Tuesday, 8 July 2008

Ujenzi: Mamlaka za Usimamizi zimelala?

Pamoja na matukio ya ajali ktk maeneo ya ujenzi hivi karibuni bado ajali zinaendelea kutokea tena kwa sababu zinazoweza kuzuilika kabisa. Inahitaji umakini tu.

Tunao wataalamu (wahandisi na wasanifu majengo) ambao wanaweza kutuondolea matukio ya ajali za kirejareja kama hii iliyosimuliwa hapo chini.

Kanuni za eneo la ujenzi (site) ziko wazi kabisa. Mtu ambaye hahusiki ktk kazi ya ujezi haruhusiwi kurandaranda eneo la ujenzi! Kama kuna mgeni ktk 'site' ni lazima avae mavazi yanayokubalika ikiwa ni pamoja na viatu vigumu (safety boots), na kofia ngumu (helmet). Sina hakika kama ni busara watu (residents) kuishi ktk site kubwa ya ujenzi kama hii (ni hatari) usalama wao unakuwa mashakani.

Pia watengeneza njia za muda ktk 'site' kama vile ngazi ni lazima wazingatie vipimo maalumu vilivyopendekezwa kitaalamu (standards and specifications). Kwa mfano:
-Upana wa ngazi (ktk jengo kama hilo la ghorofa zaidi ya moja) ni lazima uwe sentimeta 120 au zaidi kwa ajili ya watu na kupitisha mizigo (building materials),
-Urefu wa ngazi moja (rise) uwe sm. 15 hadi 16,
-kikanyagio cha ngazi (going) isiwe chini ya sm. 30,
-Kibiyongo ktk ngazi (nose) ni muhimu,
-kingo za ngazi (ballustrade) ni lazima ziwekwe,
-kishikio cha kingo za ngazi (railings) kiwe na urefu wa sm. 90 toka toleo la ngazi na kigusane na ukuta pale penye tambarare la ngazi (landing).
-urefu wa kutoka toleo la ngazi hadi juu (headroom) usiwe chini ya sm. 210 (m. 2.1) (kulingana na (sheria ndogo) bye-law husima)
-kusiwe na takataka zozote au mizigo ktk eneo la kupita watu hii ni pamoja na ngazi
-na kadhalika.

Wahandisi na ma-foreman wanatakiwa kuhakikisha vitu kama hivi vinazingatiwa wakati wote, hakuna cha njia ya mkato wala hakuhitaji fedha za kigeni.

Ajali kama hizi husababishwa na uzembe kazini na hili ni kosa. Wahanga (waliopatwa na ajali kama hizi) wana haki kushitaki wahusika (hasa mwenye jengo) na kudai fidia (under law of tort -negligence, duty of care)!!

...........................................
...........................................
...........................................
Mama Dar nusra afie ghorofani!
(SOURCE: Alasiri, 2008-07-08 17:38:29 Na FRANK MBUNDA, KARIAKOO)
Zikiwa zimepita wiki mbili sasa tangu kuanguka kwa jengo la ghorofa kumi katika mtaa wa Mtendeni eneo la Kisutu ndani ya Manispaa ya Ilala Jijini, jengo jingine la ghorofa tano na ambalo linaendelea kujengwa katika manispaa hiyohiyo nusra limsababishie umauti mama mmoja baada ya kuporomoka toka katika ghorofa ya pili na kuumia vibaya.

Taarifa zimeeleza kuwa, mama aliyepatwa na mkasa huo ni Bi. Aisa Mushi, 44, mkazi wa Kimara Jijini, ambaye alikuwa akipanda ngazi zisizo na kingo za ghorofa hilo linaloendelea kujengwa pale Kariakoo, katika nyumba namba 6 iliyopo katika Mtaa wa Mchikichi.

Bi. Aisa alianguka katika ghorofa hilo lililo na wakazi wanaoendelea kuishi ndani yake huku likiendelea kujengwa, baada ya kukanyaga kokoto za zege wakati akiwa kwenye ngazi ya ghorofa la pili kabla ya kuteleza na kuporomoka hadi chini.

Bi. Aisa alianguka baada ya kuteleza na kukosa kingo za kujishikia kwenye ngazi za ghorofa hilo.

Alikuwa akitoka katika stoo yake ya mali iliyopo katika jengo hilo na kujikuta akiteleza baada ya kukanyaga kokoto za zege zilizoachwa kwenye ngazi mojawapo ya kupandia juu.

Baada ya kukanyaga kokoto hizo, Bi. Aisa alijaribu kujishikiza bila mafanikio, kwani kingo za ngazi za kupandia bado hazijawekwa na matokeo yake ndipo akaanguka na kuumia vibaya.

Hadi sasa, Bi. Aisa angali akihangaikia uzima katika Hospitali ya Agha Khan Jijini ambako amelazwa kwa siku kadhaa sasa, huku akiwa amevunjika baadhi ya viungo vyake ikiwa ni pamoja na mikono.

Mwandishi wa Alasiri alimtembelea Bi. Aisa ili kumjulia hali pale katika Hospitali ya Aga Khan, ambapo katika maelezo yake, akasema mpaka sasa haamini kuwa bado yungali hai.

``Kwa kweli Mungu ni Mwema... nilijua ndo uahi wangu umefikia tamati. Mungu yupo na ninawaomba watu wamrudie yeye,`` akasema Bi. Mushi.

Hivi karibuni, Serikali ilipiga marufuku watu kuendelea kuishi katika majengo yanayoendelea na ujenzi Jijini, hasa baada ya tukio la kuanguka kwa jengo la ghorofa kumi lililokuwa likiendela na ujenzi na kumuua mtu mmoja, huku wengtine kadhaa wakijeruhiwa.

No comments: