Pinda awageukia vigogo waliojilimbikizia mali
* Asononeka masikini kuishi kwa 1,000/- kwa siku
* Askofu: Wananchi sasa wamepoteza matumaini
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda amewataka watumishi wa umma kuepuka uroho wa kujilimbikizia mali kwa lengo la kupata utajiri ndani ya kipindi kifupi hali inayoibua manung'uniko miongoni mwa wananchi.
Waziri Pinda aliwataka watumishi hao kumtanguliza Mungu katika kazi zao na kujiepusha na vitendo vya wizi.
Bw. Pinda alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati wa misa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mkingiwa wa Dhambi Asili Jimbo la Mpanda na kuongozwa na Padre Yustine Makungu.
“Ni lazima watumishi kama mimi wamtangulize Mungu katika kazi zao na wazifanye kwa uadilifu,” alisema Bw. Pinda na kuwataka waumini ambao ni watumishi wa umma kama yeye, kutambua kuwa wapo kwa faida ya Watanzania na si kwa ajili ya matumbo yao binafsi.
Kauli ya Bw. Pinda imekuja ndani ya kipindi ambacho baadhi ya vigogo na watumishi wa umma wamekuwa wakihusishwa na kashfa za ufisadi ikiwemo ya kuchota pesa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mkataba wa kampuni hewa ya kuzalisha umeme ya Richmond Development.
Hadi sasa serikali imefanikisha kurudishwa kwa sh. bilioni 50 zilizochotwa katika mazingira ya kifisadi ndani ya Benki Kuu huku zikiwepo taarifa za kuhojiwa kwa baadhi ya watu wanaotuhumiwa kwenye sakata hilo.
Hata hivyo wiki iliyopita, wakati akitangaza kurudishwa kwa pesa hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Bw. mustafa Mkullo alikataa kutaja majina ya wahusika kwa maelezo kwamba ni mapema mno kufanya hivyo.
Akizungumza kwenye misa ya jana, Bw. Pinda aliahidi kutumia wadhifa aliopewa kufanyakazi kwa nguvu na moyo wake wote kumshauri vizuri Rais ili kuinua hali ya maisha ya Watanzania.
Alibainisha kuwa Watanzania wengi ni masikini na wanaishi kwa shilingi 1,000 kwa siku kulingana na takwimu za kitaalamu, hata hivyo hakukubaliana na takwimu hizo na kusisitiza kuwa wananchi wengi hawana uwezo hata wa kupata kiasi hicho kwa siku.
“Wapo Watanzania ambao kwao kushika sh. 1,000 kwa siku ni kazi kubwa sana,” alisisitiza Bw. Pinda na kuongeza kuwa hizo ndizo changamoto zinazomkabili yeye na Rais Jakaya Kikwete ambaye ameahidi kwamba maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana.
Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo la Mpanda, Mhashamu Baba Pascal Kikoti, alimtaka Bw. Pinda kutumia wadhifa aliopewa kumshauri vizuri Rais Kikwete ili kupunguza manung’uniko ya watu ambayo yamezidi na kupoteza matumaini.
Alisema matatizo yamezidi kuwa mengi na kusababisha manung’uniko kwa wananchi. Alimtaka Waziri Pinda kuyashugulikia ingawa alisema hawezi kuyamaliza yote, lakini alisisitiza kwamba Watanzania wanahitaji kupewa matumaini.
Katika misa hiyo, kanisa hilo lilimzawadia, Bw. Pinda na mkewe Bibi Tunu Biblia, Rozali na sanamu ya Bikira Maria ili vimuongoze katika utendaji kazi wake.
Bw. Pinda ambaye yuko katika ziara ya siku tisa mkoani hapa, leo anaingia siku ya nne na anatembelea Wilaya ya Nkasi.
source: Majira, 03.03.2008 1151 EAT
Na Reuben Kagaruki, Mpanda
Monday, 3 March 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment