Saturday, 15 March 2008

Kanisa lapigwa stop Kiagata!

Serikali mkoani Mara, imevunja kambi ya mchungaji wa kanisa la Wasabato wenye msimamo mkali, linalohubiri kushuka kwa Yesu mwezi ujao, hatua ambayo imewafanya baadhi ya waumini wake kuanza kuuza vitu vyao.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Bw. Saveli Maketta, aliliambia gazeti hili mjini hapa kuwa kambi ya mchungaji huyo, Ephraem Mtabi, iliyokuwa katika kijiji cha Kyagata, wilayani hapa ilivunjwa Machi 12 kwa ushirikianao wa jeshi la polisi.

Bw. Maketta alisema kuwa mchungaji Mtabi, mkazi wa mjini Bunda, awali alikuwa ni muumini wa kanisa la Wasabato halisi, lakini baadaye alijiengua na kuanzisha kanisa lake ambalo lina msimamo mkali.

Baadhi ya wananchi wamemfananisha Mtabi na \'Askofu\' Joseph Kibwetere, kiongozi wa Kanisa la Kurejesha Amri 10 za Mungu, ambaye alisababisha waumini wake kujilipua moto nchini Uganda kwa kuamini kwamba mwaka 2000 ulikuwa mwisho wa dunia.

Bw. Maketta alisema alipata habari za kuwepo kwa mchungaji huyo katika wilaya yake, kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, ambaye pia alizipata taarifa hizo kutoka kwa raia wema wakiwemo walimu wa shule na wanafunzi, ambao pia walijiunga na kanisa hilo na kuacha masomo.

``Mchungaji huyo amekuwa akihatarisha amani katika jamii, kwa kuhubiri hivyo, kwani watu watakaposubiri bila kumuona huyo Yesu, kwa siku walizoambiwa, wanaweza kukata tamaa ya kuishi, na hivyo wanaweza kujiua au hata kumuua yeye mwenyewe... Sasa sisi kama serikali tumeliona hilo na kuchukua hatua ya kuvunja kambi hiyo mara moja,`` alisema.

Aliongeza: ``Kuna madai ya baadhi ya wanafunzi waliojiunga na kanisa lake kuacha masomo. Tumesikia kwamba baadhi yao hawakufanya mitihani yao ikiwemo ya kidato cha nne.``

Alisema alimuagiza ofisa tarafa kufanya uchunguzi na tathmini haraka, ili hatua zichukuliwe.

Alisema katika mahubiri yake mchungaji huyo alisisitiza kwamba Yesu atashuka mwezi Aprili mwaka huu, katika kijiji cha Kyagata na kwamba amekuwa akiwataka watu mbalimbali wakiwemo waumini wa kanisa hilo kujiandaa, ili waweze kupaa na mwokozi huyo.

Imeelezwa kuwa kutokana na mahubiri hayo, watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi walihama makwao na kwenda katika kambi ya mchungaji huyo ili kushirikiana naye katika kuhubiri ujio wa Yesu Kristo, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wengine waweze kujiunga na kanisa hilo na kukaa mkao wa kumsubiri.

Taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya waumini wenzake walikwishauza baadhi ya vitu vyao, kikiwemo chakula na mifugo, ambapo pia wanafunzi wamekataa kusoma kwa madai kuwa hawawezi kusoma wakati ufalme wa mwenyezi Mungu umekwisha kutimia na hivyo wanasubiri kupaa mbinguni.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Bw. David Saibullu, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mahubiri ya mchungaji huyo yanahatarisha amani na kwamba bila kudhibitiwa mapema, yanaweza kuleta maafa makubwa kama ilivyokwisha kutokea nchini Uganda, ambako waumimi wenye msimamo mkali walijifungia kanisani na kujilipua kwa moto.

Kamanda Saibullu alisema kuwa jeshi la polisi linawashikilia na kuwahoji watu kadhaa, wakiwemo wanafunzi wanne.

Walioshikiliwa ni Edina Joseph na Nimrod Machumu, wanaosoma katika Shule ya Sekondari Lubana ya wilayani Bunda, Eliza Joseph, Shule ya Msingi Migungani, Bunda na Manyama Benabato, Shule ya Msingi Namibu A.

Wengine ni Katibu wa kanisa hilo, Mussa Waitaro, mkazi wa Kyagata, pamoja na wazazi wawili wa wanafunzi hao, ambao ni Joyce Paul na Nyanjura Machumu, wote wakazi wa wilayani Bunda.

Kamanda Saibullu, alisema kuwa Mchungaji wa kanisa hilo kwa sasa yuko safarini mkoani Tabora, ambako inadaiwa kuwa amekwenda kuhamasisha watu wengine waweze kujiunga na kanisa lake.

* SOURCE: Nipashe, 15 Mar 2008
By Ahmed Makongo, Musoma

No comments: