Mahamama Kuu ya Kazi yawaliza tena walimu
Mahakama Kuu divisheni ya Kazi jijini Dar es Salaam imezuia mgomo wa walimu ambao ulianza jana kwa kishindo ukiwa umeguza mikoa mingi nchini.
Uamuzi wa kuuzuia mgomo huo ulitolewa jana saa 3.49 usiku na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ernest Mwaipopo, baada ya kusikiliza hoja zilizokuwa zimewasilishwa na serikali na Chama cha Walimu (CWT).
Siku nzima ya jana, kesi hiyo iliyofunguliwa na serikali Ijumaa iliyopita kupinga mgomo wa walimu uliotangazwa rasmi na Rais wa CWT, Gratian Mukoba, iliendelea kwa pande zote mbili kuvutana hali iliyoifanya endelee hadi usiku.
Akitoa uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Mwaipopo alisema mahakama imeridhika na hoja za upande wa serikali kwamba utakuwa na athari kubwa kwa watoto wa masikini ambao hawana hatia.
Alisema mgomo huo hauzihusu shule binafsi kwani umeelezwa kwa shule za umma ambazo wanasoma watoto wengi wa watu wa kipato cha chini.
Alisema madhara yatakayosababishwa na mgomo huo kwa wanafunzi hao hayawezi kufidiwa, lakini walimu wanaweza kufidiwa kwa kulipwa fedha zao wanazoidai serikali.
Alizitaka pande zote mbili leo saa saba usiku wawe wame wamewatangazia walimu kusitishwa kwa mgomo huo na atakayekaidi amri hiyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Mara baada ya uamuzi huo kusomwa, Naibu Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluochi, alisema kwamba wanawasiliana na wakili wao ili kukata rufaa kwa kuwa wanaona kama walimu nchini hawana haki.
Mgomo waanza
Awali, mgomo usiokuwa na kikomo ulioitishwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), jana ulianza kwa kishindo na kulitikisa taifa, baada ya walimu wa shule za msingi na sekondari nchini kote, kugoma kuingia madarasani wakiishinikiza serikali iwalipe madai yao.
Wakati mgomo huo wa pekee na wa aina yake ukianza jana, wanafunzi wa baadhi ya shule za msingi jijini Dar es Salaam, waliandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, kushinikiza serikali iwalipe walimu madai yao ili wapate huduma kutoka kwa walimu wao.
Mgomo huo ulianza jana licha ya serikali kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutoa vitisho mbalimbali, ikiwamo kufungua kesi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, kujaribu kuzuia mgomo huo kwa mara ya pili.
Hata hivyo, habari kutoka kwa waandishi wetu walioko katika mikoa mbalimbali nchini, zinaarifu kuwa pamoja na vitisho hivyo vya serikali, walimu katika shule za msingi na sekondari, jana walianza mgomo huo kwa kishindo na kulitikisa taifa.
Jijijni Dar es Salaam, mgomo huo ulifanyika baada ya walimu wa shule zilizoko katika wilaya ya Temeke, kushuhudiwa wakiwa wamekaa katika vikundi chini ya miti wakipiga soga, huku baadhi ya wanafunzi wakicheza mpira, wengine kukimbizana na kurushiana mabegi na wengine wakitumia muda mwingi kula `Ice cream` na maandazi.
Shule za msingi zilizoshuhudiwa walimu wakigoma kuingia madarasani, ni pamoja na Muungano, Bongoyo, Oysterbay, Msimbazi Mseto, Msimbazi, Mugabe, Boma na Mkoani wakati za sekondari, ni Salma Kikwete, Turiani, Manzese, Yusufu Makamba na Mugabe.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya walimu wa shule hizo walisema hawataingia madarasani mpaka serikali imalize kuimba wimbo wake walioutunga waliouita `Kuhakiki`.
``Mimi siwezi kamwe kuingia tena darasani mpaka nipewe changu.
Nadai laki tisa...badala ya serikali kutulipa, imebuni wimbo wao mtamu unaosema inahakiki majina.
Kuhakiki gani kusikoisha... huu ni uzushi mtupu,`` alisema mmoja walimu.
Mwalimu mwingine alisema anaona kilichobaki sasa ni kwenda kushiriki katika kampeni ya Operesheni Sangara inayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yenye lengo la kuleta fikra za mabadiliko.
Alisema hata kama serikali itawalipa malipo yao, itamchukua muda kurudisha hisia na upendo wa kazi yake ya ualimu kama mwanzo.
``Tunachofanya sisi, tunashika mapembe wengine wanakamua... inawezekana vipi sisi walimu kupewa haki yetu inachukua muda mrefu na usumbufu mkubwa, lakini mapesa mengine yapo huko Hazina wajanja wachache wanayachota kiulani,`` alisema mwalimu mwingine kwa jaziba.
Wengine wagoma kiujanja
Uchunguzi pia umebaini kuwa katika shule nyingi, baadhi ya walimu wakuu walikuwa wakidai kuwa hakukuwa na migomo na kwamba, kila kitu kinakwenda sawa, lakini walipoulizwa wanafunzi na walimu wa kawaida, walikiri kuwapo kwa mgomo.
Kwa mfano, Nelson Patrick, ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Bongoyo, alisema hakuna mgomo shuleni kwake na walimu wote walifika na kuingia madarasani kama kawaida ila wanachosubiri, ni utekelezaji wa ahadi ya serikali kuwalipa.
Lakini mwandishi alipozungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, walisema tangu asubuhi, ambapo walitakiwa kuwa wameshasoma Hisabati, Kiingereza na Kiswahili, hakuna somo lililofundishwa.
Hadi mwandishi anafika shuleni hapo saa 5:00 asubuhi, hakukuwa hata mwalimu mmoja aliyekuwa ameingia kufundisha somo lolote kati ya masomo hayo.
Wanafunzi, Judy Maghembe, Kura Kasembe na Miriami Nyarali, walikiri kutofundishwa somo hata moja tangu asubuhi licha ya kuwapo na walimu wao shuleni hapo wakipiga soga na kuongea na simu zilizoaminika ni za muda wa bure kutokana na kutumia muda mrefu kuzungumza.
Wanafunzi Dar waandamana
Katika hatua nyingine, wanafunzi wa shule za msingi Tabata, Mtambani na Jaica, jana waliandamana hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kushinikiza serikali ilipe madai ya walimu wao.
Wanafunzi hao mbali na kutaka walimu walipwe madai yao, pia walikuwa wakilalamikia kitendo cha kutofundishwa sambamba na baadhi ya walimu kutowafundisha kwa visingizio mbalimbali.
Katika madai yao, wanafunzi hao walisema baadhi ya walimu wao wamekuwa wakiwachangisha fedha za ulinzi na kulipia mitihani, jambo ambalo walidai utekelezaji wa hayo yote umekuwa hafifu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, aliwapokea wanafunzi hao na kuwataka warudi shuleni kwao akiahidi kuwa tatizo lao litafanyiwa kazi haraka iwezekanvyo.
Aliongeza kuwa tayari serikali imeshatenga zaidi ya Shilingi biloni moja kwa ajili ya madai ya walimu wa Dar es Salaam.
``Serikali imeshatoa fedha na zimeshapelekwa mikoani na moja ya mikoa hiyo ni huu hivyo kuanzia sasa wala msijali walimu wenu watalipwa,`` alisema Kandoro.
Rukwa waitikia wito kugoma
Naye Juddy Ngonyani anaripoti kutoka Sumbawanga kuwa takribani asilimia 70 ya walimu wa shule za msingi na Sekondari mkoani Rukwa wameunga mkono mgomo ulioitishwa na CWT kwa lengo la kuishinikia serikali kuwalipa madai yao.
Gazeti hili limetembelea baadhi ya shule katika Manispaa ya Sumbawanga na kujionea wanafunzi hao wakiwa nje ya madarasa yao tangu asubuhi kwa madai kuwa walimu wao hajafika shuleni na waliopo hawajaingia madarasani.
Shule zilizotembelewa ni pamoja na shule za msingi za Mwenge A na B, Chanji, Kizwite, Chemechem, Majengo na Jangwani na Sekondari ya Kanda, Mazwi, na shule ya Kutwa Sumbawanga.
Katika shule ya Sekondari ya Kanda, gazeti hili limefika na kukuta hakuna mwalimu yeyote aliyefika shuleni hapo huku wanafunzi wakiwa nje wamekaa hawana la kufanya.
Katika shule ya msingi ya Jangwani Mwalimi, Mkuu wa shule hiyo, Moris Kibona, alisema kuwa walimu wameripoti kazini kama kawaida asubuhi ingawa walimu hao hawakuingia madarasani isipokuwa wale wanafundisha darasa la kwanza.
Akizungumza na Nipashe shuleni hapo, Mwalimu Mary Kameme, alisema kuwa hawajafurahishwa na kitendo cha kugoma kwa kuwa kinawaathiri wanafunzi, lakini akasisitiza kuwa ni lazima serikali itambue kuwa kama walimu wamefikia hatua ya kugoma basi inamaanisha wamechoshwa na hali iliyopo.
Wanafunzi waathirika
Kwa upande wao wanafunzi Herriet Matala na Raymond Ng`anga wa shule hiyo ya msingi Jangwani wamekiri kuathirika kimasomo na mgomo huo ambapo wenzao wengine ilikuwa wafanye mitihani ya darasa la nne, lakini hawajafanya kutokana na mgomo.
Hata hivyo, wanafunzi hao hawakusita kuiomba serikali kuwaangalia walimu wao kimaslahi kwani bila walimu wanafunzi hawatasoma na hivyo taifa zima litaendelea kuathirika na migomo hiyo ya walimu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwennge \'A Gilbert Mwangosi, alisema kuwa ``Nimefika shuleni hapa kwa kuchelewa kwani leo nimekuja kwa mguu kwani sikuona sababu ya kuchoma mafuta yangu ya pikipiki na kuwahi shule wakati leo walimu tunaanza mgomo nchi nzima.
Alisema kuwa lengo la kufika shuleni hapa ni kuangalia usalama wa wanafunzi kwani wengi wao ni wadogo hivyo wanaweza kupigana au kutupa tatizo lolote pasipokuwa na mtu mkubwa wa kuwaangalia.
Dodoma nako wasoma
Naye Mary Edward kutoka Dodoma anaripoti kuwa baadhi ya walimu katika shule mbalimbali za msingi na mkoani Dodoma wamegoma kuingia madarasani wakishinikiza serikali kuwalipa madai yao.
Nipashe ilitembelea baadhi ya shule za Manispaa ya Dodoma na kukuta walimu katika shule hizo wakiwa wamekaa maofisini, huku wanafunzi wakiwa nje ya madarasa wakicheza.
Mmoja wa walimu katika shule ya msingi ya Makole iliyopo Manispaa ya Dodoma ambaye hakutaka jina lake lijatwe gazetini, alisema wametii amri ya Rais wao ya kuanza mgomo huo.
Alisema pamoja na serikali kutangaza kuwa wameanza kuwalipa walimu, lakini hawawezi kuamini moja kwa moja kauli hiyo kwa kuwa mara nyingi wamekuwa wakidangwanywa.
``Hii si mara ya kwanza wa serikali kutufanya sisi kama watoto,..kila wanaposikia kuwa tunaanza mgomo wanatuambia kuwa madai yetu yanashughulikiwa, lakini tunaporejea madarasani, mambo huwa ni yale yale, hakuna kinachoendelea, sasa na sisi tumefika wakati tumechoka,`` alilalamika mwalimu huyo.
Katika Shule ya Msingi ya Amani walimu walikutwa wamekaa nje ya ofisi zao, huku wanafunzi wakiwa madarasani bila ya kufundishwa.
Walipoulizwa kwa nini hawajaingia madarasani, mmoja wa walimu ambaye alikataa kutaja jina lake alisema ``Unajifanya kutuuliza kwani we hujui kuwa leo walimu wanaanza mgomo wao, mwenye macho haambiwi tazama,`` alijibu mwalimu huyo kwa hasira.
Mgomo huo pia umejitokeza kwenye shule ya Msingi ya Mlimwa B, Chamwino A na B, Ipagala, Hazina na shule ya msingi ya Kiwanja cha Ndege.
Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Dodoma, Flatel Kwahison, alipoulizwa kuhusu mgomo huo alisema, taarifa aliyokuwa nayo ni kwamba zipo baadhi ya shule zilizogoma na zingine zinaendelea na kazi kama kawaida.
Hata hivyo, alisema hakuwa na idadi na majina ya shule hizo huku akimtaka mwandishi wa habari hizi asubiri hadi atakapowasiliana na wakuu wa shule hizo na kumpa majibu baadaye.
Wakati walimu hao wakianza mgomo habari kutoka Wilaya ya Mpwapwa zinaeleza kuwa walimu wilayani humo wamesita kuanza mgomo kwa kuhofia Waziri Mkuu ambaye ameanza ziara yake jana ya kukagua shughuli za maendeleo.
Mmoja wa Maafisa wilaya humo ambaye hakutaka jina lake litajwe aliongea kwa njia ya simu na Nipashe kuwa ziara hiyo imeleta hofu kwa walimu pamoja na baadhi ya watendaji ambao walitoa matangazo kwa shule zote wakiwataka walimu kutogoma hadi ziara hiyo itakapomalizika.
Afisa Elimu Wilaya ya Mpwapwa hakuweza kupatikana kwenye simu kuzungumzia mgomo.
Mbeya watupiana lawama
Naye Thobias Mwanakatwe anaripoti kuwa Mbeya mgomo wa walimu uliotangazwa na CWT umewachanganya walimu mkoani hapa ambapo baadhi wamekitupia lawama chama hicho kwa kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa jinsi ya kuendesha mgomo huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe ilipotembelea shule kadhaa zilizopo Jijini Mbeya, walimu hao walisema CWT imewachanganya kutokana na kushindwa kuweka utaratibu mzuri wa kugoma hali ambayo imesababisha washindwe namna ya kugoma.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Sisimba, Ephata Mbise, alisema CWT kimewaacha walimu njia panda kwa sababu hakijaweza kufanya mawasiliano mazuri na walimu ya namna ya kuendesha mgomo huo.
``Hatuna barua wala mawasiliano yoyote kutoka ofisi ya CWT namna ya kugoma, kitu ambacho tunaona tumeachwa njia panda,`` alisema.
Mbise alisema hayo wakati akiongea na Nipashe ofisini kwake na kubainisha kuwa kutokana na hali hiyo hakuna mgomo.
Hata hivyo, wakati Mwalimu Mkuu huyo wa shule akisema hakuna mgomo, walimu wa shule hiyo ambao walikutwa na Nipashe wakiwa ofisini, walisema mgomo upo pale pale hawataingia madarasani hadi serikali itakapowalipa madai yao.
Walimu hao ambao walikataa kutaja majina yao, walisema wamelazimika kwenda shule kwa sababu tu ya mitihani ya mwisho wanayoiandaa, lakini hata hivyo, baada ya mitihani hiyo kumalizika wataendelea na mgomo kama kawaida.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Azimio, Gedson Swetala, alisema mgomo haueleweki upo kama haupo kwa sababu hakujawekwa utaratibu mzuri wa namna ya kushiriki.
Hata hivyo, uchunguzi huru uliofanywa na Nipashe katika shule kadhaa za Jiji la Mbeya, umebaini kuwa walimu pamoja na kwenda kazini kama kawaida, bado hawakuingia madarasani ingawa walipoulizwa walitoa maelezo kuwa ni kwa sababu wanajiandaa na mitihani.
Katika baadhi ya shule za jijini hapa, wanafunzi wengi wameonekana wakicheza katika maeneo ya shule huku walimu wakiwa katika ofisi zao hali inayoonesha kuwa wamegoma kiujanja.
Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Juma Kaponda, akizungumza na Nipashe kwa simu akiwa Tukuyu, alisema amewatuma watu wa kufuatilia kila shule kama kuna walimu waliogoma.
``Nimewatuma watu wajaribu kupita kila shule kuangalia kama wamegoma, mimi nipo Tukuyu kwa kazi maalum, baadaye nikipewa taarifa nitakujulisha,`` alisema Kaponda wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Naye Mwenyekiti wa CWT, wilaya ya Mbarali, Jailos Temba, akizungumza na Nipashe kwa simu alisema walimu katika wilaya hiyo wamegoma kama kawaida hadi hapo serikali itakapowalipa madai yao wanayodai.
Temba alipoulizwa kuhusu malalamiko ya walimu kwamba CWT imeshindwa kuweka utaratibu mzuri wa kugoma, alisema hilo siyo kweli kwani chama hicho kimetoa taarifa kupitia vyombo vya habri ambapo kila mwalimu alifahamu kuwa mgomo utaanza Jumatatu.
Mkurugenzi Mbeya: Fedha zimeletwa
Kwa upende wake, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Elizabert Munuo, alisema fedha kwa ajili ya kuwalipa walimu hao zimekwisha kuletwa na kwamba taratibu za kuwalipa zinaandaliwa na Halmashauri.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa wilaya kuhakikisha fedha za walimu zilizopelekwa katika halmashauri hizo zinalipa haraka.
Ufisadi mkubwa madai walimu
Naye Richard Makore anaripoti kuwa serikali imebaini ufisadi mkubwa katika zoezi la kuhakiki madai ya walimu na kusema kuwa kama hali hiyo isingeushtukia mapema pangeweza kutokea EPA nyingine siku za usoni.
Kwa mujibu wa habari za uhakika kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa wastani kila siku madai wanayohakiki wanabaini zaidi ya Sh. milioni 80 ambazo zingelipwa hewa.
``Hapa kama tungeingia kichwa kichwa halafu baadaye akaja mkaguzi wa mahesabu ya ndani wizara ingeonekana imetafuna fedha kama zile za EPA na sisi viongozi tuliopo ndiyo tungejibu,`` alisema mmoja wa maofisa wa serikali ambaye hakutaka kuandikwa jina lake.
Kadhalika, ofisa huyo alisema, kuanzia wiki iliyopita serikali ilianza kuwalipa walimu wa sekondari na wale wa shule za msingi ambao wapo chini ya Katibu Mkuu.
Akizungumza na Nipashe ofisa huyo alisema, uhakiki wa mwishoni mwa wiki ulionyesha kuwa majina 100 ya walimu wanaoidai serikali yalikataliwa baada ya kuonekana ni hewa. (SOURCE: Nipashe, 2008-11-18 15:06:48
Na Hellen Mwango na Joseph Mwendapole)
Tuesday, 18 November 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment