Kesho ni siku ya fainali ya Kombe la Ligi wenyewe wanaita Carling Cup - kwa sababu za udhamini. Fainali hiyo ni kati ya timu za Manchester United na Tottenham Hotspur (Spurs), itachezwa ktk uwanja wa kisasa kabisa wa Wembley uliopo ktk halmashauri ya mji wa Brent -kaskazini mwa jiji la London.
Kutokana na ratiba ya mechi hiyo, inaonekana United ndio watakuwa wenyeji na hivyo kuwa na haki ya kuvaa jezi zao za nyumbani (ingawa hata Spurs nao watavaa jezi zao nyeupe kwa vile hazifanani na za Manchester United).
Kutokana na United kuwa wenyeji, nategemea washabiki wake wataingia uwanjani kupitia mageti ya mashariki (mageti A, B, P na N) na pia kupitia mageti K na L nyuma ya goli la kusini mashariki. Kwa maana hiyo mashabiki wa Spurs watatumia mageti D, E, F na G kama wageni (away fans) na upande wa nyuma ya goli la kaskazini magharibi. Upande wa away team (timu ya genini) huangaliana na ngazi za kuingilia (ramps) za Pedestrian Way unapotokea stesheni ya Wembley Park.
Bendera za timu ya Manchester United, Chama cha soka -FA, na ya Tottenham Hotspur zinaning'inizwa kwenye paa la timu ya nyumbani kwa juu!
Nje ya uwanja mashabiki hupata nafasi ya kununua vitu (merchandise) vya timu zao mfano jezi, skafu, bendera n.k. bila kusahau 'matchday program' ambayo huuzwa Paundi 5 hadi 10 kwa kutegemea uzito wa mechi.
Mageti ya kuingia uwanjani hufunguliwa mapema siku za mechi -kama saa nne hivi kabla ya mechi - kwa hiyo kesho mageti yataanza kuwa wazi kuazia saa tano za asubuhi. kwa vile mechi inatarajiwa kuanza saa tisa alasiri za Uingereza.
Kwa wale wenye tiketi halali huingia kupitia vilango vidogo (turnstiles) ambapo tiketu zao huchambuliwa (scan) kuona kama ni za halali. Tiketi bandia hukataliwa na chombo cha ku-scan na hivyo mhusika huzuiliwa kuingia. Ukishaingia tu baada ya turnstile, kuna ukaguzi wa vitu ulivyo navyo kwa sababu za kiusalama na kama una chupa za glasi au makopo (cans) vitu hivyo huzuiliwa -huwezi kuingia navyo. Na kama una chupa za plastiki za maji au vinywaji, zinafunguliwa na vifuniko vinachukuliwa na walizi unapita na chupa yako bila mfuniko. (unajua chupa yenye mfuniko inaweza kutumika ktk fujo na ikawa silaha kumrushia mtu na kumjeruhi, ndio maana hazikubaliki kuwa na mifuniko au zile za glasi na makopo).
Ukishapita sehemu ya ukaguzi (nyuma ya turnstiles), unaelekea kwenye korido pana sana ambalo huzunguka uwanja mzima.
Upande mmoja wa korido kuna vyumba/vibanda vya biashara (migahawa, baa, vinywaji na huduma ya kwanza) na upande wa pili kuna vyoo, vyumba vya stoo na ofisi ndogondogo za walizi na biashara). Vyoo vimepakana na majukwaa ya kukaa watazamaji. Kila block moja uwanjani ina vyoo vya jinsia moja.
Katikati ya korido hilo pana kuna vimeza vidogo kwa ajili ya kuweka viungo vya vyakula mfano sukari, chumvi, pilipili, maziwa, kahawa n.k. ambavyo vinakuwa ktk vimifuko vidogovidogo vya karatasi -ni ruksa kujichukulia kadri upendavyo!
Baada ya vyoo, kuna lango jingine linaitwa Block. Napo kuna wasaidizi wa kuhakikisha mtazamaji anafika ktk siti yake. Panahitaji wasaidizi kutokana na mfumo wa uwanja. Imeshatokea mara nyingi mtu anafika uwanjani kushabikia timu moja na anatumia geti sahihi, lakini anaingia Block tofauti na hivyo kukosa siti na kama ana jezi ya timu pinzani, anaweza kupata wakati mgumu anapotangatanga maeneo ya wapinzani wake!
Kama mtu una mpango wa kukaa na mwenzako ktk siti zinazofuatana hakikikisha umekata tiketi yenye geti moja mfano gate F, Block moja (mfano Block 110) na Row moja Mfano Row 29 na siti zinazofuatana mfano seat no. 22 na 23. Unaweza kupata geti moja, block moja, na siti moja ila Row tofauti kwa hiyo hamtakaa pamoja! Au mnaweza kupata geti moja (mfano Geti F) ila Blocks tofauti bila kujua - (mfano Blocks 110 na 112), na mkapata Row na siti sawa kabisa -hamtakaa pamoja! Iko hivi: mmoja atapata tiketi hii - Gate F Block 110 Row 34 Seat 17 na mwingine hii - Gate F Block 112 Row 34 seat 18 (Hapo hamuonani ndugu!). Kwa hiyo ni muhimu kuwa makini wakati wa 'booking' au unaponunua tiketi ya watu wawili au ya kundi la watu wanaofahamiana. Ebu fikiria mke au mme wako mkapotezana siti, itakuwaje!
Sababu kubwa ya kuingia mapema uwanjani ni kwa ajili ya biashara inayoendeshwa na wenye uwanja (Wembley). Maana watazamaji wakiingia mapema watanunua vyakula, vinywaji, program za mechi n.k. na hivyo kuingiza fedha zaidi kwa wenye uwanja mbali na kiingilio ulicholipa. Pia wakati wa mapumziko watazamaji hupata fursa ya mwisho kununua wakitakacho uwanjani maana baada ya mapumziko huduma hizo hufungwa. (Ila kwa mechi zilizoandaliwa na UEFA, ni marufuku pombe kuuzwa. Mfano wakati wa mechi za Euro, Champions League au UEFA Cup final, pombe hairuhusiwi. Ila kwa kesho pombe ni ruksa kwa vile waandaaji ni FA ya Uingereza). Ni marufuku kuvuta sigara maeneo yote ya ndani ya Uwanja, na ukishaingia ndani ya geti hakuna kutoka mpaka kipenga cha mwisho au labda ukitoka hakuna kuingia tena ndani.
Hiyo ndio Wembley, na kwa vyovyote vile mechi ya kesho itakuwa ya kukata na shoka!
Saturday, 28 February 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment