Tuesday, 16 December 2008

Ukistaajabu ya Musa utaona ya 'SIRIKALI'!

Richmond bado yaitesa Serikali
Serikali imefungua uwanja mpya wa mapambano dhidi ya wabunge baada ya kutangaza wazi kwamba ina mpango wa kununua mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Dowans, uamuzi ambao unapingwa vikali na wawakilishi hao wa wananchi.

Dalili za kuibuka kwa mapambano kati ya watunga sheria na watawala, zilijidhihirisha jana baada tu ya kubainika kwamba zile tetesi za muda mrefu kuwa serikali ilikuwa na mpango wa kununua mitambo hiyo zilikuwa za kweli, baada ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuwathibitisha wabunge kuwa mpango huo ni wa kweli.

Mipango ya serikali iliwekwa hadharani jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shelukindo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu msimamo wa kamati yake kuhusiana na suala hilo.

Mara kadhaa gazeti hili limewahi kuandika kuwa kuna mpango wa siri wa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kutaka kununua mitambo ya Dowans, lakini habari hizo zimekuwa zikikanushwa na wahusika au kutotolewa ufafanuzi wa kutosha.

Shelukindo aliweka mambo yote hadharani mbele ya waandishi wa habari kuwa serikali imefikia uamuzi wa kununua mitambo hiyo kwa gharama ya Sh. bilioni 70.

Alieleza kuwa kamati yake juzi iliitwa na Waziri Ngeleja, na kuelezwa uamuzi huo wa serikali na kutakiwa kutoa maoni yake.

Hata hivyo, Shelukindo alisema kamati yake imeieleza wazi serikali kuwa haikubaliani na uamuzi huo kwa kile alichoeleza kuwa unakwenda kinyume cha Azimio la Bunge ambalo linataka mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kampuni ya Richmond ambayo iliiuzia mitambo hiyo Dowans kwanza yatekelezwe kabla ya kufikiwa uamuzi wowote wa kuinunua mitambo hiyo.

``Jana (juzi) kamati iliitwa kwenye kikao cha dharura na Waziri wa Nishati na Madini kuelezwa uamuzi wa serikali kutaka kununua mitambo ya Dowans na tukatakiwa kutoa maoni yetu.

Sisi kama wabunge tumekataa kushirikishwa katika uamuzi huo kwa sababu kwanza kanuni za Bunge haziruhusu jambo lililokwisha pitishwa na Bunge kujadiliwa upya na pili, Sheria ya Manunuzi ya Umma hairuhusu serikali kununua vifaa au mitambo chakavu,`` alisema Shelukindo.

Shelukindo ambaye katika mkutano huo na waandishi wa habari alikuwa amefuatana na mjumbe mmoja wa kamati yake, Christopher Ole Sendeka, alionyesha wazi kukerwa na uamuzi huo wa serikali, ambao alisema ni dharau kwa Bunge.

Alifafanua kuwa moja ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mkataba wa Richmond ni kutaka watu wote waliohusika kupitisha mkataba huo wachukuliwe hatua za kisheria, lakini kamati yake ikashangazwa kuona kuwa kabla ya hatua hizo kuchukuliwa, serikali imechukua uamuzi wa kutaka kununua mitambo hiyo iliyoleta matatizo makubwa.

``Tulitegemea tumeitwa ili tuelezwe utekelezaji wa maazimio ya Kamati Teule ya Bunge iliyokuwa ikichunguza mkataba wa Richmond na si kuibua tena suala la Dowans, kuihusisha Kamati ya Bunge katika maamuzi haya ni kinyume cha taratibu kwa sababu ilishaamuliwa na Bunge kwa hiyo kuridhia itakuwa ni kuleta mgogoro kati ya Bunge na Serikali,`` alisema Shelukindo, ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM).

``Hii ni sawa umemkamata mwizi wa mali yako na baada ya kumkamata mnakaa kuzungumza ili akuuzie mali aliyokuibia,`` alisema.

Alieleza kuwa kama Serikali iliona kuna umuhimu wa kuchukua uamuzi huo, kwanza ilitakiwa kujenga hoja ya msingi badala ya kulifanya jambo hilo kuwa siri na kisha kuwashtukiza wabunge kutaka ushauri wao.

``Tumeambiwa kuwa mitambo ipo minne lakini yote imekwisha tumika isipokuwa mmoja ambao ni mpya kidogo, lakini pia umetumika, sheria ya manunuzi ya umma inakataza serikali kununua mitambo chakavu,`` aliongeza.

Kwa upande wake, Ole Sendeka alisema kisheria serikali hairuhusiwi kununua vitu chakavu, lakini inashangaza Wizara ya Nishati na Madini inataka kununua mitambo chakavu.

Alisema ni heri hizo Sh. bilioni 70 zikatumika kuimarisha miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kutafuta vyanzo vingine vya uzalishaji umeme kuliko kununua mitambo hiyo.

Sendeka alisema wabunge wameshangaa kuarifiwa uamuzi huo wa serikali siku mbili kabla haijapeleka zabuni ya kununua mitambo hiyo.

``Tumekataa kushiriki kubariki kutumia Sh. bilioni 70 kununua mitambo chakavu, serikali ikiamua kufanya hivyo tutajuana mbele, lakini hatutaki kuwa sehemu ya manunuzi hayo,`` alisema Ole Sendeka.

Akizungumza na Nipashe hivi karibuni, Ngeleja alisema hawezi kulizungumzia suala la endapo serikali ina mpango wa kununua mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Dowans, kwa kile kile alichoeleza kuwa suala hilo kwanza ni lazima lipitie ngazi mbalimbali za maamuzi za serikali pamoja na kufuata taratibu za kisheria.

``Siwezi kuzungumzia suala hili, unajua serikali ina ngazi zake mbalimbali za maamuzi na kama lipo ni lazima lipitie kwanza ngazi hizo pamoja na kufuata taratibu za kisheria,`` alisema.

Hata hivyo, Ngeleja alisema serikali katika mipango yake ya kushughulia tatizo la uhaba wa umeme nchini, imejiwekea mikakati ya muda mfupi na ya muda mrefu ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo hilo na moja ya mikakati hiyo ni kununua mitambo mipya ya kuzalisha umeme.

Alipoulizwa na Nipashe, endapo katika mipango hiyo ya serikali ya kununua mitambo mipya inafikiria kununua mitambo ya kampuni ya Dowans, alisema hawezi kuzungumza lolote kwani serikali ina taratibu zake za kushughulikia suala kama hilo.

``Unajua kama nchi tuna tatizo kubwa la uhaba wa umeme na katika kulitafutia ufumbuzi suala hili na ni lazima tutanunua mitambo mipya kwa sababu ni jambo muhimu,`` alisisitiza waziri huyo.

Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, katika wiki ya mwisho ya mkutano wa 13 wa Bunge mjini Dodoma, ilimuita Ngeleja na kumuonya dhidi ya uamuzi huo kwani ni ukiukaji na dharau dhidi ya agizo la Bunge na ni mwendelezo wa maslahi binafsi ya watendaji waandamizi wa Tanesco kwenye Dowans iliyonunua mitambo hiyo kutoka kampuni ya Richmond.

Baada ya Shelukindo kutangaza uamuzi wa kamati yake jana, Ngeleja alitafutwa na Nipashe kutoa maoni yale, lakini simu yake ya kiganjani wakati wote ilikuwa haipatikani.
(SOURCE: Nipashe, 2008-12-16 11:52:35 Na Abdallah Bawazir na Joseph Mwendapole)

No comments: