Saturday, 13 December 2008

Jengo la Maliasili Samora Ave. lawaka moto

Ofisi ya Waziri nusra iungue


Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii iliyopo katika Mtaa wa Samora Jijini imenusurika kuungua wakati sehemu ya jengo la wizara yake liliposhika moto usiku wa kuamkia leo.

Kaimu Kamanda wa Polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Evarist Mangala, amesema moto huo ulianza jana kuanzia mishale ya saa 5:30 usiku na kuendelea kwa saa kadhaa kabla ya kuzimwa.

Akasema moto huo ulianzia katika ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo katika ghorofa ya tatu na kisha kusambaa kwenye ofisi nyingine zilizopo kwenye jengo hilo.

Kamanda Mangala amesema sehemu kubwa ya ofisi ya Katibu Mkuu huyo wa Wizara inayoongozwa na Waziri Shamsa Mwangunga, imeteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa.

Amevitaja baadhi ya vitu vilivyoteketea kwa moto kuwa ni kompyuta, simu, kabati, seti ya televisheni na mafaili kibao muhimu yaliyokuwa ndani ya ofisi hiyo.

Hata hivyo, Kamanda Mangala amesema moto huo ulidhibitiwa na watu mbalimbali walioshirikiana na askari wa zimamoto ambao waliwahi kufika eneo hilo na kutekeleza wajibu wao.

Aidha, amesema chanzo cha moto huo kinadhaniwa kuwa ni hitilafu ya umeme, ingawa akadai kuwa uchunguzi zaidi wa kitaalam kuhusiana na tukio hilo bado haujafanyika ili kubaini chanzo cha kuwepo na hitilafu hiyo ya umeme.

Kamanda Mangala ameongeza kuwa moto huo haukuwa na madhara yoyote kwa binadamu na kwamba hadi sasa, hasara halisi iliyotokana na tukio hilo bado haijafahamika.

(SOURCE: Alasiri, 2008-12-12 21:48:36 Na Emmanuel Lengwa na Kiyao Hoza, Jijini)

No comments: