Thursday, April 02, 2009
Mkutano wa G-20
Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ambalo ningependa kuliongelea leo hii ni kuhusu msukusuko wa uchumi wa dunia na hasa mkutano wa Kundi la Nchi Ishirini Tajiri Duniani (G-20) ambao unategemewa kufanyika kesho tarehe 2 Aprili na kumazika tarehe 3 Aprili, 2009 mjini London, Uingereza. Mkutano huu umeitishwa kutafuta njia za pamoja za kukabili kudorora kwa uchumi duniani.
Mataifa haya tajiri ishirini, ambayo yanamiliki asilimia 85 ya uchumi wa dunia ni pamoja na Marekani, Uingereza, China, Japan, Ujerumani, Ufaransa, Afrika ya Kusini, Australia, Uturuki, Brazil, Canada, Argentina, Mexico, Indonesia, India, Italy, Urusi, Korea Kusini, Umoja wa Nchi za Ulaya na Saudi Arabia.
Kwa muhtasari, matarajio ya Afrika katika mkutano wa G-20 ni kwa Afrika kusaidiwa kujikinga na kukabili madhara ya kudorora kwa uchumi wa dunia.
Miongoni mwa mambo ambayo tuliyasisitiza ni;
1. haja ya kuanzishwa mfuko maalum ambapo fedha zake zitatumika kuzisaidia nchi za Afrika kuchukua hatua za kunusuru uchumi wao kama wafanyavyo mataifa tajiri.Kwa maneno mengine tuliunga mkono pendekezo la Benki ya Dunia na kutaka Mkutano wa G-20 ukubali kwamba asilimia 0.7 ya fedha walizotumia kugharamia mipango yao ya kuchochea uchumi wao (stimulus packages) zitengwe kwa ajili ya kusaidia kuchochea kukua kwa uchumi kwa nchi za Afrika.
2. tulisitiza kuwa nchi tajiri zisipunguze misaada ya maendeleo kwa nchi maskini. Badala yake misaada hiyo iongezwe kama walivyoahidi kwenye mikutano ya Monterrey, Gleneagles na kwingineko.
3. tulisema kwamba tunatarajia pia misaada kwa Afrika, na uwekezaji kutoka nje vitaelekezwa katika kujenga na kuboresha miundombinu, kuleta mapinduzi katika kilimo, kukuza biashara miongoni mwa nchi za Kiafrika na baina yake na nchi nyingine za dunia na kusaidia zaidi makundi katika jamii ambayo yanahitaji msaada zaidi (vulnerable groups).
4. kwamba nchi tajiri duniani pamoja na Taasisi za Kimataifa za Fedha Duniani zilegeze masharti na kupunguza urasimu wa kupata fedha za misaada na mikopo kwa kutambua kwamba hiki ni kipindi kugumu na cha dharura.
Aidha, masharti ya kukopa kutoka vyombo vingine vya fedha yalegezwe pia.
5. kwamba nchi tajiri zisaidie nchi za Afrika kujenga mitaji ya vyombo vya fedha vya kikanda kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika.
6. kwamba, nchi tajiri zitakubaliana kuruhusu uwazi katika mabenki yao na taasisi zao za fedha ili kuwezesha nchi za Kiafrika kufuatilia na kurudishiwa fedha, majumba na rasilimali zilizoporwa kutoka katika bara letu na kuhifadhiwa kisirisiri katika mabenki ya nchi tajiri.
Ndugu Wananchi, Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu Gordon Brown kwa kuyapokea mapendekezo haya ya Afrika kwa moyo mkunjufu na kuahidi kuyafikisha na kusaidia kuyatetea katika kikao hicho. Pia tunamshukuru amepokea rai ya Afrika ya kuwakilishwa kwenye mkutano huo kwa kumwalika Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Meles Zenawi, ambaye atatuwakilisha kwa kofia yake ya Uenyekiti wa NEPAD.
(hotuba ya Mhe Rais, 31/March/2009)
Thursday, 2 April 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment