Friday, 28 November 2008

EPA: Mramba, Yona 'ndani'

Mramba, Yona wadaiwa kuathirika kisaikolojia

Wakati Basil Mramba na Daniel Yona wanaokabiliwa na mashitaka ya kutumia vibaya madaraka yao, wakiendelea kusota katika gereza la Keko kwa siku ya nne sasa, mawakili wao watetea wamedai kuwa wateja wao wameathirika kisaikolojia kutokana na masharti magumu ya dhamana.

Kiongozi wa jopo la mawakili wanaowatetea washitakiwa hao ambao walikuwa mawaziri waandamizi wa serikali ya Awamu ya Tatu, Joseph Thadeo, jana alidai kuwa wameamua kwenda Mahakama Kuu kupinga masharti magumu ya dhamana yaliyotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hezron Mwankenja.

Alidai kuwa kiasi ambacho wateja wao wameshitakiwa nacho ni Sh. bilioni 11.75 na kwa mujibu wa masharti ya dhamana kwa pamoja wangetakiwa watoe nusu ya kiasi cha fedha hizo ambazo ni Sh bilioni 5.87 ambazo ni Sh bilioni 2.97 kwa kila mteja.

Alidai kinyume chake Mahakama iliwataka kila mmoja kulipa Sh bilioni 3.9 kwa pamoja ni sawa na Sh bilioni 7.8

Maombi ya kupinga masharti ya dhamana yanaanza kusikilizwa leo chini ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njengafibili Mwaikugile.

Mramba na Yona walifikishwa mapema wiki hii katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Hezron Mwankenja na kusomewa jumla ya makosa 13 yakiwamo ya kutumia vibaya madaraka yao ambayo yaliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.75.

Baada ya washtakiwa kusomewa mashitaka yao, mahakama ilitoa masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na washtakiwa hao kujidhamini kwa Sh. bilioni 7.8, ambapo kila mmoja alipaswa kulipa Sh. bilioni 3.9.

Washitakiwa pia walitakiwa kuwasilisha hati za kusafiria na walitakiwa wasitoke nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama hiyo.

Baada ya mahakama kutoa masharti hayo, mawakili wa upande wa utetezi hawakuridhika na uamuzi huo na waliwasilisha barua ya kuomba mwenendo wa uamuzi wa dhamana.

Mawakili hao waliomba mwenendo wa uamuzi huo uchapishwe kwa madhumuni ya kutaka kuupinga.
Juzi mawakili hao walionekana katika harakati zao Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kujaribu kuwatoa wateja wao katika gereza la Keko ambako wanashikiliwa.

Mawakili wa washitakiwa wanadai kwamba kiwango cha dhamana kilichowekwa na Mahakama ya Kisutu ni kubwa mno hivyo kuwaathiri kisaikolojia wateja wao.

Wakati wa kusomewa mashitaka, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Joseph Ole, aliwasomea mashitaka yao akidai kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri walitumia vibaya madaraka yao.

Ilidaiwa kuwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kuipatia mkataba wa kukagua uzalishaji wa dhahabu kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza na kampuni yake tanzu Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation, kinyume cha sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2002 na ile ya Madini ya mwaka 2002.

Katika shitaka la pili, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kukagua madini ya dhahabu kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Ole aliendelea kudai kuwa, katika shitaka la tatu wote wawili wanadaiwa kuwa kati Machi na Mei mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao kwa kumualika Dk. Enrique Segura wa M/S Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation kuja kusaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kabla Timu ya Majadiliano ya serikali haijaanza kulifanyia kazi suala hilo.

Katika shitaka la nne, kati ya Machi na Mei mwaka 2005, washitakiwa wanadaiwa kuwa walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kukaidi kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali suala la kodi kama ilivyopendekezwa na Timu ya Serikali ya Majadiliano, jambo ambalo lilisababisha mkataba uongezwe wa miaka miwili bila kupitishwa na Timu ya Majadiliano.

Shitaka la tano, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Mramba Oktoba 10, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha alidharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kutokutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Katika shitaka la sita, Mramba anadaiwa kati ya 18 na 19 Desemba mwaka 2003, akiwa Waziri wa Fedha, alitoa kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.
Katika shitaka la saba, Mramba anadaiwa kuwa Desemba 19, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Ole aliongeza kuwa shitaka la nane, Oktoba 15, mwaka 2004 akiwa Waziri wa Fedha alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Shitaka la tisa, Mramba anadaiwa kuwa kati 14 na 15 Oktoba 2004, akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la 10, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la 11, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume cha mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka 12, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005 wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11, 752,350,148.00.

Katika shitaka la mwisho, Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 na 2007 akiwa Waziri wa Fedha kwa makusudi alishindwa kuwa makini au kutotimiza wajibu wake alisaini vibali vilivyotajwa katika mashitaka yaliyoelezwa hapo juu, kuruhusu kampuni hiyo kutokulipa kodi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.75.

Washitakiwa kwa nyakati tofauti walikana mashitaka yote.

Hata hivyo, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba hauna pingamizi la dhamana dhidi ya washitakiwa. Kesi yao itatajwa Desemba 2, mwaka huu. (SOURCE: Nipashe, 2008-11-28 10:25:32
Na Joseph Mwendapole)
.........................................................................

Katika hatua nyingine, (mwandishi wa Majira anaripoti kuwa) leo Mahakama Kuu itasikiliza maombi ya Bw. Mramba na Yona ya kuitaka Mahakama Kuu iingilie kati kile watuhumiwa hao wanacholalamikia kuwa ni masharti magumu ya dhamana waliyowekewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Watuhumiwa hao kupitia mawakili wao waliwasilisha rasmi maombi yao hayo jana kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vilivyo karibu na watuhumiwa hao, rufaa hiyo itasikilizwa leo ambapo vigogo hao watawasilisha hoja za kupinga masharti ya dhamana kama yalivyotolewa na Hakimu Hezron Mwankenja wa Kisutu.

Mahakama hiyo iliwataka watuhumiwa hao kila mmoja kujidhamini kwa sh. bilioni 3.9 ambapo katika kesi ya msingi, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.

Bw. Mramba na Bw. Yona walifikisha mahakamani hapo juzi wakikabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo matumizi mabaya ya ofisi, madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Washitakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Hezron Mwankenja anayesikiliza kesi hiyo.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Joseph Ole, aliwasomea mashitaka watuhumiwa hao mapema wiki hii alidai kuwa, kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa kukagua kampuni za madini nchini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba na kampuni tanzu kuzalisha madini ya dhahabu kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mramba na Yona wanadaiwa kuwa Mei 28, mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma jijini Dar es Salaam, wakiitumikia serikali katika nafasi za Uwaziri wa Fedha na Nishati na Madini, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mikataba ya kuiongezea kampuni hiyo muda wa miaka miwili wa kuendelea kuzalisha madini kuanzia Juni 2005 hadi Juni 2007 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Ole aliendelea kudai kuwa, katika shitaka la tatu wote wawili wanadaiwa kuwa kati Machi na Mei mwaka 2005 wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao kwa kumualika Dk. Enrique Segura wa M/S Alex Stewart ( ASSAYERS) Government Business Corporation kusaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili kabla timu ya majadiliano ya Serikali kulifanyia kazi suala hilo.

Katika shitaka la nne, kati ya Machi na Mei mwaka 2005, washitakiwa wanadaiwa kuwa walitumia nyadhifa zao vibaya kwa kukaidi kupeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali suala la kodi kama ilivyopendekezwa na Timu ya Serikali ya Majadiliano, jambo ambalo lilisababisha mkataba uongezeke kwa miaka miwili bila kupitishwa na timu ya majadiliano.

Shitaka la tano, ilidaiwa kuwa mshitakiwa Mramba Oktoba 10, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha alidharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kutotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Katika shitaka la sita, Mramba anadaiwa kati ya 18 na 19 Desemba mwaka 2003, akiwa Waziri wa fedha, alitoa kibali namba GN 423/2003 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume na mapendekezo yaliyopendekezwa na TRA.

Katika shitaka la saba, Mramba anadaiwa kuwa Desemba 19, mwaka 2003 akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka vibaya kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Ole, aliongeza kuwa shitaka la nane, Oktoba 15, mwaka 2004 akiwa Waziri wa Fedha alitoa kibali namba GN 497/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.

Shitaka la tisa, Mramba anadaiwa kuwa kati 14 na 15 Oktoba 2004, akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 498/2004 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la 10, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, mwaka 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 377/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kinyume na mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la 11, Mramba anadaiwa kuwa Novemba 15, 2005 akiwa Waziri wa Fedha alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa kibali namba GN 378/2005 kilichotoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.

Katika shitaka la 12, Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005 wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia Serikali hasara ya Sh. 11, 752,350,148.00.

Katika shitaka la mwisho, Mramba anadaiwa kuwa kati ya 2003 na 2007 akiwa Waziri wa Fedha kwa makusudi alishindwa kuwa makini au kutotimiza wajibu wake alisaini vibali, kuruhusu kampuni hiyo kutokulipa kodi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 11.7. (source: majira 28/11/2008. Mwandishi: Rabia Bakari)

1 comment:

MOSONGA RAPHAEL said...

Rais Kikwete awatisha vigogo wa Richmond

*Mramba, Yona wamefungua njia
*Lowassa,Msabaha, Karamagi kupona?

KUFUNGULIWA mashitaka dhdi ya waliokuwa mawaziri waandamizi wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Basil Mramba na Bw. Daniel Yona ambao wote wamehusishwa na kuliingizia taifa hasara, kunaelezwa kuwa kumewatisha vigogo wa Serikali ya Awamu ya Nne waliohusika katika kashifa nyingine iliyotikisa taifa ya Richmond.

Katika kashifa hiyo ya Richmond, kama yalivyo mashitaka dhidi ya Mramba na Yona, ripoti ya Kamati ya Bunge ilibaini Taifa kupata hasara kubwa kwa kugharamia mkataba feki wa kufua umeme uliopewa kampuni feki ya Richmond LLC iliyojieleza kutoka Marekani, huku shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiathirika nchi nzima baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza matakwa ya mkataba kwa wakati.

Vyanzo vyetu vya kuaminika, vinasema kufanana kwa aina na kiwango cha hasara ambacho Taifa liliipata kupitia sakata la Richmond na aina ya mashitaka ambayo akina Mramba na Yona wamefunguliwa kutokana na jinsi walivyoshughulikia suala la kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS), kunaashiria kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imedhamiria kuwaburuta kortini vigogo wengi zaidi waliohusika kwa namna moja au nyingine katika miradi au uamuzi ulioliingizia hasara Taifa.

" Msingi wa hofu ya hawa jama wa Richmond kwa msimamo usiotabirika wa Kikwete ni jinsi kina Mramba walivyoburutwa kortini. Sasa wanahaha kuona jinsi gani watajinasua iwapo uamuzi ujao utakuwa dhidi yao. Kila unapoyaangalia mashitaka ya Mramba na Yona unaiona kabisa hati ya mashitaka ya wale jamaa zetu wa Richmond," kilisema chanzo chetu.

Miongoni mwa vigogo wa Serikali ya Awamu ya Nne walioguswa katika sakata hilo la Richmond ni Waziri Mkuu aliyestaafu, Bw. Edward Lowassa ambaye ushahidi wa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dkt. Harrison Mwakyembe, ingawa haukumkuta na hatia ya moja kwa moja ya kuamuru Richmond kupewa mkataba huo, Kamati ilieleza "kuyaona mawasiliano yake ya karibu na Wizara ya Nishati na Madini wakati wa mchakato wa kuichukua Richmond."

Bw. Lowassa kwa mujibu wa ushahidi uliopo ndiye aliyeunda Kamati ya Makatibu Wakuu iliyokuwa na kazi ya kuunda timu ya wataalamu katika kuhakikisha kuwa inapatikana kampuni yenye uwezo wakati huo sehemu kubwa ya taifa likiwa kizani.

Ni katika utendaji wake Kamati hiyo ya Makatibu Wakuu iliyoundwa na Lowassa ndipo mwishowe ilipopatikana Richmond, kampuni iliyokuja kubainika kuwa ililaghai juu ya masuala kadhaa juu ya uwezo wake wa kiufundi na kifedha huku Kamati ikibaini pia kuwa kuna vigogo "walioamua kufa, lakini wahakikishe Richmond inapata mkataba huo."

Iwapo Serikali ya Kikwete itaamua kwenda mbali zaidi kuhusu Lowassa aliyeamua kujiuzulu kutokana na kashifa hiyo huku akionesha kutoridhika na uchunguzi wa Kamati ya Bunge, ni suala la kusubiri muda, kimedokeza chanzo chetu.

Kisheria, Lowassa hana kinga ya kutoshitakiwa kwani wakati ibara ya 46 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiweka bayana kuwa Rais hawezi kushitakiwa akiwa madarakani na hata baada ya hapo kwa makosa aliyoyatenda yawe ya daawa (madai) au jinai kwa kufuata madaraka yake ya kisheria, katiba hiyo hiyo iko kimya kuhusu nyadhifa nyingine za juu Serikalini ikiwemo ya Uwaziri Mkuu.

Lakini wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema ugumu ulioko kwa Kikwete katika kuchukua hatua za mbali zaidi kwa Lowassa si sheria bali uswahiba wao wa muda mrefu katika maisha ya kawaida na kisiasa.

Kikwete na Lowassa wote ni makada wa CCM walioandaliwa vyema tangu siku zao wakiwa wanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kikwete akiwa darasa la mbele katika kitivo cha uchumi, Lowassa akiwa nyuma kidogo katika kitivo cha sanaa, lakini walifahamiana.

Wote baada ya UDSM, walifanya uamuzi mgumu wa kwenda kukitumikia Chama, kisha wote wakaingia jeshini katika nyakati tofauti kabla ya kuingia moja kwa moja katika utawala.

Lowassa pia ndiye aliyekuwa 'mtendaji mkuu' katika kampeni za Kikwete kuanzia mwaka 1995 waliposhindwa kutimiza lengo lao na baadaye mwaka 2005 walipofanikiwa. Rais Kikwete amekiri uswahiba wake huo na Lowassa hadharani zaidi ya mara mbili tangu achukue Urais. Hiki ndicho kikwazo kikuu, wanaeleza wapashaji na hata wasomi wanaofuatilia siasa kwa karibu.

Kigogo mwingine ambaye suala la mashitaka ya kuliingiza taifa katika hasara kupitia mkataba wa Richmond linamgusa ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati mkataba huo ukisainiwa, Dkt. Ibrahim Msabaha.

Kamati Teule ya Bunge imesheheni ushahidi wa jinsi Dkt. Msabaha kwa maagizo kutoka juu yake au yeye mwenyewe jinsi alivyokuwa mara kadhaa akiwaamuru viongozi wa TANESCO.Maagizo yake mengi yalikuja kubainika kukiuka sheria kadhaa za nchi.

Akionekana kuungama yaliyotokea, Dkt. Msabaha aliiambia Kamati Teule ya Bunge kuwa yeye katika mchakato wote huo ni 'Bangusilo,' neno kutoka kabila la Kizaramo lenye maana sawa na au inayokaribiana na 'mbuzi wa kafara.'

Katika mkumbo huo pia aliingia Waziri aliyemfuatia Msabaha katika wizara hiyo, Bw. Nazir Karamagi ambaye kimsingi Kamati Teule ya Bunge haikuona tatizo lake katika kuufanisha mkataba huo bali imesheheni ushahidi wa jinsi alivyokuwa 'akiitetea sana Richmond,' isipokwe mkataba huo hata baada ya kuonekana haina uwezo.

Pia upo ushahidi unaomgusa mmojawapo kati ya Karamagi au Dkt. Msabaha ambao unaonesha jinsi alivyokuwa akifika usiku kwenye ofisi za Richmond bila kujulikana sababu.

Ni Karamagi ambaye sasa imebainika kuwa amenusurika kufikishwa kortini kwa kuliingizia Taifa hasara kupitia mkataba mwingine tata wa madini wa Buzwagi, ambaye katika hili la Richmond alifikia hatua ya kupiga simu akiwa Calgary, Kanada, akiwaagiza viongozi wa TANESCO wahaulishe mkataba kutoka kwa Richmond kwenda kampuni ya DOWANS, ambayo nayo ushahidi uliopo hata Serikalini ilikuwa ni kama pacha wa Richmond, kwa namna nyingi.

Vyanzo vyetu vinapasha zaidi kuwa katika hasara iliyotokana na kashifa ya Richmond wanaweza kuunganishwa viongozi wengi katika timu zilizoundwa na Serikali kuhakikisha inapatikana kampuni yenye uwezo, lakini kikwazo kingine ni jinsi suala hilo linavyowagusa vigogo kadhaa wa Serikali ya Kikwete yenyewe.

"Hizi ni hatua za wazi kuchukuliwa kama sheria zinafuatwa kama zilivyo na kama suala la kina Mramba na Yona lilivyochukuliwa. Lakini bado, inaweza kuchukua muda, zile hatua za nidhamu tu kwa watendaji Serikali hadi sasa bado hakuna hata mmoja aliyetangazwa uamuzi juu yake," kiliongeza chanzo chetu hicho kinachofahamiana na vigogo wengi Serikalini.

Chanco hicho kilipasha kuwa kutokana na kufunguliwa kwa mashitaka yanayofanana na kilichotokea katika sakata la Richmond-kuliingizia taifa hasara, dhidi ya Mramba na
Yona, wengi kati ya wahusika wa Riuchmond wamestuka na kuna harakati za kujipanga kwa lolote, hawauamini msimamo wa Kikwete.

"Zipo harakati zimeanza, wametishika kwa kweli na baadhi yao wanajaribu kuangalia jinsi walivyohusika kwa kuangalia mashitaka ya kina Mramba kuona nao watakuwamo au la," kiliongeza chanzo chetu.

Juhudi za gazeti hili kuwasiliana na viongozi wa idara husika na uchunguzi wa masuala ya jinai nchini ili kuthibitisha iwapo kuna uchunguzi wowote wa kijinai dhidi ya vigogo kadhaa waliohusika kwa namna yoyote katika sakata la Richmond na kama kuna mpango wa kuwafikisha kortini, ziligonga mwamba, wengi wao wakiwa mapumzikoni jana, hawakuwa katika nafasi ya kupokea simu.

Hadi jana pamoja na kuibua kashifa hiyo nzito nchini na kufutwa kwenye orodha ya Msajili wa Kampuni (BRELA), kampuni hiyo ya Richmond kupitia tovuti yake ya www.rdveco.com, ilipofunguliwa na gazeti hili majira ya saa 12:30 jioni, imeendelea kujinasibu na kujitangaza duniani kuwa ilikamilisha vyema sehemua ya megawati 25 za kwanza katika mradi huo wa umeme.

"Mwaka 2006, tulikamilisha Mradi wa Umeme wa Dharua wa Ubungo Dar es Salaam, Tanzania. Tulishughulikia masuala yote ya uendelezaji wa mradi, masuala ya kiuhandisi, ununuzi na ufungaji na uwashaji wa megawati 25 za kwanza za umeme na kuandaa m,aandaliz yote muhimu kwa ajili ya awamu ya pili ya megawati 100 za umeme wa gesi," inasomeka sehemu inayozungumzia miradi ya hivi karibuni kwenye tovuti hiyo ya Richmond.

Utafiti zaidi wa gazeti hili hata hivyo umebaini kuwa mtambo wa kwanza wa megawati hizo 25, tofauti na inavyojinasibu kampuni hiyo, uliletwa nchini wakati DOWANS wameshachukua mkataba na ndio waliolipwa kwa kuusafirisha, kuufunga na kuuzindua.

Msemaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bibi Dorin Mosha alipopigiwa simu na gazeti hili saa 8:27 jana mchana, simu hiyo iliita kwa muda wa sekunde 27 hadi ilipokatika bila kupokewa.

Naye Msemaji wa Wizara ya Sheria na Katiba, ambaye pia huratibu shughuli za mawasiliano katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP), Bw. Omega Ngole naye alipopigiwa simu majira ya saa 9:28 alasiri hakupokea simu.
(kutoka: majira, 01.12.2008 00:13 EAT)