Shilingi Milioni 358 zaliwa
Jumla ya Sh. Milioni 358 zilizokuwa zitumike kwa shughuli mbalimbali za kuiendeleza nchi na wananchi wake zimeangukia mikononi mwa `wajanja` Serikalini na kuliwa.
Mamilioni hayo ya fedha yanadaiwa kuidhinishwa kiujanja na afisa mmoja wa zamani pale Hazina Jijini Dar na hatimaye kuyeyuka kama moshi hewani.
Pesa hizo inadaiwa ziliyeyuka kwa staili ya mishahara kwa wafanyakazi hewa.
Erady Sanga, aliyekuwa Afisa wa Hazina, ndiye anadaiwa kucheza dili hiyo.
Hata hivyo tayari ameburuzwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma hizo.
Kigogo hiyo anadaiwa kuidhinisha mishahara kwa watumishi hewa wa halmashauri 12 za wilaya nchini.
Sanga ambaye alikuwa Kamishna Msaidizi wa Bajeti na maafisa wengine saba wa zamani pale Hazina, wanatuhumiwa na makosa mbalimbali ya rushwa na wizi ulioisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. Bil 1.5.
Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa, PCB, Bw. Ernest Makale ameiambia mahakama iliyokuwa chini ya Hakimu Mkazi Sivangilwa Mwangesi kuwa watuhumiwa walitenda makosa yao kati ya mwezi Januari na Agosti mwaka mwaka 2002.
Upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na waendesha mashtaka Lizy Kikwia na Tabu Mzee, umedai kuwa katika kipindi hicho, Sanga aliidhinisha jumla ya Sh. 2,729,204,585, yakiwemo malimbikizo ya Sh. 670, 782, 997.
Kwa mujibu wa Ofisa wa PCB, malipo hayo yaliyoidhinishwa yalihusisha pia kiasi cha Sh. Milioni 308,437,132 kama mshahara kwa watumishi wa Halmashauri za wilaya tano za Musoma, Kisarawe, Tabora, Korogwe na Tarime.
Bw. Makale ameiambia Mahakama kuwa Kamishna huyo msaidizi wa bajeti alifanya hivyo kwa makusudi, akijua kuwa kiasi alichoidhinisha ni zaidi ya kile kilichotakiwa kwa mishahara ya watumishi wa Halmashauri hizo za wilaya kutokna na ukweli kuwa baadhi walishapunguzwa.
Kesi hiyo itaendelea tena Machi 6 mwakani. Wengine walioburuzwa kizimbani ni Mhasibu Godfrey Bwana, Wataalam wa kompyuta Herbert Tenson, Arnold Matoyo na Mkuu wao Cleofas Mutayabalwa.
(SOURCE: Alasiri, 01 Feb 2007. By Mwandishi Wetu, Jijini)
Friday, 5 September 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment