Monday, 16 July 2007

President Kikwete Shows the way .....!*

Watanzania tunyanyuke tupime ukimwi, tusiogope
Jana Serikali ilizindua rasmi kampeni ya upimaji wa virusi vya ukimwi kwa hiari nchini kote, kwa kauli mbiu `Tanzania bila ukimwi inawezekana, kapime`. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma ndio walioongoza Watanzania kupima virusi hivyo katika uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam jana.
Ni kampeni iliyoonyesha kuungwa mkono na wafadhili yakiwemo mashirika ya kimataifa yaliyopo nchini, mabalozi, asasi na taasisi mbalimbali zilizojikita katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi na viongozi mbalimbali wa dini na wa kisiasa.
Hii ni bahati ya kipekee ambayo Watanzania tumeipata ambapo serikali yetu imelivalia njuga suala la watu kupima afya ili kujua mustakali wa maisha yao. Moyo wa kufanya hivyo umeongezwa chachu na Rais wetu, ambaye ameonyesha mfano kuwaondoa hofu wananchi kupima ili kujua usalama wa afya zao. Kutokana na uwazi huo, hakuna sababu ya kuchelewa, sote tunyanyuke twende kwenye vituo vya upimaji ili kujua kama tumeathirika au la ili tuweze kupanga mustakabali wa maisha yetu. Hakuna sababu ya kuogopa kwani Rais Kikwete amelihakikishia taifa kuwa vifaa vya upimaji pamoja na dawa za kurefusha maisha zipo za kutosha. Amesema kuwa shabaha ya kampeni hiyo ni kufikia watu milioni 4, lakini akaongeza kuwa hata kama ni watu milioni 10 uwezo wa kuwahudumia upo. ``Kupima ndio njia ya kutambua afya yako...ukijua mapema, utaishi kwani kujua tatizo ni nusu ya jawabu``, alisema Rais. Kama alivyosisitiza Rais Kikwete, sote tuko vitani hivyo kila mmoja wetu hana budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari. Hata wageni waalikwa waliopewa fursa ya kuzungumza jana walikuwa na lugha na kauli moja kwamba upimaji ndio njia sahihi ya kutambua kama umeathiriwa na gonjwa hilo au la. Balozi wa Marekani, Ujerumani na Japan wameeleza jinsi nchi zao zilivyo bega kwa bega katika mapambano dhidi ya gonjwa hilo nchini. Nchi hizi na nyinginezo zimekuwa zikitoa misaada ya hali na mali katika sekta ya afya kupitia asasi zake kwa lengo la kuiunga mkono serikali kukabiliana na janga hilo. Jitihada hizi zipewe msukumo kwa wananchi kuitikia wito wa kila mmoja kwenda kupima ili kujua usalama wa afya zao kuhusiana na ugonjwa hatari wa ukimwi. Wengi wamekuwa waoga kwenda kupima kutokana na kutokuwepo usiri wakati wa matokeo. Hili wizara ya Afya imeliona na imewahakikishia wananchi kuwa watapimwa kwa namba na kupewa majibu kwa namba hizo. Ni matumaini yetu kwamba wananchi wote watajitokeza vituoni kujua afya zao kuanzia baba, mama na watoto. Hakika, kujua mapema afya yako kutakupa nguvu na ari mpya ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo. Tunyanyuke twende vituoni tukapime kwani linalowezekana sasa lisingoje kesho.
SOURCE: Nipashe (Jumatatu, 2007-07-15 11:24:33 Na Mhariri -Nipashe).

Vijana ‘wajitosa’ kupima ukimwi
-Wajaa kwenye misururu
-Walalama upimaji kuchukua muda mrefu
VITUO vya upimaji virusi vya ukimwi kwa hiari vimeendelea kufurika jijini Dar es Salaam, kundi la vijana likiwa linaongoza.Hata hivyo, baadhi wamelalamika kutumia muda mwingi katika misururu mirefu ya kwenda kupima. Upimaji virusi vya ukimwi kwa hiari ulizinduliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete, ambapo umati ulijitokeza kuitikia wito wa ‘Tanzania bila ukimwi inawezekana, kapime’.Vijana katika vituo mbalimbali jana walikuwa kwenye misururu wakisubiri kupima, majibu na wengine kupata ushauri.Katika kituo cha Karume kilichopo wilayani Ilala, Sultan Nassor (20), alisema ameamua kujitokeza kupima ili aweze kujua afya yake.“Walijitokeza wengi, lakini wengine wameondoka kwa sababu ya kukaa kituoni muda mrefu. Mimi nimekaa hapa tangu saa 4: 00 asubuhi hadi saa 7: 00, bado sijapima,” alisema.Naye Hussein Zuia (21), aliomba upimaji usiwe wa muda mrefu, ili kuwafanya watu wasichukue uamuzi wa kundoka.Muhudumu wa afya katika kituo hicho, ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa vile si msemaji, alisema watu wamejitokeza kwa wingi, na wamelazimika kuwahamishia wengine kwenye vituo vya jirani.Katika kituo cha afya Magomeni, William Nyarata (35), alisema ameamua kujitokeza kupima ili aweze kuwa makini au kupata ushauri ambao utamwezesha kuishi kwa muda mrefu.Nyarata alisema alisubiri kwa saa mbili ili kupata huduma.“Kwa upande wangu sioni tatizo kusubiri muda mrefu, kwani wako sahihi kuweza kumwelewa mpimwaji kwa undani,” alisema Nyarata.Katika kituo kilichopo hospitali ya Temeke, vijana walijitokeza kwa wingi, ingawa idadi ya jumla ya walioitikia wito wa kupima kwa hiari haikuwa kubwa sawa na vituo vingine.Wakati huo huo, taasisi isiyo ya kiserikali ya Rahman Social Development Network (RSDN) imeandaa kampeni ya kuhamasisha, kuelimisha na kuhusisha jamii ya Kiislamu katika mapambano dhidi ya ukimwi.Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Othman Ntarru alisema kampeni hiyo itakuwa ya nchi nzima ili kuunga mkono mpango wa upimaji kwa hiari.Alisema uzinduzi wa kampeni hiyo utafanyika Julai 28, mwaka huu.Ntarru alisema itatanguliwa na kongamano la siku mbili litakalofanyika Julai 16 na 17, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee. Litafunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro.
Source: Uhuru, NA MAGRETH KINABO.


*It is very interesting to see the President pioneering this campaign, but it is more interesting, to me, to see my own wife in the front run!!! Last weekend, my wife was among the supporters of the campaign as she participated in the exercise.
I fully support her. Together we can beat AIDS!

No comments: