Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wameanzisha mkakati maalum wa dharura utakaomuwezesha mteja kutoa mzigo wake ndani ya siku moja.
Mkakati huo unalenga kuondoa mrundikano wa makontena na mizigo mingine inayopitia katika bandari hiyo.
Kadhalika, kuanzia sasa mteja hatalipa gharama za kusafirisha makontena kutoka bandarini kwenda bandari ya nchi kavu iliyoko Ubungo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Meneja wa biashara wa kampuni inayoshughulika na utoaji wa makontena Bandarini ya (TICTS), Bw. Jay Nen, alisema mteja akiwasilisha kwao vielelezo vyote anaweza kupata mzigo wake ndani ya siku moja.
Alisema mkakati huo ni mpya ambao hivi sasa umeanza kufanya kazi.
Aliongeza kuwa utaratibu wa utoaji wa mizigo ni mrefu na ambao unahusisha watu wengi lakini mara mteja anapofika TICTS atahudumiwa kwa muda usiozidi siku moja.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari, Bw. Jason Rugaihuruza, alisema mteja alikuwa akiumia kwa kulipa gharama za kupeleka makontena Ubungo.
Kwa mujibu wa wateja gharama hizo zilikuwa zinafikia dola 500 za Marekani kiasi mbacho ni kikubwa na kwamba hivi sasa TICTS yenyewe itazilipa.
Bw. Rugaihuruza alisema, kupitia mkakati huo hivi makontena 800 yamepelekwa kuhifadhiwa Ubungo na kwamba mamlaka zote zimeagizwa kufanya kazi kwa saa 24.
Aidha, Bw. Rugaihuruza alisema, mrundikano wa makontena hivi sasa umepungua kutoka 11,000 hadi kufikia 8900 na wanataka yafikie 7500.
Aliwataka wateja kuharakisha ulipiaji wa mizigo yao kwani mkakati huo umelenga kuwasaidia wao.
Aliwataka wadau wote wa Bandari wakiwemo Mamlaka ya Mapato (TRA) kufanya kazi kama timu ili kuleta ufanisi na hatimaye kuondoa kupunguza mrundikano.
Mrundikano wa makontena na urasimu wa kutoa mizigo Bandarini ni moja ya kilio cha siku nyingi cha wateja ambapo walikuwa wakilalamikia mizigo yao kucheleweshwa.
* SOURCE: Nipashe, 06 Mar 2008
By Richard Makore
Thursday, 6 March 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment