alisema taarifa za kupokewa na matumizi ya fedha hizo ifikishwe wizarani ifikapo Novemba 30, mwaka huu.

Katika kusisitiza matumizi ya fedha hizo, alisema nakala za taarifa hizo zitumwe kwa uongozi wa mikoa na wilaya katika kipindi hicho.
“Taratibu za matumizi ya fedha za serikali zifuatwe …wizara ipate taarifa ya kupokewa kwa fedha hizo Novemba 30 …nakala zitumwe kwa uongozi wa mkoa na wilaya,” aliagiza Waziri Margaret.
Aliongeza: “Fedha zilizotumwa zitumike kama ilivyokusudiwa bila ya ucheleweshaji … kinyume cha hilo, kamati na bodi za shule zitahojiwa,” alisema Waziri Margaret.

Alisisitiza kuwa matumizi ya fedha hizo yawe ya uwazi na ushirikishwaji, na waratibu wa elimu ya sekondari wafuatilie maagizo hayo ya serikali.
Waziri Margaret alisema fedha hizo zilizopelekwa kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara tangu Oktoba 12 na 15, na zimegawanywa katika mafungu ya ruzuku ya uendeshaji na maendeleo.

“Tumeona ni vizuri kuwajulisha wananchi kuwa serikali imeshatuma fedha kila mkoa kupitia hazina ndogo, kwa wakati huu lengo ni kuunga mkono nguvu za wananchi ili ujenzi wa madarasa na miundombiu mingine ikamilike mapema iwezekanavyo,” alisema.
Alisema ujenzi huo utasaidia kujua idadi ya wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza mwakani, ambao unakusudiwa usiwe chini ya asilimia 75.
Waziri Margaret alisema kati ya fedha hizo sh. 20,038,000,000 za ruzuku ya maendeleo, zitatumika kwa ujenzi wa nyumba 1,470 za walimu, ambazo zitagharimu sh. bilioni 13.5.
Margaret alisema fedha hizo pia zitatumika kwa ujenzi wa madarasa 777, maabara 84, maktaba 19, hosteli 12 na majengo ya utawala tisa katika mikoa mbalimbali nchini.
Alisema zaidi ya sh. bilioni 25.1 zimetolewa kwa ajili ya uendeshaji, ambapo sh. bilioni 5.7 zitatumika kwa chakula katika shule za bweni, wakati sh. bilioni 10.1 zikiwa fidia ya ada, na sh. bilioni 9.1 kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Waziri Margaret alisema serikali pia imepeleka kwenye hazina hizo sh. bilioni 3.8 kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotoka kwenye familia zenye kipato duni.
Alisema barua zimetumwa kwa wakuu wa shule kuhusu kiasi cha fedha kilichotumwa na matumizi yake kupitia kwa maofisa wa elimu wa mikoa, hivyo shule zinatakiwa kufuatilia ili kupata fedha hizo kwenye hazina ndogo.

Mgawanyo wa fedha hizo kimkoa ni kama ifuatavyo:
Arusha sh. milioni 976, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu (70), madarasa (37), maabara (nne) maktaba (moja) na hosteli (moja).
Dodoma sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37) maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Dar es Salaam sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne) maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Iringa, sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Kagera sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne) maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Kigoma sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Kilimanjaro sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Lindi sh. milioni 967, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne) na hosteli (moja). Manyara sh. milioni 976, nyumba (70) madarasa (37), maabara (nne), hosteli (moja) na maktaba (moja).
Mara sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Mbeya sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne) maktaba (moja ) na jengo la utawala (moja).
Morogoro sh. milioni 967, nyumba (70), maabara (nne), madarasa (37) na hosteli (moja).
Mtwara sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Mwanza sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Pwani sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Rukwa sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Ruvuma sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Shinyanga sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne) maktaba (moja) na hosteli (moja).
Singida sh. milioni 976, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na hosteli (moja).
Tabora sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).
Tanga sh. milioni 968, nyumba (70), madarasa (37), maabara (nne), maktaba (moja) na jengo la utawala (moja).


Gazeti Uhuru

No comments: