Monday 29 December 2008

"Hatusomi, hatudadisi!!!"

Watanzania hatusomi, hatudadisi
NILIPATA kusimulia kisa kifuatacho. Kuna wakati mwandishi wa safu moja ya gazeti nchini alipata kuambiwa na Profesa Seithy Chachage kuwa tatizo kubwa la wanafunzi wake, yaani wanafunzi wa Chachage, ni kutopenda kujisomea.

Jambo hili nilipata kuliandika huko nyuma. Lakini kwa vile bado ni tatizo kubwa, basi, tunahitaji kukumbushana. Chachage alisema wanafunzi hao wakiwa chuoni, husoma kwa ajili ya kufanya mitihani ili wavuke kwenda mwaka unaofuata. Kwamba mtindo wao wa kusoma ni wa madesa (vitini) tu na si vitabu.

Kwa mujibu wa mwandishi huyo, Chachage alilalamika kwamba wanafunzi walio wengi hushindwa kupambanua mambo kadhaa yanayowazunguka. Ni dhahiri, kwa anayefuatilia jamii yetu kwa sasa, hatapata taabu sana kukubaliana na maelezo ya Chachage kwa rafiki yake huyo.

Ni kweli kuwa Watanzania tulio wengi, na si wanafunzi pekee, tumepoteza utamaduni wa kusoma. Inafika mahala mwanafunzi au hata aliye nje ya shule anaangalia kwanza ukubwa wa kitabu na wingi wa kurasa kabla ya kuamua kuazima au kununua kitabu badala ya kuangalia maudhui ya kitabu husika. Imejitokeza hofu juu ya kurasa za kitabu, zisiwe nyingi sana, vinginevyo msomaji anatishika nacho.

Hakuna atakayebisha, kwamba nchi yetu haiwezi kupiga hatua zozote za maana kuelekea kwenye chochote kinachoitwa maendeleo kama watu wetu walio wengi hawatapenda kujisomea, kujiendeleza kimaarifa na hivyo basi, kujijengea uwezo wa kudadisi mambo.

Wengi tumekuwa wavivu sana wa kusoma. Leo ni kawaida kumkuta kijana aliyemaliza kidato cha nne hata cha sita bila hata kusoma maandiko yeyote yale ya Shaaban Robert kwa kutoa mfano wa mwandishi mmoja. Itawezekana vipi kijana wa Kitanzania amalize miaka 20 shuleni bila kusoma hata kurasa tatu tu za maandiko ya Shaaban Robert ukiacha waandishi wengine mahiri wa nchi hii?! Hivi kijana huyu atajijua kweli kuwa yeye ni nani kwa maana ya utambulisho wake?

Katika Kenya hakuna kijana anayemaliza miaka 20 shuleni bila kumsoma Ngugi Wa Thiong'o. Nigeria hakuna kijana anayemaliza miaka 20 shuleni bila kumsoma Chinua Achebe au Wole Soyinka. Iweje katika nchi yetu vijana wamalize miaka 20 shuleni bila kusoma maandiko yaliyojaa hekima na yaliyosheheni utamaduni wetu kama yale ya Shaaban Robert? Maandiko kama: Adili Na Nduguze, Kusadikika, Utu Bora Mkulima na mengineyo.

Hadi hii leo,tunaamini, kuwa katika Afrika ya Mashariki nzima hajatokea mwandishi wa fasihi kwa lugha ya Kiswahili mfano wa Shaaban Robert. Si ajabu, kuwa marehemu Shaaban Robert alitokea kuwa mwandishi mzuri. Shaaban Robert alikuwa ni msomaji mzuri wa vitabu vya hadithi, mashairi na maarifa mengine.

Naam. Elimu juu ya maarifa mbalimbali humu duniani hupatikana kwa mtu kujiendeleza kielimu. Hatua ya kwanza na ya msingi kabisa katika kuelekea kwenye mapenzi na elimu ni ile hali ya mtu kupenda kujisomea vitabu hata vile ambavyo viko nje ya mitaala ya shule na vyuo.

Ni ukweli usiopingika, kuwa utamaduni wa kujisomea umedorora na unaendelea kudorora mno katika jamii yetu. Kudorora kwa utamaduni wa kujisomea kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini na pia mabadiliko ya kijamii yaliyojitokeza katika miaka ya karibuni.

Si ajabu siku hizi kwa watoto na hata wazazi kuchukua muda wao mwingi kuangalia televisheni na hivyo basi kutotilia maanani suala zima la kujisomea. Ni rahisi mno kukaa kwenye kiti na kuangalia televisheni badala ya kuchukua kitabu na kujisomea.

Watanzania pia wamepoteza utamaduni wao wa miaka mingi wa kusikiliza vipindi vya maarifa redioni. Wengi wanapendelea kusikiliza idhaa za redio zenye kupiga muziki kutwa kucha. Muziki unaoambatana na matangazo na vipindi vya kijamii visivyofanyiwa utafiti na wala maandalizi ya kutosha. Tunaamini, kuwa miaka ya nyuma Watanzania walikuwa na upeo mkubwa wa uelewa wa mambo yanayotokea ndani ya nchi na hata kimataifa.

Hili la kudumaa kwa utamaduni wa kujisomea limesababisha pia kudumaa na kushuka kwa viwango vya ubora wa uandishi, Uwe uandishi wa habari, hadithi na hata ripoti mbali mbali. Umefika wakati wa sisi wenyewe kuchukua hatua za makusudi kabisa za kujijengea utamaduni wa kujisomea. Tujijengee kiu ya kupenda kusoma.

Tukumbuke pia, kuwa kiu ya kusoma haiji hivi hivi tu, inajengwa utotoni na hata ukubwani. Katika hili Shaaban Robert alipata kuandika: " Bahati haiji yenyewe, hunyoshewa mkono au hufuatwa". Na ndivyo ilivyo kwa maarifa. Hayaji yenyewe bila kujibidisha kujisomea.

Tujitahidi kubadilika na kuondokana na mtazamo hasi juu ya vitabu. Baadhi yetu, tangu utotoni, shule na vitabu huwa ni kama uchungu wa lazima kuupitia. Ukishamaliza masomo, basi, huwa mwisho wa kusoma vitabu. Walio shuleni hawajengewi misingi imara ya kupenda kujisomea hata baada ya kumaliza masomo. Wanasoma ili wafaulu mitihani, wanakariri majawabu. Hatuwaandai watoto wetu wawe ni watu wenye kuuliza maswali, kudadisi na kuhoji ili waongeze zaidi maarifa yao.

Mwisho kabisa, kusoma ni burudani kama burudani nyingine. Ukisoma kitabu ukipendacho utafurahi, utacheka peke yako, utasikitika, utatokwa na machozi, utafarijika. Kwa kupitia vitabu unaweza kupata maarifa mbali mbali katika ulimwengu huu. Unaweza kusafiri katika maeneo ambayo hujapata kufika, na kujua jiografia ya sehemu hizo, yote haya kwa kupitia maandiko tu, vitabu. Wakati tukiumaliza mwaka huu jiulize; nimesoma vitabu vingapi mwaka huu?
(chanzo: Raia Mwema, Na Maggid Mjengwa Disemba 24, 2008 Simu: 0754 678 252
Barua-pepe: mjengwamaggid@gmail.com Blogu: mjengwa.blogspot.com)

No comments: