(Na George John, Musoma. Majira 04/07/2008)
TAASISI ya Mwalimu Nyerere nchini (MNF), imetoa tamko kuhusu mgogoro wa Zimbabwe ambao umejitokeza kutokana na marudio ya uchaguzi wa Rais na kusema kamwe hoja ya kutaka Rais Robert Mugabe kuachia madaraka haina nafasi katika kurejesha amani nchini humo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa mbele ya waandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo (MNF), Bw. Joseph Butiku.
Bw. Butiku alisema mgogoro huo utatatuliwa tu endapo wahusika wote raia wa Zimbabwe watahimizwa na kushauriwa kukubali kukaa meza moja na kuzungumza kwa amani, ili kuondoa kero kwa pande zote.
Alisema jitihada za upande mmoja kwa kumtuhumu Rais Mugabe na kumtaka kuachia ngazi, si suluhisho la kudumu la matatizo ya Zimbabwe na kutaka Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) na jumuia za kimataifa, kuhimizwa kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na Rais wa Afrika Kusini, Bw. Thabo Mbeki aliyeteuliwa na SADC kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Bw. Butiku alisema chanzo kikuu cha mgogoro huo, si Rais Mugabe, bali ni tatizo la kihistoria, linalotokana na mgogoro wa ardhi ambao haujapatiwa ufumbuzi kwa kipindi kirefu.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisema baada ya mkutano wa pamoja na Watanzania mashuhuri, wasomi na wanasisa na uongozi wa taasisi hiyo uliofanyika wiki iliyopita Dar es Salaam, ilibainika kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro huo, ni kuheshimu uamuzi wa Wazimbabwe bila kuingiliwa kwa lawama za upande mmoja.
Kwa sababu hiyo, alisema hakuna haja ya kutafuta jitihada mpya za suala hilo, bila kutambua jitihada za awali za Rais Mbeki na kuweka mbele maslahi ya wananchi wa Zimbabwe, kwa vile ni nchi huru, bila kutumia nguvu za kijeshi kama inavyodhaniwa na mataifa ya Magharibi.
Alisema tasisi yake inalaani vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini si kwa kumshutumu Rais Mugabe, kwani hata kupora ardhi ya Wazimbabwe pia ni ukiukwaji wa haki hizo, kinyume na makubaliano kati Serikali ya Uingereza na wapigania Uhuru wa Zimbabwe wakati huo, akiwamo Rais Mugabe yaliyofikiwa baada ya nchi hiyo kupata Uhuru huo.
“Watu wanapopigania Uhuru na kuupata, wanatarajia kunufaika na matunda yake na inapotokea kuwekwa vikwazo, lazima wananchi wa nchi husika wakatae na si kumbebesha lawama Rais Mugabe kwani lazima tuangalie misingi ya tatizo kwanza," alisema Bw. Butiku nyumbani kwake mjini hapa.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa vile Rais Mugabe ndiye Rais wa nchi hiyo kwa sasa, ni kweli lawama hizo zinaweza kusukumwa kwake, ili kutafuta ufumbuzi, lakini si kumhukumu kwa manufaa ya wachache.
Bw. Butiku alisisitiza kuwa hoja ya sasa kwa mataifa hayo ni kuhimiza mazungumzo kati ya Serikali na wapinzani, ili kuheshimu Uhuru wa demokrasia wa Wazimbabwe, kuamua na kusuluhisha masuala yao, bila kuingiliwa.
Friday, 4 July 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment