Tuesday, 3 July 2007

Madiwani*

Madiwani kuzoa posho nono

Posho za madiwani zilizokuwa zimeongezwa kwa asilimia 100 zimeongezwa zaidi kutokana na maombi ya wabunge. Posho hizo awali zilikuwa zimeongezwa kutoka Sh. 30,000 hadi 60,000 na wakati wa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi ya Waziri mkuu na Ofisi ya Bunge katika kipindi cha mwaka 2007 na 2008 iliyotolewa bungeni wiki iliyopita.
Akihitimisha mjadala wa hotuba hiyo, Waziri Mkuu, Mhe. Edward Lowassa, amesema Serikali imeridhia kuboresha maslahi ya madiwani hao na kusisitiza kuwa posho hizo zitatokana na mapato yatokanayo na vyanzo vinavyokusanywa na halmashauri zenyewe.
Amesema kwa sasa madiwani hao watapata posho ya mwezi Sh. 60,000, posho ya kikao sh. 40,000, posho ya madaraka kwa wenyeviti wa kamati Sh. 40,000 kwa mwezi na posho ya madaraka kwa Mwenyekiti na Meya wa Halmashauri kati ya 100,000-350,000 kwa mwezi kulingana na uwezo wa halmashauri.
`Serikali inaangalia uwezekano wa kulipa kiinua mgongo kwa asilimia 25 ya posho ya mwezi ya diwani kwa kipindi alichotumikia, na pia suala la matibabu, huduma za mazishi na unafuu wa kodi pale watakaponunua usafiri kwa mfano pikipiki maelezo yatatolewa na halmashauri pale taratibu zitakapokuwa zimekamilika,` akasema.
Aidha amesema serikali inaangalia na kuchambua vyanzo vya mapato vya serikali kuu kwa madhumuni ya kuziongezea halmashauri vyanzo zaidi ili viweze kutoa huduma bora na kudumu gharama za uendeshaji.

*(source: Nipashe, 03/7/2007 imeandikwa na Ussu-Emma Sindila, Dodoma)

No comments: