Thursday, 31 January 2008

Saruji kutoka majuu kuingia TZ

Wabongo sasa kupata saruji kutoka majuu

Kutokana na uhaba mkubwa wa saruji unaolikabili taifa, Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, imesema muda si mrefu Wabongo wataanza kupata bidhaa hizo kutoka majuu.

Wizara hiyo imesema imechukua hatua hiyo, baada ya kuona licha ya kuruhusu wafanyabiashara waagize saruji kutoka nchi za Afrika Mashariki, EAC, bado kiasi kinachoingizwa hakikidhi haja, hali inayosababisha bidhaa hiyo kupanda bei kila kukicha.

Akizungumza ofisini kwake, Naibu Mkurugenzi wa Viwanda wizarani hapo Bi. Eline Sikazwe akazitaja nchi zinazotarajiwa kuingiza saruji nchini kuwa ni Afrika kusini, Uarabuni, Hispania, China na Msumbiji.

Amesema tayari mfanyabiashara aliyeomba kuagiza saruji toka Afrika Kusini ameshapewa kibali.

Pia akasema wanawakaribisha watu wenye uwezo kuagiza saruji hata nchi za Ulaya ili kupunguza tatizo la saruji nchini.
Akasema makampuni mengi yamejitokeza na kupeleka maombi wizarani hapo.

Bi. Sikazwe amesema ili kutoa motisha, Serikali imepunguza ushuru kutoka asillimia 45 hadi 25 kwa bidhaa hiyo kwa saruji itakayoingizwa Lengo la punguzo hili ni kutoa motisha ya kuagiza saruji kutoka nchi zote ulimwenguni badala ya kutegemea nchi za EAC ambapo kuna uhaba pia,akasema.

Na kuongeza Upungufu wa saruji nchini, umesababisha kuzorota kwa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na serikali, taasisi binafsi na ile ya wawekezaji.

Vilevile amesema upungufu huo umerudisha nyuma juhudi za wananchi za kujenga nyumba bora kwa ajili ya makazi na biashara.

Bi. Sikazwe akasema kutokana na tatizo hilo, itashindikana
kukamilisha miradi ya Serikali kwa gharama zilizopangwa, kutokana na kuongezeka kwa gharama za saruji.

Tathmini iliyofanyika mapema mwezi uliopita ilionesha kuwa hali ya upatikanaji wa saruji nchini bado haijawa nzuri, jambo ambalo linathibitishwa na bei yake kwa walaji ambayo imeendelea kuwa kubwa, akasema.

Aliongeza kwamba licha ya kufungua milango kwa wafanyabiashara kuingiza saruji toka nchi za EAC ni tani 2,066 tu za bidhaa hiyo ambazo zimeingizwa.

Bi. Sikazwe akasema hilo linatokana na ukweli kwamba nchi kama Kenya na Uganda nazo zina matatizo ya saruji, hivyo kuzitegemea ni sawana kwenda kuomba Jamvi kwenye nyumba yenye kilio.

* SOURCE: Alasiri, 31 Jan 2008
By Simon Mhina
(www.ippmedia.com)

No comments: