Waziri Mkuu kulimwa maswali kila Alhamisi
Kanuni inayotoa ruksa kwa waheshimiwa wabunge kumlima maswali Waziri Mkuu moja kwa moja inaanza kutumika katika mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa mjini hapa.
Kanuni hiyo mpya ni miongoni mwa zile zilizoingizwa katika kitabu cha kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007.
Spika wa Bunge hilo, Mheshimiwa Samwel Sitta amesema kanuni hiyo sasa inaanza kutumika ipasavyo katika mkutano huu wa Bunge unaoendelea mjini hapa.
Spika Sitta amewaambia waheshimiwa wabunge leo asubuhi kuwa ili kutekeleza kanuni hiyo, kila Alhamisi kwa kipindi chote cha Bunge, watapata ruksa ya kumuuliza maswali Waziri Mkuu moja kwa moja.
``Waheshimiwa wabunge kila Alhamisi ndiyo siku ambayo tutakuwa tukimuuliza Waziri Mkuu maswali moja kwa moja ili kutekeleza kanuni yetu ya toleo la mwaka jana inayotutaka tufanye hivyo,`` akasema Mheshimiwa Spika.
Spika amesema hayo wakati akihitimisha kipindi cha maswali na majibu leo asubuhi.
Amesema jioni ya leo Naibu wake, Mhe. Anne Makinda atatangaza utaratibu mzima utakaofuatwa na wabunge wakati wa kumuuliza maswali Waziri Mkuu.
* SOURCE: Alasiri, 31 Jan 2008
By Job Ndomba, Dodoma
(www.ippmedia.com)
Thursday, 31 January 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment