Saturday, 6 September 2008

Wauwawa kwa tuhuma za wizi wa ng'ombe

Gazeti limegeuza habari, hii sio vita ya kikabila bali ni tuhuma za wizi wa mifugo, kama vile kibaka anavyotuhumiwa na kupigwa au kuchomwa moto na watu wanaojichukulia sheria mikononi.
Ni vizuri waandishi wawe wanatafsiri vema habari na sio kuwashambulia wakurya.
-na mosonga.
.........................

Mapigano ya kikabila yaibuka tena Tarime
*Safari hii ni ya Wamera na Waunyaga

WATU watatu wameuawa kwa kuchomwa mishale na kukatwa mapanga katika ugomvi wa koo mbili za Wakurya wilayani Tarime mkoani Mara na kusababisha kuteketezwa kwa moto nyumba 39.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Bw. Stanley Kolimba, alisema jana watu hao waliuawa juzi katika mapigano hayo yanahusisha koo za Wamera na Waunyaga wote wa kata ya Numera wilayani hapa.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Tarime, aliwataja watu waliouawa katika vita hiyo ya kikabila kuwa ni Nyaibarwi Samwel (30) wa ukoo wa Waunyaga katika kijiji cha Turugeti, Otaigo Nyaisori (55) wa ukoo wa Wamera katika kijiji cha Kitenga na Marwa Mtunda (25) wa ukoo wa Wamera katika kijiji cha Kwisarara.

Bw. Kolimba alisema miili ya Samwel na Nyaisori zimehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime, lakini mwili wa Mtunda haukufikishwa katika chumba cha maiti kutokana na kuwa vipandevipande, hivyo kushindikana kuviokota kirahisi.

Alisema chanzo cha mapigano hayo kinaaminika kuwa ni wizi wa mifugo, ambapo juzi inadaiwa kuwa ukoo wa Waunyaga waliiba ng’ombe mmoja wa Wamera na wakati wakifuatilia ng'ombe huyo ndipo vita hiyo ilipoanza.

Alisema nyumba hizo zilizoteketezwa kwa moto siku hiyo moja, 34 zikiwa za Wamera na tano za Waunyaga na kusababisha familia hizo kukosa makazi.

Mkuu wa Wilaya aliagiza kupelekwa kwa polisi wa Kikoisi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walidhibiti mapigano hayo kwa kiasi kikubwa huku akisema kuna baadhi ya watu walijeruhiwa ingawa hawakutaka kufikishwa hospitalini.

Wakati koo hizo zikiibua mapigano hayo mapya, pia koo za Wanchari, Wakira na Warechonka, zimekuwa zikiwindana hali ambayo ilililazimu Jeshi la Polisi mkoa wa Mara kuweka ulinzi mkali katika maeneo hayo ya kata ya Mwema.
source: majira, Na George John, Tarime. 06.09.2008 0129 EAT

No comments: