Hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili dunia nzima kwa sasa, imeingia nchini Uingereza kwa kishindo. Waajiri wanapunguza wafanyakazi au kufunga kabisa shughuli zao na hivyo watu wasio na ajira wamekaribia milioni 3 kwa mujibu wa tarakimu za wiki iliyopita kutoka ofisi ya mtakwimu wa serikali.
Hali hii pia inapelekea misuguano ya kitabaka hasa baina ya wazawa na wahamiaji walioko hapa kutafuta maisha.
Magazeti ya leo yametoa kilio kikubwa kuwa wahamiaji kutoka nchi za Ulaya mashariki wanaua soko la ajira kwa wazawa kwa vile wahamiaji hao wanakubali kupokea ujira mdogo sana (chini ya theluthi ya kima cha chini). Imeripotiwa na magazeti hayo kuwa wahamiaji hao hupokea kiasi cha Paundi 2 za Uingereza kwa saa wakati kima cha chini ni Paundi 5 za Uingereza. Endapo hawa wahamiaji wataendelea kufanya kazi kwa ujira huo, ina maana kuwa waajiri wengi watawatumia ili kuokoa hala. Kwa hiyo waingereza wanataka wahamiaji hao waondolewe ili kazi hizo ziende kwa wazawa na kwa malipo halali.
Kwa maoni yangu, naona dalili za 'kiubaguzi' zinarejea taratibu kwa kisingizio cha uhaba wa ajira. Wazawa wanaibana serikali yao ili kazi zisiende kwa wahamiaji, lakini kwa kichinichini wale wabaguzi wanatumia mwanya huo kufikisha ujumbe na kutimiza ndoto zao. Maana kila wazawa wanapoongelea mambo haya ya ajira, wanaunganisha kuwa waondolewe wahamiaji.
Hii ni patashika, mwisho wake hakuna ajuae ...!
Monday, 16 February 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment