Maregesi: Tume ndiyo itaamua hatima yangu
Adai aliisaidia Jumuia ya Wazazi mil. 100/-
Asema anaheshimu maamuzi ya Chama
Na Thomas Mtinge
MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Abiud Maregesi amekiri kuwa amesimamishwa uongozi na kwamba, tume iliyoundwa kumchunguza ndiyo itatoa ukweli.Kukiri kwa Maregesi kumekuja baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti kuwa, yeye na wenzake kadhaa wamesimamishwa uongozi na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwa madai ya ubadhirifu wa fedha za jumuia hiyo zaidi ya sh. milioni 160.Akizungumza kwa njia ya simu jana, Maregesi alisema ni kweli yeye na Kaimu Katibu Mkuu wake Hinju Cosmas wamesimamishwa uongozi.Alisema Kamati Kuu imeunda tume itakayofanya kazi ya kuchunguza tuhuma zinazowakabili. Taarifa ya kusimamishwa kwao uongozi bado haijatolewa rasmi na Chama.Maregesi alisema anaheshimu uamuzi wa Chama na kwamba yeye kwa nafsi yake anaamini hakuna baya alilolifanya kwenye jumuia hiyo, aliyoitumikia kwa kujitolea zaidi.Alidai alipoingia madarakani katika jumuia hiyo aliikuta ina uwezo mdogo wa kifedha na alilazimika kusaidia sh. milioni 100.“Wakati nilipoanza uongozi niliikuta jumuia ikiwa katika hali mbaya kifedha, hivyo nilijitahidi kutoa sh. milioni 100 kwa ajili ya kuisaidia ili iweze kuendesha shughuli zake. Itashangaza leo hii tena nibadilike na kuanza kufuja fedha za jumuia ambayo hali yake si ya kuridhisha kifedha,” alidai Maregesi.Alidai jumuia hiyo aliikuta ikiwa katika hali isiyoridhisha kiuchumi, huku ikikabiliwa na deni kubwa la pango la nyumba inayotumika kwa ajili ya ofisi zake. Jengo hilo linamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), liko karibu na soko kuu la Kariakoo, Dar es Salaam.Maregesi alidai kutokana na hali hiyo, amekuwa akitumia sehemu ya fedha zake kuisaidia jumuia hiyo, ikiwa ni pamoja na kulipia sehemu ya kodi ya pango, ili kuepusha ofisi kufungwa na shirika hilo.Hata hivyo, Maregesi hakutaka kuzungumzia zaidi suala hilo kwa maelezo kwamba anaheshimu maamuzi yaliyotolewa na Kamati Kuu.“Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikinitafuta kwa ajili ya kutaka kujua undani wa sakata la mimi na wenzangu kusimamishwa uongozi kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za shule zinazomilikiwa na Jumuia ya Wazazi.“Kwa sasa sina muda wa kuzungumzia suala hilo kwa sababu lipo katika ngazi ya juu ya CCM... lazima tuheshimu utaratibu uliowekwa mpaka tume iliyoundwa itakapomaliza uchunguzi wake,” alisema Maregesi.Alisema haoni sababu na si jambo la busara kuanza kulizungumzia suala hilo kwa undani kupitia vyombo vya habari, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka maadili ya CCM.Kwa mujibu wa Maregesi, tume hiyo ndiyo itakayobaini ukweli wa tuhuma hizo, na kuongeza kwamba binafsi hakuhusika na ubadhirifu huo kama inavyodaiwa.Katika sakata hilo, Kamati Kuu iliyomaliza kikao chake cha siku mbili mjini Dodoma juzi, ilitoa maamuzi ambayo pamoja na mambo mengine, imewasimamisha uongozi kwa muda usiojulikana Maregesi, Hinju na msaidizi wake aliyefahamika kwa jina moja la Mpemba.
Lowassa apangua tena wakurugenzi
Na Mwandishi Maalum
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa amewahamisha vituo vya kazi wakurugenzi wanane wa halmashauri za wilaya.Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotokewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu, uhamisho huo unatokana na kuanzishwa kwa halmashauri za wilaya mpya na kuteuliwa kwa wakurugenzi wapya.Waliopata uhamisho na vituo vyao vya kazi vya zamani katika mabano ni Theones A. Nyamhanga anayekwenda Babati (akitokea Musoma); Gladys Dyamvunye, Ileje (Mpwapwa) na Halifa H. Hida, Arusha (Mufindi).Wengine ni L.A. Shimwela, Mufindi (Kishapu); Andrew F. Juma, Meatu (Kiteto); Jacob Kayange, Rorya (Tarime); Yona Mlaki, Mpwapwa (Ileje) na Frederick Ntabakanyule, Musoma (Handeni).Uhamisho huo unatokana na kuanzishwa kwa halmashauri za wilaya mpya nane, kubadilisha majina nyingine mbili na kupandisha hadhi Mamlaka za Miji Midogo ya Mpanda na Njombe kuwa Halmashauri za Miji.Halmashauri mpya ni Arusha, Longido, Bahi, Misenyi, Chato, Nanyumbu, Mkinga na Rorya.Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mkuu Lowassa aliwateua wakurugenzi wapya wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.Wakurugenzi wapya waliotangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na vituo vyao vya kazi ni Christian M. Laizer (Longido); Elly Jesse Mlaki (Kishapu); Fortnatus Fwema (Iramba); Hamida Kikwega (Chato) na Lucy L. Msofe (Lushoto).Wengine ni Shaibu Mnunduma (Bukoba); Festo L. Kang’ombe (Kiteto); Mohammed S. Nkya (Nanyumbu); Mariam Mtunguja (Nachingwea); Beatrice Msomisi (Bahi) na Xavier Tilweselekwa (Handeni).Wakurugenzi waliohamishwa na kutangazwa mwishoni mwa wiki iliyopita na vituo vyao vya zamani kwenye mabano ni Dk. Isdor Mtalo, Misenyi (Iramba); Philibert Ngaponda, Mkinga (Babati); na Tarsias B. Kagezi, Tarime (Nachingwea).Katika mabadiliko hayo, Mohammed Gwalima ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino.
Wananchi wanaitaka adhabu ya kifo- Waziri
Na BAKARI MNKONDO, DODOMA
SERIKALI imesema wananchi wengi wamependekeza adhabu ya kifo iendelee, Bunge limeambiwa.Akiwasilisha makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2007/2008, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Mary Nagu alisema utafiti uliofanyika kuhusiana na hoja hiyo umebaini wengi wanataka iendelee.Alisema uratibu wa masuala ya haki za binadamu ulitekelezwa vizuri na serikali ilishughulikia uchunguzi kuhusu kufutwa kwa adhabu ya kifo.“Kufuatia taarifa iliyowasilishwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali katika Tume ya Haki za Binadamu na Watu ya Afrika iliyoko Banjul… mashirika hayo yalitaka tume hiyo itoe tamko dhidi ya adhabu hii,” alisema.Aliongeza kuwa: “Wabunge watakumbuka kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria imefanya utafiti kuhusu hoja hii na wananchi walio wengi walitaka adhabu ya kifo iendelee”.Katika hatua nyingine, serikali inaendelea na juhudi za kuboresha utoaji haki na kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuendeleza mchakato wa kutenganisha shughuli za upelelezi na zile za uendeshaji mashitaka.Dk. Mary alisema polisi na asasi zingine za upelelezi zitaendelea na jukumu la upelelezi tu na Mkurugenzi wa Mashitaka ataendesha mashitaka.“Mawakili 156 na wafanyakazi 27 wa kada nyingine wataajiriwa kwa awamu kufanikisha kazi hii,” alisema na kuongeza kuwa mchakato wa mapendekezo ya kutunga sheria mpya ya kusimamia mfumo wa kuendesha mashitaka umeanza.Kuhusu kesi za rushwa, serikali imesema hadi sasa majalada 19 yameshughulikiwa, ambapo 15 yameonekana kufaa kufunguliwa kesi na manne hayawezi kufunguliwa kesi mahakamani.Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa sh. 69,860,784,800 kwa ajili ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2007/2008.Katika hatua nyingine, Dk. Mary alitangaza bungeni jana kuwa jina halisi la wizara yake ni Wizara ya Katiba na Sheria.Hali hiyo inafuatia kuwepo kwa mkanganyiko wa jina la wizara hiyo, ambapo wengine walikuwa wakiita au kuandika Wizara ya Sheria na Katiba.
NEC yakutana kushughulikia wagombea
Kamati Kuu haikumkemea Makamba
NA JACQUELINE LIANA, DODOMA
HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi inakutana leo na kesho mjini hapa, kushughulikia uteuzi wa wagombea uongozi wa CCM ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Aggrey Mwanri ilisema kikao hicho pia kitajadili hali ya kisiasa ilivyo nchini.Mkutano huo utakaofanyika chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete, unafuatia kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kilichomalizika juzi.Agenda nyingine za kikao cha NEC, zilizotajwa katika taarifa hiyo ni kujadiliwa kwa taarifa ya maendeleo ya maandalizi ya mkutano mkuu wa nane wa taifa wa CCM, utakaofanyika Novemba, mwaka huu.”Pamoja na agenda ya hali ya kisiasa ilivyo nchini, mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya Taifa utashughulikia uteuzi wa wagombea uongozi wa CCM ngazi ya wilaya, mkoa na taifa,” ilisema taarifa hiyo.Kikao hicho cha NEC pia kitapokea na kujadili taarifa ya ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais Amani Abeid Karume aliyoifanya Ujerumani Mei 6 hadi Mei 9, mwaka huu.Pia mkutano utapokea na kujadili taarifa ya mkutano mkuu, kuhusu wajibu na nafasi ya vyama vya siasa katika mchakato wa ushirikiano wa kikanda Afrika, uliofanyika Naivasha, Kenya, mwezi huu.Wakati huo huo, CCM imetoa rai kwa vyombo vya habari kuisaidia jamii kwa kuipatia habari sahihi na zilizothibitishwa kuhusu vikao vya Chama vinavyoendelea.Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Mwanri alisema upatikanaji wa habari sahihi kuhusu yanayojadiliwa na kuamuliwa kwenye vikao hivyo ni jambo muhimu.“CCM ni Chama tawala, kikiwa na dhamana ya kiutawala, takribani Watanzania wote wangependa kujua nini kinajadiliwa na kuamuliwa kwani maamuzi ya kisiasa ya Chama kinachotawala kwa vyovyote vile yatagusa maisha yao. “Hivyo basi upatikanaji wa habari sahihi kuhusu yanayojadiliwa na kuamuliwa kwenye vikao hivyo ni jambo muhimu sana,” ilifafanua taarifa hiyo.Baadhi ya vyombo vya habari, ilisema taarifa hiyo, vimeshatoa habari zinazodaiwa zimejadiliwa au kuamuliwa na vikao, wakati si kweli na si sahihi.“Navishauri vyombo vya habari kutafuta habari za kweli kuhusu CCM kutoka kwenye vyanzo vyenye mamlaka ya kutoa habari za Chama. Subirini habari za kweli zitolewe na wanaohusika kwa utaratibu uliowekwa na Chama, na ambao vyombo vya habari vinaufahamu kwani vimekuwa vikiwasiliana na CCM mara kwa mara kupitia utaratibu huo,” ilisema taarifa.Taarifa hiyo ilitoa mfano kwamba, habari zilizoandikwa na gazeti la Majira kuwa Kamati Kuu imemkemea Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, kwa kutumia lugha nzito katika kuzungumzia mwafaka baina ya CCM na CUF si za kweli.“Si vyema kwa chombo cha habari kuokoteza taarifa, ilhali wasomaji wanakitegemea katika kupata habari sahihi. Kwenda kinyume cha matarajio ya wasomaji ni kujivunjia heshima,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Uhuru, 31/7/2007
Tuesday, 31 July 2007
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment