Tuesday, 31 July 2007

MHE. BENJAMIN MKAPA:Ushupavu wa Uongozi (The Courage of Leadership)

HOTUBA YA MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE MKUTANO WA HALMASHAURI KUU YA CCM, DODOMA, 25 AGOSTI 2004


Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara),
Mhe. John Samwel Malecela, Mb.;
Rais na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Mzee Ali Hassan Mwinyi;
Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu,
Mhe. Dkt. Salmin Amour;
Katibu Mkuu wa CCM,
Mhe. Philip Mangula;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu;
Mabibi na Mabwana:

Karibuni nyote tena kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi.
Leo nimeamua kutoa hotuba, tena iliyoandikwa, maana jambo nitakalo kulizungumza ni zito na nimelitafakari kwa muda sasa. Napenda kuzungumza nanyi kuhusu Ushupavu wa Uongozi, kwa Kiingereza: “The Courage of Leadership.”
Nafanya hivyo kwa vile tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani, uchaguzi ambao tuna kila sababu ya kuamini kuwa utaendeleza Awamu ya Sita ya Uongozi Zanzibar, na utaanzisha Awamu ya Nne ya Uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Chama Cha Mapinduzi. Na ningependa tujiandae vizuri kifikra, kimaadili, kiutawala, na kwa kujikumbusha kanuni na taratibu zetu zote.
Napenda leo tujiulize swali la msingi kabisa: Sisi Chama Cha Mapinduzi tunataka uongozi; vema, lakini je Chama chetu kinao ushupavu wa uongozi unaohitajika katika mazingira ya Karne ya 21? Wagombea wetu watarajiwa nao je?
Waheshimiwa Wajumbe:
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi imeorodhesha malengo na madhumuni ya CCM, na mwanzo kabisa kwenye orodha hiyo ni:

“Kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.”

Na zipo njia mbili kubwa za mtu kushinda uchaguzi. Moja ni kuhakikisha unakuwa mgombea wa chama chenye nguvu na mvuto, kama ilivyo CCM hivi sasa. Maana yake ni kuwa hata wewe mgombea ungekuwa hovyo kiasi gani, utabebwa na chama, na utachaguliwa kuwa diwani, mbunge au rais, kwa sababu tu ya chama. Njia nyingine na ya pili ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi wampigie kura, sio chini ya kivuli cha chama chake. Napenda leo tujikumbushe kuwa yote haya mawili ni muhimu: Chama imara, chenye ushupavu wa uongozi; na wagombea imara, wenye sifa, uwezo na ushupavu. Na kuhakikisha kabisa, yote mawili ni muhimu na ni vema yaambatane.
Napenda tujikumbushe maana upo uwezekano wa wana-CCM kubweteka. Kwa vile tunajua chama chetu kina nguvu na mvuto, hatuweki mkazo mkubwa kwenye kujinoa binafsi. Badala yake tunapigana vikumbo kutafuta kuteuliwa, kwa kuamini ukishateuliwa ndio “umeula”. Na tukishaelekea huko, hakutakuwa na kingine kinachotusukuma ila ubinafsi—ubinafsi wa kusema mimi lazima niendelee, na anayenisogelea ni adui; au ubinafsi wa kusema wewe sasa imetosha, sasa ni zamu yangu. Upo uwezekano pia kuwa tusipokuwa waangalifu, ajenda yetu kuhusu mwakani haitaandaliwa na sisi, katika CCM, bali na wapinzani wetu na vyombo vya habari. Wapinzani wanataka kutuvuruga na kutugonganisha, na wenye magazeti wanataka kuuza na kupata faida. Lakini wajibu wa hatma ya nchi yetu umo mikononi mwa CCM, si mikononi mwa wapinzani wala waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari. Lazima tuuchukulie wajibu huo kwa uzito unaostahili, na tujenge ushupavu wa uongozi wa kuutimiza.
Hivi sasa waandishi wa habari na vyama vya upinzani wanatuchokoza tujielekeze kwenye kuzungumzia wagombea wetu kwa uchaguzi wa mwakani. Tusikubali. Tukiwaendekeza, tutajikuta tunatafuta au kuunga mkono wagombea kabla ya wakati, na hivyo kuanza kugawanyika na kudhoofika, badala ya kushirikiana kubuni malengo na dira kwa miaka 5 ijayo. Vyama vya upinzani na vyombo vya habari wanataka tuzungumzie watu, badala ya kuzungumzia kazi muhimu ya chama iliyo mbele yetu. Kama ilivyo mtego wowote, huu pia unavutia, hasa kwa wanaokusudia kugombea uongozi. Tuwe shupavu kuukwepa mtego huu.
Waheshimiwa Wajumbe:
CCM ina nguvu. Lakini nguvu peke yake haitoshi. Nguvu hiyo inapasa kudhihirisha na kuainisha mwelekeo wake. Huu ni wakati wa kujenga ushupavu wa uongozi, ili CCM iandae ajenda na mwelekeo wa taifa, na iongoze taifa—kwa maana ya watu na raslimali—katika karne ya 21 ya utandawazi. Ushupavu huo ndio utasaidia kuhakikisha chipukizi wa CCM nao watakuja kuongoza nchi hii.
Mimi ni muwazi na mkweli: Naamini hivi sasa wananchi wana wasiwasi mkubwa kuhusu hatma ya uongozi wa taifa letu baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani. Wasiwasi huo ni wa kweli, na upo, ingawa wanajua CCM itashinda. Tujiulize kwa nini wana wasiwasi. Wanaona mapungufu gani ambayo sisi viongozi wao ama hatuyaoni, au hatuna ushupavu wa kuyashughulikia?
Nizungukapo mikoani wazee wa CCM hunijia, pamoja na viongozi wengine wa CCM, na hata wananchi wa kawaida, wakinisihi nihakikishe CCM inachagua vizuri wagombea wake katika ngazi zote za uongozi. Wanahofu kuwa pengine hatutakuwa makini vya kutosha, na kwamba pengine CCM italewa nguvu yake na kubweteka. Wangejua tutakuwa makini wasingehofu. Huo ndio ukweli. Na hofu yao inatokana na kujua, kama alivyobainisha Baba wa Taifa, kuwa: “Bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba.”
Pamoja na kelele zote za wapinzani na magazeti, mwananchi wa kawaida anajua kuwa CCM ndiyo mhimili wa taifa hili, na ndiyo bima yake dhidi ya matatizo yanayozikumba nchi nyingine, ikiwemo baadhi ya nchi jirani. Ndio maana hata wapinzani wenyewe wanafuatilia sana afya ya Chama Cha Mapinduzi. Tukipiga chafya sisi, kila mtu anapata homa. Sisi tuna dhamana ya uongozi wa nchi hii, dhamana ya amani, usalama na utulivu wa nchi, na dhamana ya kuongoza vita dhidi ya umaskini. Tujikumbushe kila mara uzito wa dhamana hiyo. Na wale miongoni mwetu tulio Serikalini, tuliokula viapo vya utumishi wetu, tutafakari tena uzito wa viapo hivyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakula viapo vitatu:

· Kiapo cha kwanza ni cha utii, ambapo anaapa kuwa atakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa moyo wake wote, na kwamba ataihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

· Kiapo cha pili ni cha Rais, ambapo anaapa kwamba atatenda kazi zake za Urais kwa uaminifu na kutimiza wajibu wa kazi hizo kwa bidii na moyo mkunjufu, na kwamba atawatendea haki watu wote kwa mujibu wa Sheria, mila na desturi za Tanzania bila woga, upendeleo, huba wala chuki; na,

· Kiapo cha tatu ni cha kudumisha Muungano, ambapo anaapa kwamba ataitetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wao, Mawaziri wanakula viapo viwili. Kiapo cha utii kinachofanana na kile cha Rais, na kiapo cha Waziri ambapo wanaapa kuwa wataitumikia vema na kwa moyo thabiti Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kazi za Uwaziri na kuwa kwa wakati wote watamshauri kwa hekima na uaminifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa kwa vyovyote vile hawatatoa siri za Baraza la Mawaziri.
Waheshimiwa Wajumbe:
Hivi ni viapo vizito. Tunaapa sisi tulio Serikalini, lakini tumetumwa na Chama. Hivyo viapo hivi vinakipa Chama wajibu kuhakikisha waliomo Serikalini wanaishi na kutumikia nchi yetu kwa utimilifu wa viapo hivyo. Wapinzani hawali viapo kama hivi, hivyo wanaweza kupayuka hovyo na kukosa umakini. Hawana wajibu tulionao sisi. Lakini sisi tunaokula viapo hatupaswi kwa vitendo vyetu na kauli zetu kuonekana na sisi ni wapayukaji hovyo na watu wasio makini. Tukionekana au kufikiriwa hivyo, hatutoshi kuongoza!!
Lazima, kwa ushupavu, tuwatoe wananchi hofu, waishi na kufanya kazi zao wakiwa na uhakika kuwa nchi yao imo, na itaendelea kuwa, mikononi mwa viongozi waadilifu, na Chama makini. Tupende tusipende, hofu miongoni mwa raia ni hisia, na hata kielelezo, cha mapungufu ya uongozi. Na hofu hiyo huzidi waonapo watu wanataka kuingia Serikalini kwa uhodari wa ujanja, hila au rushwa, badala ya kutaka kuingia kwa uhodari wa ushupavu wa kutumikia nchi.
Siku moja walikutana marafiki wawili waliokuwa wamepoteana kwa muda mrefu. Mmoja akamuuliza mwenziwe, “Hivi yule kaka yako aliyekuwa anatafuta kazi Serikalini anafanya nini siku hizi?
Rafiki yake akajibu, “Ah, yule hafanyi kitu siku hizi. Alipata ile kazi ya Serikali aliyokuwa anaitafuta!”
Waheshimiwa Wajumbe:
Iwapo wananchi watapata hisia hizi, au iwapo kwa vitendo vyetu tutawadhihirishia, kuwa tunatafuta uongozi Serikalini ili tusifanye kazi zao, lakini tushibe, watakuwa na hofu kila tunapoelekea kwenye uchaguzi.
Tunahitaji ushupavu wa uongozi. Nikiwaulizeni hapa mmojammoja, nina uhakika wengi watasema kuwa zimeanza kampeni za chinichini huko mikoani na wilayani. Wengine wameniambia wapo wenye mkakati wa kununua wajumbe wa Mikutano Mikuu ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa. Kama ni kweli, ujasiri wa viongozi huko mliko wa kusimamia maadili uko wapi? Kwa nini sisikii viongozi wa CCM wanaokerwa na hali hiyo wakiikemea katika vikao vya ndani? Kwa nini taarifa za namna hiyo haziji rasmi, kwa taratibu zetu, lakini zinakuja kwa njia ya tuhuma, minong’ono na kupakana matope? Waasisi wetu wasingekuwa jasiri na shupavu tusingepata uhuru, wala kufanikisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar. Ujasiri na ushupavu wetu sisi, tunaodai haki ya urithi wa waasisi wetu, uko wapi?
Ninyi ndiyo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Na mojawapo ya kazi za Halmashauri hii ni “Kudumisha uangalizi juu ya vitendo vya Wanachama na Viongozi wa CCM na endapo itadhihirika kwamba tabia na mwenendo wa Mwanachama fulani vinamwondolea sifa za uanachama au uongozi itakuwa na uwezo wa kumwachisha au kumfukuza uanachama au uongozi alio nao…” (Katiba ya CCM, 77(8)). Haya ni madaraka makubwa, lakini sioni ushupavu wa kuyatumia katika ngazi zote za uongozi wa Chama. Badala yake ni malalamiko ya chini kwa chini. Hiyo ni hatari kubwa kwa Chama, na kwa Taifa.
Nasema ninyi ndio Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi. Hatma ya CCM na Taifa letu imo mikononi mwenu. Jiulizeni: Kama kweli hiyo minong’ono ni ya kweli, hivyo ndivyo mnavyotaka iwe? Ndio mustakabali wa Chama chetu mnaoutaka—kwamba maslahi binafsi yawe na nguvu kuliko maslahi ya CCM na Taifa? Kama sivyo, ujasiri wenu wa kusimamia maadili na haki uko wapi? Nitauliza maswali mengi leo.
Kwa asili yetu, huko tulikotoka, kulikuwa hakuna fedheha kama ile ya mwanachama kujulikana kuwa eti amenunuliwa. Tuliona kununuliwa ni sawa na utumwa, ni sawa na kuuza utu wako. Maana, huamui tena kwa akili aliyokupa Mwenyezi Mungu, bali kwa kutumwa na aliyekununua. Utakuta mtu na akili yake anatetea ambacho hakiwezekani kutetea. Tutastahilije kuongoza nchi katika mazingira hayo? Mtu mzima una macho, lakini unakuwa huoni kwa kupofushwa na fedha; una masikio lakini husikii kwa vile masikio yako yamezibwa na ahadi za vyeo. Kisha unapojiangalia kwenye kioo, unamwona nani: unaona kiongozi, au unaona kibaraka?
Nasema sisi katika Halmashauri Kuu ya Taifa, wenye jukumu la kusimamia maadili, lazima tuwe mfano wa kufuata maadili, mfano wa kuheshimu Katiba; mfano wa kuheshimu haki za kila mwanachama. Agombeaye nafasi si adui. Na tusisahau kuwa sifa moja ya kiongozi iliyo ndani ya Katiba ni kuwa, “Awe ni mtu aliyetosheka, na asiwe mtu aliyetawaliwa na tamaa.” (Katiba ya CCM, (17(1)). Aliyetawaliwa na tamaa yuko radhi kuhujumu haki za wengine kugombea, yuko radhi kuwazulia kashfa anaowaona ni washindani wake, na yuko radhi hata kuhujumu maslahi ya Chama, ili mradi tu apate anachokitamani. Hatujengi Chama namna hiyo!
Ipo hadithi ya mgombea mmoja kwenye uchaguzi aliyetaka ushauri wa kiongozi wake wa chama kabla ya kampeni kuanza.

Mgombea: “Nadhani jambo muhimu kwenye kampeni hii ni mimi kuelezea na kusimama kwenye rekodi yangu.”

Kiongozi wa chama: “Hapana. Jambo muhimu ni wewe kukanyaga na kupondaponda rekodi ya mpinzani wako.”

Sasa, pengine mbinu hiyo inafaa kwa wapinzani kutoka vyama tofauti. Lakini inawapa wananchi mashaka pale inapotumika miongoni mwa wagombea kutoka chama kimoja. Wana-CCM tuiepuke! Tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, tahadhari ni kwamba adui wa CCM anaweza kuwa yupo miongoni mwetu. Kikulacho kinguoni mwako. Hakuna wapinzani wenye nguvu ya kutudhoofisha. Tukidhoofu, tumejidhoofisha wenyewe, na hasa kwa kuendekeza ubinafsi.
Hivi Mbunge au Diwani ambaye haoni lolote jema lililofanywa na Serikali ya CCM anafanya nini ndani ya CCM? Na atajinadi vipi kwa rekodi ya utekelezaji wa sera za CCM? Nchi hii imepata sifa kubwa kwa kazi zilizofanywa na Serikali ya CCM, halafu Diwani au Mbunge wa CCM anasema hakuna kilichofanyika. Nauliza tena. Anafanya nini ndani ya CCM? Ana tofauti gani na wapinzani? Mwalimu Nyerere alituonya tuhakikishe CCM haiwi dodoki linalonyonya maji masafi na maji machafu sawia. Ushupavu wa NEC uko wapi?
Waheshimiwa Wajumbe:
Sitaki ieleweke kwamba Wabunge na Madiwani wa CCM hawana haki ya kuikosoa Serikali. Wanayo haki hiyo. Lakini, kuna tofauti ya kukosoa utekelezaji wa sera, ambao ni wajibu wa Wabunge na Madiwani wa Chama Tawala; na kukosoa sera yenyewe, ambao ni wajibu wa Wabunge na Madiwani wa Upinzani. Katiba na busara zinataka tupambanue wapi na lini tukosoe sera na utekelezaji wake. Mbunge na Diwani lazima aamue yuko upande gani.
Na hata ukosoaji wa utekelezaji sera lazima nao uwe wa staha, wa kujenga heshima na kuimarisha umoja, si ukosoaji wa kudhalilisha, kubomoa na kukomoa. Nitatoa mfano. Hivi Mbunge au Diwani anaposema madarasa ya MMEM hayafai kabisa, maana yake ni nini. Kwanza, kauli hiyo si ya kweli kwa ujumla wake. Maana mimi nimezunguka nchi hii kuliko wengi wenu. Nimeona madarasa ya MMEM vijijini ambayo ni mazuri kuliko baadhi ya yaliyopo mijini. Nimezungumza na wahisani wetu ambao wamekiri hivyo. Nimepokea barua za pongezi kutoka kwao.
Ni kweli kuna maeneo machache ambapo ujenzi wa madarasa hayo haukuwa mzuri. Lakini, tatizo si sera, wala MMEM yenyewe, wala Waziri mhusika. Tatizo ni uongozi wa eneo linalohusika; na Mbunge au Diwani ni sehemu ya uongozi huo. Kashfa ambayo Mbunge au Diwani anafikiri anaizua, anajizulia yeye mwenyewe kwanza. Iweje maeneo ya Wabunge au Madiwani wengine yawe na madarasa ya MMEM mazuri yanayosifiwa mpaka Washington, na ya kwake yeye ndiyo yawe mabaya? Kulalamika Bungeni au kwenye Halmashauri, badala ya kuongoza kusahihisha makosa, ni mapungufu ya ujasiri wa uongozi.
Nasema, tunahitaji ushupavu wa kuongoza. Ushupavu huo si hotuba nzuri Bungeni au kwenye Halmashauri; ni ushupavu wa kukaa na wananchi na kuwaongoza. Penye makosa ni kusaidia kusahihisha, si kugeuka mwangwi wa kuchafua rekodi ya Serikali ya CCM. Fedha za Serikali zinaliwa kwenye jimbo la Mbunge, lakini anakuja kupigia kelele Bungeni. Anaogopa kusemea kwenye jimbo lake kwa kukosa ujasiri. Hayo nayo ni mapungufu ya ushupavu wa uongozi. Halmashauri au Bunge la watu wenye haraka ya maendeleo ni mahali pa kubadilishana uzoefu wa uhamasishaji na uchangiaji maendeleo huko Wabunge na Madiwani wanakotoka, kila mmoja akieleza aliyoyafanya yeye kwenye jimbo lake, au kata yake, kusudi wengine wamuige. Tusigeuze Bunge, Baraza la Wawakilishi na Halmashauri kuwa mahali pa kumlaumu kila mtu isipokuwa wewe mwenyewe. Narudia. Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ina wajibu kusimamia nidhamu ya Chama. Bila nidhamu, punde si punde hatutakuwa na Chama.
Waheshimiwa Wajumbe:
Nchi rafiki, wahisani na mashirika ya kimataifa nao wamenieleza hofu yao. Wawekezaji wamenieleza hofu yao. Wanataka uhakika wa kitakachotokea baada ya uchaguzi mwakani. Na kwa nchi maskini na tegemezi kama yetu, ambapo asilimia 42 ya bajeti yetu bado inawategemea wahisani, hatuwezi kupuuza hofu yao. Kwa nchi ambayo fursa za ajira na mapato ya Serikali hutegemea zaidi na zaidi uwekezaji wa sekta binafsi, hatuwezi kupuuza hofu ya wawekezaji.
Si kwamba wana husuda tu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu; wengi wao ni watu makini wanaotaka uhakika kuwa yale ambayo sisi na wao tumekubaliana kuwa ni mema na ya maslahi kwa nchi yetu yatadumishwa; na yale ambayo si mema na hayana maslahi kwetu, ambayo tumeanza kuyashughulikia, kuyafuta au kuyakomesha, yataendelea kushughulikiwa. Wao pia wanajua CCM itashinda mwakani, lakini bado wana wasiwasi. Kwa nini? Kwa kazi kubwa ya mageuzi na kukuza uchumi tuliyoshirikiana nao kuifanya, wangependa Tanzania ipige hatua mbele kwa kasi, si kuanza kubabaika, kusuasua, au kurudi nyuma. Kila mara ninarudia kuwaambia wahisani na wawekezaji kuwa mageuzi haya si yangu mimi binafsi, na kwamba ninaongoza utekelezaji tu wa Mwelekeo, Sera na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Lakini bado wana hofu. Najiuliza, kwa nini? Nanyi nataka mjiulize: Kwa nini, na kwamba mtazamo huo unaashiria nini?
Waheshimiwa Wajumbe:
Leo napenda, kwa unyenyekevu kabisa, nikupeni tathmini yangu kwa nini wananchi wanahofu, kwa nini wanachama wenzetu wanahofu, na kwa nini wahisani na wawekezaji wanahofu. Kwa tathmini yangu binafsi, hofu yao inatokana na mambo mawili ya msingi yanayoashiria mapungufu ya ushupavu wa CCM katika kuongoza nchi yetu kwa kuzingatia mahitaji, na mazingira halisi, ya dunia ya leo na ijayo.
Kwanza, wanashuhudia utekelezaji wa baadhi ya mambo yaliyo katika Ilani yetu, na Mwelekeo wa Sera za CCM, ukichelewa au kusuasua kwa upinzani wa baadhi ya wenzetu katika CCM, au kwa kukosa umakini miongoni mwa baadhi ya wenzetu tuliowakabidhi kazi ya kusimamia utekelezaji. Mara kadhaa wamesikia kuwa imebidi mimi mwenyewe kukutana na Wabunge wa CCM kuwakumbusha kwamba Serikali inachotaka kukifanya ni utekelezaji wa Sera za CCM. Mara kadhaa inabidi tufanye semina za Chama katika ngazi mbalimbali kuelimishana na kukumbushana sera hizo. Sera zetu zinapopingwa kidogo na wapinzani wetu au vyombo vya habari, au Asasi Zisizokuwa za Serikali, ambao wengi wao hawaitakii CCM mema, baadhi ya wenzetu wanaanza kuyumba. Hofu ya wahisani na wawekezaji inatokana na mapungufu ya ushupavu wa CCM kutetea sera zake yenyewe, hata pale ambapo mafanikio yake yanaonekana wazi. Wanasikia kauli tofauti kutoka ndani ya CCM. Njia pekee ya kuondoa hofu hiyo ni kurejesha umoja, mshikamano na ushupavu wa uongozi wa taifa letu ndani ya CCM.
Chanzo cha pili cha hofu yao, kwa tathmini yangu, ni kuwa kwa miezi kadhaa sasa wanaona sisi wenyewe kwenye Chama Cha Mapinduzi tukitaka kutoana roho kwa kujiweka vizuri kwa Uchaguzi Mkuu mwakani. Kama nilivyosema, baadhi ya madiwani waliopo wanafanya kila mbinu wasitokee wengine kuwania nafasi zao. Baadhi ya wabunge waliopo wanafanya kila mkakati kulinda wanachokiona kama vile ni himaya yao. Sisemi wanaotarajiwa au kushabikiwa kujipanga kuwania Urais!!
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kugombea au kutetea nafasi za uongozi ni haki ya kila mwanachama. Tatizo langu si hilo. Tatizo langu ni kuwa wakati bado. Kama nilivyosema awali, tatizo langu ni pale tunapogombea nafasi kabla ya kukubaliana hao tutakaowapendekeza kugombea watakwenda kufanya nini. Hivyo naomba tuache kwanza kuzungumzia, na pengine hata kuchukiana na kuhujumiana, juu ya majina ya wagombea.
Tusitangulize mkokoteni kabla ya farasi. Tusiwe kama wapinzani. Sisi tuzungumze kwanza kuhusu programu na Ilani ya CCM kwa miaka 5 ijayo. Tuzungumze mambo ya maslahi kwa wananchi na taifa badala ya yale ya maslahi ya wagombea na wapambe wao. Tuzungumze kukuza uchumi wa kisasa katika mazingira ya utandawazi. Tutafakari changamoto zilizopo na zijazo, na kisha ndipo tuone nani kati ya makada wetu wanaweza, na wanatosha, kuaminiwa kukabidhiwa usimamizi wa utekelezaji wake.
Mambo hayo yatatutofautisha na wapinzani na ndiyo yatatupa vigezo vya kisayansi vya kujua nani miongoni mwetu anafaa kwa uongozi, kwenye ngazi ipi, kwa malengo gani. Tutapata pia vigezo vya kupima utendaji wa tutakaowachagua. Kama tunataka kujenga ushupavu wa uongozi lazima tuanze hivi. Kazi ijulikane kwanza; majina ya watakaosimamia kazi hiyo yaje baadaye.
Maana CCM inayo hazina kubwa ya wanaofaa kuwa madiwani, wabunge, na marais. Chama kimoja cha siasa kiliitisha mkutano wa kura za maoni kupata mgombea wa chama hicho. Mmoja kati ya ambao hawakushinda akalalamika, “Mimi nilisikia kabisa sauti za wananchi wakinitaka nigombee!”
Rafiki yake akamfariji, “Usijali rafiki yangu. Pengine sauti hiyo ilikuwa yako mwenyewe ukiwaza kwa sauti.”
Waheshimiwa Wajumbe:
Ipo tofauti kubwa kati ya Chama kuwa na nguvu, na Chama kuwa shupavu. Nguvu ya CCM leo ni ya kihistoria; ni ya huko tulikotoka kwa waasisi wetu, na mazingira tofauti ya wakati huo. Na nguvu hiyo imeegemea sana kwenye heshima ya waasisi hao. Tuelekeako, nguvu ya CCM itategemea zaidi ushupavu wa uongozi wa leo na wa kesho, na hasa katika kusimamia maadili ya utendaji katika mazingira tofauti kabisa kitaifa, kikanda na kimataifa. Ushupavu wa uongozi una sifa nne kuu: Kwanza ni upeo mkubwa wa kubuni malengo na dira; Pili, ni uongozi madhubuti wa watu na raslimali kuelekea kwenye malengo hayo na kuzingatia dira hiyo; Tatu, baada ya kuridhia malengo, ni ung’ang’anizi na kukataa kuyumbishwa bila sababu za msingi; na Nne ni ujasiri wa kusimamia na kutetea maadili. Maana kwa hakika, asiye na maadili hawezi kuwa shupavu.
Kuongoza ni kupanga kwanza. Mipango mizuri huleta maamuzi mazuri kimkakati na kiutendaji. Chama Cha Mapinduzi kinapaswa kuongoza kwa kupanga; ili iwe rahisi kwa Serikali yake kutekeleza. Uzoefu wangu wa kuongoza Chama hiki na Serikali yake ni kuwa Chama kimeiachia Serikali madaraka ya kupanga, lakini wakati wa maamuzi ya mkakati na utendaji, kama nilivyosema, wanatokea viongozi wa Chama, wakiwamo Wabunge na Madiwani wanaochelewesha maamuzi, hata pale ambapo msingi wa maamuzi hayo ni sera za Chama.
Waheshimiwa Wajumbe:
Chama Cha Mapinduzi ndicho hasa kiongozi wa nchi hii. Au tuseme hivyo ndivyo inavyopasa kuwa. Chama kwanza, mtu baadaye. Ndiyo maana huko nyuma tukasema, “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Nami leo naongeza: Chama shupavu, huzaa viongozi shupavu.
Mtaalamu mmoja wa menejimenti alisema: “Wajibu wa kwanza wa kiongozi ni kuwafafanulia anaowaongoza hali halisi.” Kama Chama Cha Mapinduzi kinataka kuendeleza sifa zake za uongozi, na nguvu yake katika siku za usoni, lazima kiwe chama shupavu, chama kisichoogopa kusimamia maadili yake, chama kisichoogopa kusema ukweli, chama cha kuwafafanulia wananchi hali halisi ya tulipo, na mahitaji na masharti ya mafanikio ya huko tuendako.
Waheshimiwa Wajumbe:
Ninakusudia mwishoni mwa mkutano wetu huu kutangaza timu ya kuandaa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2005, na kuwataka kuikamilisha kabla hatujafikia kipindi cha kuteua wagombea. Kama nilivyosema, hii ina faida mbili. Kwanza Ilani hiyo ndiyo itamwezesha anayetaka kugombea aitafakari vizuri na kujishauri yeye mwenyewe iwapo anaona anazo sifa na nia thabiti ya kutekeleza Ilani hiyo, akijua sisi wengine tutamtarajia afanye hivyo kwa niaba ya Chama. Pili, Ilani hiyo, na majukumu itakayokuwa imeyaainisha, itatuwezesha sisi kwenye Chama kubaini ni kada gani miongoni mwetu anafaa kugombea wadhifa gani, kwa malengo na sababu gani, na kwa kipindi gani. Maana, hatimaye, katika kuamua nani awe mgombea wetu wa Udiwani, Ubunge na Urais, kigezo cha msingi ni uwezo wa kutekeleza sera na malengo ya Chama. Uhodari binafsi wa kampeni si sifa ya msingi, maana jukumu la kampeni kimsingi ni la Chama, si la mgombea binafsi.
Naomba sana tujifunze kwa marafiki zetu wa siku nyingi, Wachina. Hapana shaka kuwa kiongozi hasa wa China ni Chama cha Kikomunisti cha China. Chama hicho kina uwezo mkubwa na ushupavu wa kupanga na kusimamia mwelekeo, si wa Chama tu, bali wa nchi nzima. Kila awamu ya uongozi nchini China inapangiwa majukumu ya msingi (Central Tasks), tena yanapangwa mapema kabisa, na yanapangwa na Chama, hayapangwi na Serikali. Kisha kila awamu inapatiwa viongozi wanaolingana na kushabihiana na mahitaji ya majukumu hayo ya msingi. Hivi leo, tayari wanajua majukumu ya miaka 20 – 25 ijayo, na tayari wanaandaa viongozi wa kuyasimamia majukumu hayo. Huo ndio ushupavu wa uongozi ninaouzungumzia.
Uongozi shupavu hauogopi kubadili mkakati iwapo ni lazima kufanya hivyo. Leo China ina uchumi wa soko unaoshindana, na kwa kweli unaowatoa jasho, wakongwe wa uchumi wa soko kwenye nchi za Magharibi. Leo China, kwa uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, imeweka ndani ya Katiba yao haki ya kumiliki mali na raslimali binafsi. Nani angeamini, miaka 10 tu iliyopita, kuwa China ingefanya hivyo? Wameweza kwa vile hawaogopi kukubali ukweli kuwa dunia imebadilika; hawaogopi kuwaeleza wananchi wao hivyo; hawaogopi kubuni mipango na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo; hawaogopi kuwaonyesha wananchi wao njia sahihi ya kuinusuru nchi yao, na kuwaongoza katika njia hiyo; na hawaogopi kusimamia maadili ya Chama chao. Wakishakubaliana kwenye Chama wote wanazungumza lugha moja. Ukimsikiliza mmoja ni sawa na umewasikiliza wote.
Sisi hapa tunababaika kwa nini? Wakati mwingine, ungempeleka mgeni kutoka nje ya nchi kwenye Bunge letu, kwenye Baraza la Wawakilishi, au kwenye Mabaraza ya Madiwani, akisikiliza mijadala hawezi kujua anayezungumza ni wa Chama Tawala au anatoka kwenye vyama vya upinzani. Tunapimana uhodari wa ubishi, badala ya uhodari wa kuelezea sera na kuongoza utekelezaji wake kwa makini na ushupavu. Maneno hayajengi nchi. Nchi gani imejengwa kwa uhodari wa maneno? Nchi inajengwa kwa kazi. Tukishaamua sera tunahitaji ujasiri wa kutenda, si wa maneno. Ukiwepo ubishi uwe wa kasi na ubora wa utendaji, si wa sera tena.
Nchi pia haijengwi kwa madai. Maana tunazoea kila mara kuuliza: Serikali ina mpango gani? Serikali inafanya lini jambo hili au lile? Serikali italipa lini mshahara wa kutosha? Na hakuna anayekwambia fedha zitatoka wapi. Hakuna anayejenga hoja kuwa uwezo utoke wapi, au utokane na nani! Na sisi ndio viongozi, lakini hatuna ujasiri wa kulinganisha mapato na matumizi, wala matokeo yake. Uwazi na ukweli, ushupavu na ujasiri.
Haifai viongozi wa Chama hiki wakose ujasiri wa kueleza ukweli wa uwezo mdogo, kama alivyokosa ujasiri bwana mmoja aliyeambiwa na mkewe waende kununua vitu vya sherehe ya mwaka mpya. Alikuwa hana fedha za kutosha, na alikuwa hana ujasiri wa kutosha. Alipofika kazini akamwendea mkubwa wake wa kazi. Akamwambia, “Tafadhali bwana mkubwa, naomba ruhusa niende na mke wangu kununua vitu vya sherehe ya mwaka mpya.”
“Haiwezekani”, akajibu mkubwa wake wa kazi. “Tuna kazi nyingi sana.”
Bwana yule akashusha pumzi, “Nakushukuru sana, bwana mkubwa. Una huruma tele kwa kunikatalia.”
Waheshimiwa Wajumbe:
Wakati wa kuandaa Ilani mpya ni wakati pia wa kufanya tathmini yetu ya ndani ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2000. Mimi nadhani tumefanya vizuri, lakini kufanya vizuri kwa kipindi kilichopita si sifa pekee ya kuaminiwa kuendelea kuongoza nchi. Utekelezaji mzuri wa Ilani ya 2000 ni ushahidi wa usahihi wa sera kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine ni ushahidi kuwa sisi ni waungwana, na kwa kadri ya uwezo wa Serikali tunatekeleza tunayoyaahidi.
Uungwana huo ni sifa nzuri, lakini tutakachowaahidi wananchi kwa miaka 5 ijayo nacho ni muhimu, tena pengine ni muhimu zaidi. Yaliyopita yamepita; japo ni mema, wananchi watakuwa wanaangalia yajayo. Lazima tujiandae vizuri kuelezea tuliyoyafanya, na yale tunayoahidi kuwa tutayafanya. Hata kama awamu ya sasa italala salama, wananchi watatahayari: wataamka salama na awamu ya taswira gani?
Kwa heshima na unyenyekevu, nathubutu kusema kuwa mwaka 2000, CCM ilipata ushindi mkubwa kuliko mwaka 1995, si kwa sababu ya uhodari wetu wa maneno bali kwa vile wananchi walianza kuelewa usahihi wa sera zetu kutokana na matunda ya utekelezaji yaliyoanza kuonekana. Matunda hayo yameongezeka tangu mwaka 2000. Wananchi wanaona wazi matunda hayo kwenye elimu, afya, maji, miundombinu kama vile barabara, madaraja, vivuko, bandari na simu, kushuka kwa mfumuko wa bei, nyongeza ya mapato ya Serikali, mafao mazuri zaidi ya watendaji wa Serikali, heshima ya taifa na diplomasia yake, misamaha ya madeni, nyongeza ya misaada na uwekezaji. Wanachotaka wananchi ni uhakika kuwa hatutarudi nyuma.
Mambo mawili ni muhimu sana yazingatiwe kwa makini. La kwanza ni kuwa Ilani ijayo itahusu kipindi cha 2005-2010, ambacho ndicho kipindi cha mwisho cha kutekeleza Mwelekeo wa Sera za CCM Katika Miaka ya 2000-2010. Kwa hiyo Ilani lazima iandaliwe kwa kuzingatia ukweli huo. Tupitie tena mwelekeo huo, na kuona yapi yametekelezwa, na yapi yanapaswa kuzingatiwa kwenye kipindi kijacho. Na kwa yale ambayo yametekelezwa tuone ni namna gani tutahakikisha kwamba haturudi nyuma, kwamba tunayaimarisha, na kwamba tunajenga juu ya msingi wa mafanikio ambayo tayari yamepatikana na kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii.
Tufanye hima kukubali pia kuwa dunia yetu inabadilika haraka sana, na kila mabadiliko yanahitaji nasi tujipime tulipo. Tuwe wepesi kutambua maslahi yetu katika mabadiliko hayo, na tuwe wepesi kubuni mikakati ya kutetea maslahi hayo. Tuwe shupavu kama Chama kuwaiga rafiki zetu Wachina. Uchumi wa dunia ya leo ni uchumi wa soko. Ni kujidanganya kufikiri tunaweza kuukwepa.
Ushupavu wa uongozi ni kuwaeleza wananchi ukweli huo, na kutekeleza kwa dhati na makini yale tunayoamua ili kujenga uwezo wetu wa ushindani kibiashara na kiuwekezaji. Leo tunasifiwa kuwa nchi yetu imedhibiti vizuri vigezo vya uchumi mkuu, kama vile mfumuko wa bei na mapato na matumizi ya Serikali. Tunasifiwa kwa kujenga uwezo wa ushindani kibiashara na kiuwekezaji. Tunao uwezo wa kuamua na kuhakikisha haturudi nyuma, na tunalinda sifa hizo.
Waheshimiwa Wajumbe:
Ni kweli Tanzania imepata mafanikio mengi baada ya Serikali kujiondoa kwenye uwekezaji, biashara na huduma za kiuchumi, na kwa kushirikisha zaidi sekta binafsi katika kukuza uchumi, kuongeza nafasi za ajira, kuingiza nchini teknolojia ya kisasa, kutoa huduma za kiuchumi na kijamii, na kuongeza mapato ya Serikali. Napenda niongeze jambo muhimu sana. Tunaondoa mikono ya Serikali kwenye uchumi wa soko, lakini hatuondoi macho ya Serikali. Uchumi wa soko unahitaji sana usimamizi wa Serikali, kwa maana ya mwelekeo wa sera za kiuchumi na kijamii, kuleta ushindani wa haki kwenye soko, na kulinda maslahi ya taifa na wananchi. Aidha, yapo baadhi ya mambo ambayo kwenye hatua yetu ya maendeleo hatuwezi kutegemea sekta binafsi iyafanye, ikiwemo ulinzi na usalama, utawala wa sheria na haki za binadamu, huduma za kijamii, na miundombinu.
Tumeanza katika Awamu ya Tatu, na inabidi tuendelee katika Awamu ya Nne, kuimarisha dola na asasi zake za uongozi na usimamizi wa uchumi wa soko. Usimamizi huo ni pamoja na kuendeleza na kudumisha mambo ya msingi kwa utaifa na umoja wetu, usawa wa fursa za kuishi na kujiendeleza, na mshikamano wa kitaifa na muungano wetu. Nchi hii pia, chini ya uongozi wa CCM, lazima iendeleze dhana ya maendeleo ambayo hayapishani sana. La msingi si kuwarudisha nyuma wanaotajirika kwa njia halali, bali kuwasaidia wanaofukarika kwa kuwahimiza na kuwawezesha kutumia fursa zinazoletwa na uchumi wa soko.
Uchumi wa soko hauwezi kushamiri iwapo wananchi walio wengi si washiriki. Kwa hiyo kazi kubwa iliyo mbele ya Chama chetu ni kubuni na kusimamia mikakati ya kuingiza wananchi wengi iwezekanavyo kwenye uchumi rasmi wa soko. Mkakati mmojawapo, ambao tayari tunaushughulikia, ni wa kutambua rasmi raslimali na biashara za wanyonge ambazo bado ziko kwenye sekta isiyo rasmi ili zitumike kuwafanya wawe washiriki kamili kwenye uchumi rasmi wa taifa.
Jambo la pili muhimu sana ni wajibu wa dola kujenga miundombinu ya kiuchumi na kijamii ambayo bila kuwapo uchumi wa soko hauwezi kushamiri. Tumeanza, na lazima tuendeleze, ujenzi na uimarishaji wa barabara, madaraja, vivuko, reli, bandari, simu na umeme. Lazima tuendeleze maandalizi ya Watanzania kuwa na elimu, ujuzi na afya ya kuwawezesha kushiriki uchumi wa soko. Hivyo miradi ya elimu, maji, afya na vita dhidi ya UKIMWI na Malaria itabidi iendelezwe kwa kasi. Mapato ambayo Serikali inapata kutokana na shughuli za sekta binafsi hayana budi kuelekezwa kwenye kuimarisha uwezo wa Serikali kutimiza wajibu wake huu usiokwepeka.
Waheshimiwa Wajumbe:
Napenda kumalizia kwa kuwakumbusha mambo matatu tuliyoyabainisha kama ndiyo mambo makuu ya kuzingatiwa katika kipindi cha 2000-2010:

· Kwanza, kwamba CCM iwe mhimili wa umoja wa taifa, na wa muungano wetu. Mwelekeo unasema “Ili CCM iendelee kuwa na nguvu ya mhimili wa umoja wa taifa, lazima ihakikishe kuwa sarakani ya udini, ukabila na ubaguzi wa aina nyingine yoyote haijipenyezi ndani ya CCM yenyewe...Wana-CCM wanaoendekeza au kupandikiza ubaguzi ndani ya Chama chetu lazima wafichuliwe au kuchukuliwa hatua”;

· Pili, kwamba CCM idumishe amani na kutoa uongozi kwa taifa. Mwelekeo unasema, “CCM lazima ionekane kuwa ndilo chimbuko la sera za kuwawezesha wananchi kiuchumi.” Mwelekeo unaendelea kusema, “Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ziendeleze msimamo thabiti wa kulinda na kutetea maslahi ya chama dhidi ya maslahi ya ubinafsi; na maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya vikundi vya kibinafsi. Hivi ndivyo CCM itajijengea uhalali wa kuwa chama kiongozi kwa taifa;” na

· Tatu, kwamba CCM iongoze ujenzi wa uchumi wa kisasa na kuutokomeza umaskini. Leo dunia nzima inakiri kuwa vita dhidi ya umaskini haiwezi kufanikiwa bila uchumi kukua. Kwa hiyo jukumu la msingi ni kwanza kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi, na pili kwamba uchumi ukuavyo maslahi ya wanyonge na ya taifa yanazingatiwa. Uwezeshaji wa wananchi, na usimamizi wa uchumi wa soko, ni mambo ambayo yatahitaji mkazo maalum. Mwelekeo unasema, “Kazi hii ni nzito na inahitaji uongozi thabiti wa vitendo wa Chama na Serikali zake. Serikali zitabidi ziyaelewe na kuyaainisha majukumu yake na kuyatafsiri katika programu mbalimbali.”

Waheshimiwa Wajumbe:
Mimi ninaamini kuwa iwapo tutaandaa programu yetu, na Ilani yetu, kwa kuzingatia majukumu haya ya msingi, tutaonekana wazi kustahili kuendelea kukabidhiwa uongozi wa nchi hii. Lakini narudia. Tukubaliane kwanza kuhusu programu na Ilani, kabla ya kutafuta wagombea. Pili, tuazimie kuwa na uongozi shupavu, uongozi usiosuasua, uongozi unaokiri hatua tuliyopiga, usioogopa kubuni, kuongoza na kusimamia mabadiliko. Chama kisicho tayari kubadili mikakati na mbinu kitapoteza uhalali wa uongozi katika dunia inayobadilika, na Chama ambacho si shupavu, hakiwezi kubadilika.
Unaweza kuwa nahodha hodari wa merikebu, lakini huwezi kuwa nahodha wa bahari. Watanzania, Chama Tawala cha CCM na viongozi wake, tusifikiri tunaweza kuwa nahodha wa bahari ya utandawazi inayotuzunguka kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Badala yake, tuboreshe unahodha wetu wa merikebu ya taifa katika bahari iliyotibuka. CCM tuna wajibu kuwa waaminifu, shupavu, kubadilika, na kuongoza na kusimamia mabadiliko, bila kuathiri hata chembe imani yetu ya kisiasa na itikadi inayoambatana nayo. Tunahitaji ushupavu wa uongozi. Tukiamua tulio ndani ya ukumbi huu, inawezekana kujenga ushupavu huo. Ombi langu ni kuwa kila mmoja wetu asikilize dhamira yake na kisha atimize wajibu wake.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

source: http://www.ccmtz.org/

No comments: